Na Innocent Kansha - Mahakama
Uongozi wa Shule ya
Sheria kwa Vitendo umekiruhusu Chama cha Michezo cha Mahakama ya Tanzania,
Mahakama Sports, kutumia viwanja vyake kwa ajili ya kufanyia mazoezi ya michezo
mbalimbali ili kujiandaa na mashindano ya SHIMIWI yanayotarajiwa kufanyika mkoani
Morogoro kuanzia Oktoba 20, 2021 hadi Novemba 2, 2021.
Hayo yalibainishwa leo
Septemba 27, 2021 na Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede, alipokuwa
akizungumzia juhudi zilizofanywa na uongozi wa Chama kwa kushirikiana na ofisi
ya Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala ya Mahakama ya Tanzania katika kutatua changamoto
ya ukosefu wa viwanja vya kufanyia mazoezi.
“Tunaushuru sana Uongozi
wa Shule ya Sheria kwa Vitendo chini ya Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Mhe. Dkt
Zakayo Lukumay, kwa kutoa kibali kutumia viwanja hivi kufanya mazoezi katika
michezo mbalimbali. Inaonekana hata yeye anapenda sana michezo, maana kuna
baadhi ya siku huwa tunashiriki naye katika mazoezi,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
huyo, tayari “program” ya mazoezi inatekelezwa na watumishi wa Mahakama ambao wameanza
kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa
miguu kwa wanaume, mpira wa pete, kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake, riadha
za mbio fupi kwa wanaume na wanawake pamoja na “draft.”
“Kwa hiyo nawaomba wanamichezo
wenzangu kuhudhuria mazoezi kwa wingi ili kujiandaa vema kushiriki katika
mashindano haya ya SHIMIWI,” alisema. Hata hivyo, Bw. Dede alisisitiza kuwa
mazoezi ya michezo mbalimbali kwa watumishi wote wa Mahakama yataendelea mara
baada ya mashindano hayo kumalizika.
Hivi karibuni, Uongozi wa
Mahakama Sports ulikutana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Eliasante Ole Gabriel, ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam
ambapo aliahidi kuwapa ushirikiano ili kuboresha ushiriki katika michezo inayoandaliwa
na sekta mbalimbali hapa nchini.
Hata hivyo, Mtendanji Mkuu huyo aliwataka viongozi hao, kwa kupitia uongozi wa Mahakama ya Tanzania, kuona uwezekano wa kuomba kuwa na viwanja vya michezo katika jiji la Dodoma ili Mahakama Sports iwe na wigo mpana wa kushiriki michezo yote katika mashindano mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni