Na Innocent Kansha – Mahakama
Chama cha Wanamichezo wa
Mahakama ya Tanzania, maarufu kama “Mahakama Sports” kimefanya uchaguzi wa viongozi wake wa
ngazi mbalimbali watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ijayo
kwa mujibu wa Katiba.
Akifungua mkutano wa
uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Jijini Dar es Salaam Septemba
11, 2021, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Bw. Anthony Mfaume aliwahakikishia
wajumbe kuwa zoezi hilo limepata baraka zote kutoka Shirikisho la Michezo
nchini (TFF), Uongozi wa Mahakama na SHIMIWI. Aidha, aliwatoa hofu wajumbe kuwa
zoezi hilo lililowashirikisha wajumbe kutoka masjala ndogo zote za Mahakama nchi nzima litaendeshwa kwa uwazi, uhuru bila upendeleo wa aina yoyote.
Mwenyekiti huyo akataja
nafasi zilizokuwa zinawaniwa na wagombea mbalimbali kuwa ni Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Wajumbe wa Kamati Tendaji
na Mjumbe Mwakilishi SHIMIWI Taifa. Aidha uchaguzi huo uliwashirikisha Wanamichezo wapatao 300 ambao ni watumishi wa Mahakama.
Mara baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika kwa nafasi zote zilizokuwa zikiwaniwa na wagombea, Bw. Mfaume kwa mamlaka aliyopewa, akatangaza Bw. Wilson Magero Dede kuwa Mwenyekiti wa Mahakama Sports mara baada ya kupata idadi ya kura 96 na kuwaacha washidani wake, Bw. Alquine Michael Masubo, aliyepata kura 91 na Mhe. Kifungu Mrisho Kariho, aliyeambulia kura 56.
Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Bw. Fidelis Lusenga Choka aliibuka mshindi kwa kupata kura 174 na kumuacha kwa mbali Bw. Fadhil Lameck Mbaga aliyepata kura 76. Bw. Robert Donald Tende alichakuliwa kuwa Katibu Mkuu kwa kupata kura 172 na kumshinda mpinzani wake, Bw. Ismail Ibrahim Lulambo aliyepata kura 67. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu ilikwenda kwa Mwanamama Bi. Theodosia Jackson Mwangoka aliyeibuka kidedea kwa kura 193 na kuwagalagaza wapinzani wake, Bw. Juma Juma Pazi, aliyepata kura 49 na Bw. Julius Leonard Kilimba aliyeambulia kura 9.
Nafasi nyingine
iliyogombaniwa ilikuwa ni ya Mweka Hazina ambapo Bw. Rajabu Dhiwa aliibuka mshindi
kwa kura 152 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, Bw. William Yohana, aliyepata
kura 105. Kulikuwepo na wagombea tisa kwa upande wa nafasi ya Wajumbe wa Kamati Tendaji waliokuwa wanawania nafasi nne. Walioibuka kidedea na idadi ya kura walizopata kwenye mabano ni Bi. Rhoida John Makassy (183), Bi. Judith Yoram
Mwakyalabwe (172), Bi. Mchawi Hussein Mwanamsolo (152) na Bw. Rajabu Said
Mwaliko (140).
Mjumbe Mwakilishi SHIMIWI
Taifa Bw. Shaibu Hassan Kanyochole alipita bila kupigwa baada ya mshidani wake
kujitoa kabla ya uchaguzi kuanza.
Uongozi huo uliochaguliwa utadumu kwa kipindi cha miaka minne madarakani hadi kufikia uchanguzi mwingine. Kwa mara ya mwisho Mahakama Sports ilifanya uchaguzi kama huo
mwaka 2013 na mwaka 2017 zoezi hilo halikufanyika kutokana na Serikali
kuzuia michezo kwenye Wizara na Idara za Serikali.
Wakati akifunga zoezi la uchaguzi huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Pancras, aliwashauri viongozi waliochaguliwa kwenda kuboresha maeneo yenye
mapungufu waliyoyaona katika utawala uliopita na kuwaleta wanamichezo wote
pamoja, kwani michezo ni afya na furaha.
“Umati huu una imani
nanyi, sasa ni muda muafaka wa kuvunja kamati na kambi zenu za uchaguzi,
tuungane tuwe kitu kimoja katika kuwatumikia wanamichezo, kwani lengo la kila mgombea lilikuwa kuimarisha chama, kujenga afya za wachezaji na kulinda
maslahi ya wanamahakama sports”, Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema.
Wanamichezo wa Chama Mahakama Sports wapatao 300, walioshiriki katika uchaguzi huo wakiwa ukumbini tayari kwa kupiga kura kuchagua viongozi wa Chama hicho.
Mmoja wa wajumbe akimuuliza
swali mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mahakama Sports katika uchanguzi huo, uliofanyika
katika ukumbi wa Mahakama Kuu Jijini Dar es salaam Septemba 11, 2021.
Mkurugenzi Msaidizi Utawala
Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Pancras akifunga zoezi la uchaguzi huo na
aliwashauri viongozi na wajumbe (hawapo pichani) waliochaguliwa kwenda kuboresha maeneo yenye mapungufu.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni