Na Innocent Kansha - Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, leo Septemba 17, 2021, amekutana na
uongozi wa Mahakama Sports ofisini kwake, Mahakama ya Rufani Jijini Dar es
Salaam na ameahidi kuwapa ushirikiano wa hali na mali ili kuboresha ushiriki
kwenye michezo inayoandaliwa na sekta mbalimbali nchini kwani michezo ni sehemu
ya kujenga afya ya mwili na akili.
Katika mazungumzo yake na
viongozi hao, Prof. Ole Gabriel hakusita kuonesha hisia zake kwa kutamka bayana
kuwa yeye ni mwana michezo na anapenda sana michezo, hivyo atahakikisha
Mahakama ya Tanzania inakuwa na timu bora na zenye ushindani wa kweli katika
michezo mbalimbali.
“Kama mwaka huu
mtashiriki katika michezo ijayo, itategemea na bajeti iliyopo. Hivyo mnatakiwa
kutoa uwakilishi kwenye kila mchezo wenye washiriki wachache. Mwaka ujao
nitashirikiana na viongozi wengine wa ndani ya Mahakama ili kuongeza bajeti kwa
ajili ya kuimarisha ushiriki katika michezo,” alisema.
Hata hivyo, Mtendanji
Mkuu huyo aliwataka viongozi hao, kwa kupitia uongozi wa Mahakama ya Tanzania,
kuona uwezekano wa kuomba kuwa na viwanja vya michezo katika jiji la Dodoma ili
Mahakama Sports iwe na wigo mpana wa kushiriki michezo yote katika mashindano
mbalimbali.
Mwenyekiti wa Mahakama
Sports, Bw. Wilson Dede, alimwambia Mtendaji Mkuu kuwa Mahakama Sports imekuwa
ikishiriki katika michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira
wa wavu pamoja na kuvuta kamba.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
huyo, mwaka 2014 Mahakakama Sports iliposhiriki kwa mara ya mwisho kwenye
michezo ya SHIMIWI ilifanikiwa kunyakua vikombe vitatu katika michezo ya mpira
wa miguu, mpira wa pete na kuvuta kamba, ambapo washiriki walishika nafasi ya
tatu kwa kila mchezo.
Hata hivyo, Bw. Dede
alibainisha changamoto wanayokabiliana nayo katika kuboresha ushiriki wa
michezo mbalimbali, ikiwemo ufinyu wa bajeti ambayo haikidhi ushiriki wa michezo
yote. Mwenyekiti huyo aliyeambatana na Katibu wake, Bw. Rorbert Tende, alibainisha
pia kuwa Mahakama Sports ina changamoto ya ukosefu wa viwanja vya kufanyia
mazoezi.
“Kwa sasa kwa
kushirikiana na uongozi wa Mahakama tumeomba viwanja katika Shule ya Sheria kwa
Vitendo. Ni Matumaini yetu kuwa wafanyakazi wote wa Mahakama watapata nafasi ya
kushiriki katika michezo yote kama tutaruhusiwa kufanyia mazoezi katika viwanja
hivi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alimweleza Mtendaji Mkuu pia kuwa Mahakama Sports siyo tu ina washiriki kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam, bali kuna wanamichezo wengine wengi katika kila Kanda wenye timu za michezo mfano; Bukoba, Mbeya, Mwanza, Musoma na Kanda zingine za Mahakama Kuu ya Tanzania
Safi sana viongozi na hongereni kwa hatua nzuri aiseee..
JibuFuta