· Aipongeza Mahakama kwa maboresho, hususani matumizi ya TEHAMA
Na.
Mary Gwera na Ashura Amiri, [MSJ]
Balozi
Mstaafu wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Wilson Masilingi, ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika, hususani katika eneo la matumizi ya TEHAMA, ambayo
imerahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Balozi
Masilingi ametoa pongezi hizo leo Septemba 15, 2021 alipomtembelea Msajili Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Chuma, na kufanya mazungumzo naye juu ya
suala zima la mabadiliko na maboresho yanayoendelea katika Mahakama ya Tanzania.
“Mahakama
imefanya maboresho mbalimbali katika suala zima la utoaji haki, hivyo ni vyema
kuendelea kutangaza maboresho hayo kwenye vyombo vya habari ili wananchi waweze
kuyafahamu. Sio kwamba nawasifia tu pia mimi mwenyewe ni shuhuda wa maboresho
hayo ambapo nimetumia Mfumo wa Mawakili Tanzania ujulikanao kama ‘TAMS’ na
kufanikiwa kuhuisha leseni yangu ya Uwakili ndani ya muda mfupi,” alisema.
Balozi Masilingi aliongeza kuwa kwa muda mrefu
baadhi ya watu wamekuwa wakielekeza shutuma mbaya kwa Mahakama na kusahau kuwa
kuna mambo mazuri yameshafanyika, ambayo yanahitaji kupongezwa.
“Wakati
sasa umefika wa kupongeza jitihada hizi na maboresho mbalimbali ambayo Mahakama
ya Tanzania imefanya na inaendelea kufanya katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji
haki kwa wananchi inapatikana kwa wakati,” alisema. Aidha,
Balozi Masilingi alishauri watumishi wa umma kuwa wavumilivu, kuheshimu mamlaka
na kuwa waadilifu katika kazi zao.
Kwa
upande wake Msajili Mkuu wa Mahakama alimshukuru Balozi Masilingi kwa
kutembelea Mahakama ya Tanzania na kumwomba kuwa Balozi mzuri wa maboresho aliyoyashuhudia.
“Mimi
nashauri kwamba kutokana na uzoefu ulionao, ni vema ukatumia nafasi ya uwakili kuwasaidia
na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kijamii na
kimahakama,” Mhe. Chuma alimweleza Balozi Masilingi, ambaye baada ya kustaafu
serikalini kama Balozi ameamua kuendelea na Uwakili wa Kujitegemea
Balozi
Masilingi aliwahi kuwa Mtumishi wa Mahakama kama Hakimu ambapo alishika
nyadhifa mbalimbali za kiutawala katika Mhimili huo ikiwemo kuwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi. Kwa upande wa Serikali, Balozi Masilingi amewahi kushika nyazifa
mbalimbali, ikiwemo kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora).
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni