Na Lydia Churi- Mahakama, Songwe
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ametoa wito kwa wadau wa Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) katika kazi zao ili kuendana na Mahakama ya Tanzania ambayo imeshaanza
matumizi hayo na ifikapo mwaka 2025 kazi zake zote zitakuwa zikifanywa kwa mtandao.
Akizungumza na wadau wanaofanya kazi na Mahakama
wakati akihitimisha ziara ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Songwe,
Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania haiwezi kuwa ya mtandao kama wadau wake hawataingia
kwenye matumizi hayo kwa kuwa mnyororo wa upatikanaji wa haki unawahusisha
wadau wote.
“Ukiiangalia ramani ya Mkoa wa Songwe utagundua kuwa
kwa jinsi ilivyo, wananchi wengine wa mkoa huo watalazimika kufuata huduma za
Mahakama kwa umbali mrefu hivyo Tehama ndiyo jibu”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza
wadau hao kuwekeza kwenye Tehama.
Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa
kwenye miundombinu ya Tehama ambapo uwekezaji huo ukitumiwa vizuri utauwezesha
Mhimili huo kulingana na Mahakama nyingine duniani zenye maendeleo makubwa
katika matumizi ya Tehama ifikapo mwaka 2025.
“Mahakama tumefanya uwekezaji mkubwa katika Teknolojia,
ili tufikie Mapinduzi ya nne ya viwanda tutasukumwa na matumizi ya Tehama”,
alisema Jaji Mkuu.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili za mkoa wilaya
za mkoa wa Songwe, Jaji Mkuu aliwataka wajumbe hao kusimamia Maadili na nidhamu
ya Mahakimu kwa kuwa wajumbe hao ni kiungo muhimu kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama
na wananchi.
“Kuweni karibu na Mahakama hapa Songwe na msome
miongozo mbalimbali inayotolewa na kuielewa ili iwasaidie katika kuwalea
Mahakimu wetu katika maadili yapasayo na pia kufahamu mipaka ya Mahakama pale mnapotekeleza
majukumu yenu kwa mujibu wa sheria”, alisema Jaji Mkuu.
Aidha aliwashauri Wenyeviti wa Kamati za Maadili za
Mkoa na wilaya kuitisha vikao kwa mujibu wa sheria ili kujadili changamoto
mbalimbali za Mahakama ikiwemo ya ukosefu wa majengo na kutoa mapendekezo ya
maeneo yanayofaa kujengwa majengo mapya ya Mahakama.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza
ziara yao katika mikoa ya Iringa, Njombe,Mbeya na Songwe mwishoni mwa wiki.
Lengo la ziara hiyo ya siku tano kwenye mikoa hiyo ni kuitangaza Tume ya
Utumishi wa Mahakama pamoja na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za
Mikoa na Wilaya na wadau wa Mahakama.
Mdau wa Utoaji haki akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau hao uliofanyika mwishoni mwa Wiki mkoani Songwe.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Utoaji Haki uliofanyika mwishoni mwa Wiki mkoani Songwe.
Wadau wa Utoaji haki wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau hao uliofanyika mwishoni mwa Wiki mkoani Songwe.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe ambalo pia litajumuisha Mahakama ya wilaya ya Songwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni