Na Faustine Kapama na Lydia Churi – Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma ametoa wito kwa Watanzania kubadili mtazamo kwanza badala ya kutaka mabadiliko ya Katiba na Sheria kabla ya kupima vifungu
vilivyopo kama vinatekelezeka na kuleta matokeo bora yanayotarajiwa katika
ustawi wa nchi.
Prof. Juma alitoa wito huo jana Oktoba 4, 2021 mara
baada ya kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Eliezer Mbuki
Feleshi, kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Hafla ya uapisho huo
ilifanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma na kuhudhuriwa
na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi.
“Ningependa kuwaambia Watanzania wenzangu, Sheria
za Tanzania siyo mbaya, mtazamo ndiyo mbaya. Sheria hii hii ukiipeleka Marekani
itafanyakazi vizuri sana. Pengine badala ya kufikiria kufanya mabadiliko ya
sheria, tuanze kufikiria mabadiliko ya nafsi. Nafsi zetu zinaheshimu sheria?
Nafsi zetu zinafuata utaratibu? Kwa sababu bila sisi wenyewe kufuata utaratibu,
hata tukiwa na sheria nzuri namna gani haitasaidia,” alisema.
Aidha, Jaji Mkuu aliwaomba wananchi wanapotaka
mabadiliko ya Katiba na Sheria wahakikishe vifungu vilivyopo hivi sasa
wanavitumia ili kujua kama kuna changamoto yoyote katika utekelezaji wake kabla
ya kufikiria kwamba pengine kuna vifungu vingine huko nje ambavyo vinaweza
kuleta matokeo bora zaidi.
Prof. Juma aliwakumbusha wananchi uwepo wa
utaratibu wa kushughulikia nidhamu katika ngazi ya Majaji, Mahakimu, ambapo
kuna ushiriki wa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, viongozi wa dini na wote
hao hukaa kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa watendaji hao wa
Mahakama.
“Ukiangalia sheria inayoendesha shughuli za
Mahakama imeunda kamati za maadili. Kuna Kamati za Maadili za Majaji, ambazo
zinapokea malalamiko ya kinidhamu dhidi ya Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi na
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kwenye suala la nidhamu
kuna ushirikishi ambapo wajumbe wanakuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji
wa Mahakama Kuu pamoja na wajumbe ambao wanatoka miongoni mwa maafisa wa
Mahakama katika ngazi za chini, lakini wanakaa kwenye ile kamati ya Majaji
inayosimamia maadili.
Alibainisha kuwa kwa bahati mbaya wananchi wengi
hawaelewi uwepo wa utaratibu wa kupokea malalamiko dhidi ya Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama Kuu na kuna utaratibu wa kumwomba
ajileleze mbele ya kamati hiyo na mapendekezo hupelekwa mbele ya Tume ya
Utumishi wa Mahakama na suala hilo likiwa zito hupelekwa kwenye mamlaka ya
uteuzi na kuna ngazi zingine za kufanya kama kuna haja ya kumwondoa Jaji
kazini.
“Hivyo, mimi nawaomba wananchi watumie mifumo ya
kulalamika masuala ya kinidhamu dhidi ya kiongozi yoyote yule ndani ya
Mahakama. Jaji Mkuu ni sehemu ya Mahakama ya Rufani na malalamiko ya kinidhamu
yanaweza kuletwa na yakashughulikiwa. Vile vile hatua kama hizo zinaweza
kuchukuliwa kwa Jaji mwingine yoyote au Hakimu kwa vile hakuna mtu yoyote yule
ambaye yupo juu ya sheria na uzuri mfumo wetu umewakilishwa hadi wilayani na
mikoani ambapo huweza kupokea malalamiko na kuyashughulikia,” alisema.
Jaji Mkuu alibainisha pia kuwa Kamati ya Maadili ya
Majaji sio kwamba haina mashauri inayosikiliza, ambapo malalamiko yanapoletwa
hufanyiwa kazi na ile kamati ambayo Jaji Kiongozi anaiongoza ni
kamati ambayo inashughulikia masuala ya kinidhamu dhidi ya watumishi wa
Mahakama. Hivyo, aliwaomba wananchi wanapokuwa na malalamiko yanayogusa nidhamu
watumie mifumo iliyopo ili kuweze kuipima kama inatosha, na kama haitoshi
ifanyiwe marekebisho. “Tusifanye marekebisho bila kupima kama
vifiungu vilivyopo vinaweza kufanya kazi,” alisema.
Hivyo alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kuapishwa kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Jaji Mkuu alimwelezea
Dkt Feleshi jinsi alivyokuwa msaidizi wake muhimu alipokuwa Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye kila asubuhi alikuwa anafuatilia kwenye mfumo
wa Mahakama kujua hali ya mashauri inavyokwenda, kuangalia ni mashauri mangani
yamesajiliwa kwa njia ya mtandao na mashauri mangapi ambayo hayajapangiwa
Majaji na Mahakimu.
“Alikuwa anafuatilia mlundikano wa mashauri. Sisi
huku Mahakamani tuna utaratibu, kwa mfano shauri likisajiliwa Mahakama ya
Mwanzo linatakiwa liwe limeisha ndani ya miezi sita, katika Mahakama wa Wilaya
na Mahakama ya Hakimu Mkazi, shauri linatakiwa limalizike ndani ya miezi 12 na
kwa upande wa Mahakakama Kuu na Mahakama ya Rufani, shauri lazima liishe ndani
ya miezi 24. Mimi naamini huko unakokwenda utaleta huo mfumo wa watu kutopata
usingizi. Usikubali watu walale kwa sababu usimamizi ni jambo ambalo ni muhimu
sana,” alisema.
Jaji Mkuu
alimwahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali huyo kuwa Mahakama ya Tanzania
itaendeleza huo utaratibu aliouweka wa kufuatilia kwa karibu mienendo ya
mashauri na kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi yake kwa wakati na hivyo
kupunguza malalamiko kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana jijini Dodoma.
Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) akizungumza wakati wa hafla ya kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Amon Mpanju.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni