Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha-Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel, leo amekutana na
viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambapo
amewashauri kubuni miradi itakayowawezesha kupata fedha za kujiendesha.
Viongozi
hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Joaquine De-Mello, walifika katika ofisi ya Mtendaji Mkuu Mahakama ya Rufani
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha na kuwasilisha baadhi ya
changamoto zinazowakabili, ikiwemo Chama hicho kukabiliwa na uhaba wa fedha za kuendesha
shughuli mbalimbali.
‘’Fikirieni
miradi ambayo itawasadia kupata fedha za kuweza kuendesha shughuli mnazozifanya
ili chama kisije kushindwa kujiendesha. Miradi hiyo ikifanikiwa itawasaidia kupata
fedha na kuondokana na utegemezi wa wafadhili mbalimbali’’, Prof. Ole Gabriel alisema.
Aidha,
Mtendaji Mkuu huyo alikishauri Chama hicho kuangalia vyanzo vinavyopelekea vitendo
vya kikatili na unyanyasaji wa kijinsia wanavyofanyiwa wanawake na watoto ili kubaini
mapungufu yaliyopo, hatua itakayowawezesha kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kujiepusha
na vitendo hivyo.
Prof
Ole Gabriel pia alikishauri chama hicho kinapofanya shughuli zake kuwashirikisha
viongozi wa dini na wabunge, hasa wa jinsia ya kike, ambao ni miongoni mwa wadau
muhimu katika kupunguza vitendo hivyo.
Kwa
upande wake, Mhe. Jaji De-Mello, kwa niaba ya TAWJA, alipendekeza suala la jinsia
katika Tume ya Utumishi wa Mahakama kuangaliwa upya ili kuongeza uwakilishi wa
wanawake miongoni mwa wajumbe wa tume hiyo. Akijibu pendekezo hilo, Prof. Ole
Gabriel alikumbushia kuwa swala hilo ni la kikatiba ambalo linapaswa kutazamwa
kwa jicho la kipekee.
Hata
hivyo, Mtendaji Mkuu huyo, ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
alisema kuwa watatafuta namna bora itakayojadiliwa na wadau ili kuongeza uwakilishi
wa kijinsia ambao hautaathiri sheria iliyounda tume hiyo.
TAWJA
ni chama cha Kitaaluma, ambacho hutoa elimu katika maeneno mbalimbali juu ya ukatili
wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto na mambo yanayohusu haki za binadamu, hususani
katika mashule na vyuo na pia hushiriki katika matukio ya kitaifa kama vile Wiki
ya Sheria, Wiki ya Utumishi wa Umma na kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa,
“SabaSaba.”
Mhe.
Jaji De-Mello, ambaye aliambatana na viongozi wengine wa TAWJA alimwelezea pia Mtendaji
Mkuu huyo majukumu mengine ambayo Chama kinafanya kama kuandaa machapisho
mbalimbali ambayo hulenga kuelimisha Umma haki za mtoto, haki za
mwanamke na haki za binadamu kwa ujumla.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni