Jumatano, 29 Septemba 2021

BARAZA LA ELIMU YA SHERIA LASHAURIWA KUBORESHA MTAALA

Na Stanslaus Makendi – Mahakama Kuu Dodoma

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. George Masaju, amewashauri Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini kutoa michango itakayokuwa chachu ya maboresho ya Mtaala wa Mafunzo ya Sheria ili kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na kwa ufanisi mkubwa.

Akifungua kikao cha siku tatu (3) cha Wajumbe wa Baraza hilo hivi karibuni, kinachofanyika jijini Dodoma, Mhe. Jaji Masaju alisema ni muhimu kufanya mapitio na maboresho ya Mtaala huo wa mwaka 2010 (National Legal Training Curriculum of 2010) katika maeneo mbalimbali ili kujibu mahitaji ya nchi na hivyo kuchagiza maendeleo ya Taifa.

Nawapongeza Viongozi wa Baraza na Mahakama kwa ujumla kwa kuandaa na kuratibu kikao kazi hiki. Naamini michango yenu itakuwa chachu ya kuwa na programu nzuri za Sheria katika Vyuo vyetu ambazo ni msaada katika maendeleo kama Taifa na kuwajenga wahitimu ili wawe na uwezo wa kujiajiri na kutekeleza majukumu yao vizuri katika Sekta ya Umma na binafsi,” aliwaambia wajumbe hao.

Akizungumza katika kikao hicho, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, ambaye ni Katibu wa Baraza la Elimu ya Sheria, aliweka bayana kuwa Mtaala wa Mafunzo ya Sheria nchini wa Mwaka 2010 unaotumika sasa umepitwa na wakati, hivyo unapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa.

Mhe. Sarwatt alibainisha kuwa Mtaala uliopo hauakisi mahitaji ya hali ya sasa ya maendeleo makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), uchumi na biashara za kimataifa pamoja na shughuli zingine za maendeleo, ikiwemo uchimbaji madini, mafuta na gesi.

Kikao cha wajumbe wa Baraza hilo ambacho kilifunguliwa Septemba 27, 2021 na kinatarajiwa kumalizika leo Septemba 29, kimewaleta pamoja wawakilishi kutoka vyuo mbalimbali nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Wawakilishi wengine wametoka Chuo Kikuu Mzumbe (Morogoro na Mbeya), St. Augustine (Mwanza), Jordan (Morogoro), Kampala University, Chuo cha Ushirika – MuCOBS, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Muslim University of Morogoro, Chuo Kikuu cha Iringa, Chuo cha Tumaini Makumira Arusha na Chuo Kikuu cha Ruaha.

Wajumbe wa kikao hicho watakuwa na siku tatu za kuboresha Mtaala huo ili, pamoja na mambo mengine, uweze kuakisi maendeleo ya kiteknolojia na hali ya uchumi wa kisasa na kuweka viwango vitakavyowezesha vyuo vinavyotoa elimu ya Sheria kuwa na muda maalum wa mafunzo ya vitendo vyuoni (Moot court) na kuwa na uwiano mzuri baina ya wanafunzi na walimu.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. George Masaju, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Baraza hilo kinachofanyika Jijini Dodoma. Kushoto ni Mhe. Sharmillah  Sarwatt, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Katibu wa Baraza la Elimu ya Sheria.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini wakimsikiliza mgeni rasmi alipokuwa akifungua kikao hicho.
Mgeni rasmi  (aliyeketi katikati mwenye tai ya rangi ya zambarau) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria. Walioketi kuanzia kushoto ni Mhe. Abdallah Gonzi (Mwezeshaji), Bi. Aisha Sinda na Bw. Silwan Galati Mwantembe (Wawakilishi kutoka TLS), Dkt. Erasmo Nyika (Mwakilishi wa Vyuo Vikuu), Frida Mwera (Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mhe. Sharmillah  Sarwatt, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Katibu wa Baraza la Elimu ya Sheria.
Picha ya pamoja kati ya Mgeni rasmi, Mhe. Jaji Masaju (aliyeketi katikati) na wajumbe wa Sektretarieti ya kikao kazi cha Baraza la Elimu ya Sheria (waliosimama).




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni