Faustine Kapama na Lydia Churi – Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, leo Oktoba 4, 2021 amemuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikari, Dkt Eliezer
Mbuki Feleshi, kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Hafla ya uapisho huo ilifanyika katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma ilihudhuriwa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Palamagamba Kabudi, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. John Mugeta, Makamishna wa Tume, Katibu wa Tume, Naibu Katibu wa
Tume hiyo na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda
ya Dodoma, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pamoja na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt Feleshi alieleza
kuwa uapisho huo unamkumbusha namna alivyokuwa akitekeleza majukumu yake katika
ngazi mbalimbali kabla na baada ya kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Alieleza kuwa katika miaka 12 kwa madaraja tofauti akiwa Wakili wa Serikali
alikuwa mjumbe wa Kamati za Maadili katika ngazi ya Mkoa.
Dkt Feleshi alieleza kuwa alipokuwa Mkurugenzi wa
Mashitaka kwa miaka saba na nusu alikuwa na dhamana nyingine lakini kwenye
Kamati ya Maadili ya Mawakili, wakati katika kipindi cha miaka mitatu au minne
akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania alikuwa mjumbe wa Kamati ya Maadili ya
Majaji chini ya Kifungu cha 36 na 37 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama.
“Miaka mitatu na robo mingine nilikuwa mjumbe wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama wakati nilipokuwa Jaji Kiongozi. Hivyo, nashukuru
kwa dhamana nyingine ya kuwa mjumbe wa Tume hii nikiwa kama Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, hii ni heshima kubwa kwangu kwa kuaminiwa,” alisema. Hivyo aliahidi
kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria na Katiba na miongozo mingine
iliyopo.
Akiozungumza baada ya uapisho huo, Jaji Mkuu wa
Tanzania, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, alielezea
umuhimu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuapishwa kuwa Mjumbe wa Tume kutokana
na nafasi hiyo kutambuliwa kikatiba na kwamba ni matakwa ya kisheria kwa mujibu
wa Sheria ya Uendeshaji wa Shughuli za Mahakama ambayo yanamtaka kufanya
uapisho huo.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kuapishwa kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia kunatokana na majukumu mazito ambayo Tume
imepewa Kikatiba, ambapo anatakiwa kuwahakikishia wajumbe wengine kuwa atakuwa
tayari kuishi kiapo hicho, ikiwemo kutekeleza kikamilifu majukumu ya Kamishna
na kutunza siri ya mambo ambayo yanajadiliwa ndani ya Tume kabla ya kufikia
maamuzi.
Prof. Juma aliyataja baadhi ya majukumu ya
Makamishna wa Tume kuwa ni Pamoja na kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuhusu uteuzi wa Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
kumshauri Rais kuhusiana na masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji
na pia kushauri kuhusu uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye
ndiye mwajiri wa watumishi wote wa muhimili huo.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.
Palamagamba Kabudi alimpongeza Jaji Dkt Feleshi kwa kuteuliwa kuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na kwa nafasi hiyo kuapishwa kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama na kupitia kwake atakuwa kiunganishi na mwakilishi muhimu wa Wizara
ndani ya Tume na Mahakama kwa ujumla.
“Mhe. Feleshi ulikuwa na jukumu la Jaji Kiongozi,
na mamlaka ya uteuzi imeona jukumu la Jaji Kiongozi umelifanya vema na
inakuhitaji katika jukumu la Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hivyo hakuna haja ya
kuanza kulinganisha ni cheo kipi ni kikubwa na kipi ni kidogo, na ya Mungu ni
mengi, utajuaje kesho utakuwa wapi. Mhe. Rais ameona umsaidie katika jukumu
hili,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel, ambaye ndiye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,
aliwashukuru wajumbe na wadau wote waliohudhuria hafla hiyo na pia kumpongeza
Mhe. Dkt Feleshi kwa kuapishwa kuwa mjumbe wa Tume hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, leo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi uliopo ndani ya jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla ya kumuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, leo jijini Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akiapa mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbart Chuma na katikati ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akipongezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kuapishwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza kwenye hafla hiyo.
Viongozi wa wizara ya Katiba na Sheria wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa kwa Mwanansheria Mkuu wa Serikali kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, katikati ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Sifuni Mchome na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Amon Mpanju.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni