Jumatano, 27 Oktoba 2021

PROGRAMU MAALUMU KUTAFSIRI HUKUMU YAANDALIWA

Na Faustine Kapama na Mary Gwera , Mahakama-Serengeti

Mahakama ya Tanzania inaandaa programu maalumu, ‘software’ itakayotumika kutafsiri hukumu zinazotolewa katika ngazi zote za Mahakama kwa lugha mbalimbali, ikiwemo Kiswahili na Kiingereza.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 27 Oktoba, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa anaongea na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi aliyoianza hivi karibuni ya kutembelea Mahakama mbalimbali katika Kanda ya Musoma.

“Fedha tayari zimeshatengwa na tumepata wataalam wa kuweza kutupa ‘software’, unaweza kuamua kuandika hukumu yako katika lugha ya Kiswahili, hiyo ‘software’ itaitafsiri kwa lugha ya Kiingereza, au ukaiandika kwa Kiingereza, ‘software’ hiyo ikaitoa kwa lugha ya Kiswahili. Tunataka tutakapokuwa kwenye Wiki ya Sheria mwakani tuweze kuwa na ‘software’ hiyo ya kumuwezesha mwananchi kuchagua ni lugha gani ambayo anataka hukumu yake itoke,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu wameamua kuwepo kwa ‘software ‘hiyo kwa sababu hawawezi kuacha kutumia lugha ya Kiingereza, kitendo ambacho kinaweza kutafsiriwa kama kujitenga na Dunia. Amesema kuwa Mwalimu Nyerere alishawahi kusema Kiingereza ni Kiswahili cha Dunia na kwamba Kiingereza ni lugha ya biashara, ingawa Kiswahili kinaweza kuwa muhimu zaidi.

“Sasa tukiwa na software hiyo tutawawezesha wananchi kufahamu maneno mengi yaliyo katika lugha ya Kiingereza  waweze kuyafahamu katika lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, mwananchi atakuwa anachagua, akitaka hukumu yake itoke kwa Kiingereza, inatoka, akitaka itoke kwa lugha ya Kiswahili, inatoka na tunaweza baadaye kuijaza maneno iweze kutoa lugha yoyote,” Jaji Mkuu alisema.

Mhe. Prof. Juma ametahadharisha kuwa lugha za Kitanzania zimeaza kupotea, mfano lugha ya Kimasai, Kingoreme, ambapo Dunia ya karne ya 21 inaelekea kwenye matumizi ya lugha zaidi ya moja, ikiwemo Kiingereza ambacho bado ni lugha ya kibiashara ya kimataifa. Ameonya kuwa kujitenga na lugha ya Kiingereza ni sawa na kujichimbia kwenye shimo ambalo huwezi kutoka.

Amebainisha pia kuwa suala la kutafsiri hukumu zinazotolewa mahakamani kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine ni jambo ambalo ni la kisera. “Tutahakikisha kwamba Mahakama zote zinatoa hukumu katika lugha ya Kiswahili. Lakini sisi kuna hatua ambazo tunafuata hadi kufikia huko,” amesema.

Jaji Mkuu ameeleza hatua hizo kuwa zinaanzia kutafsiri sheria ili ziwe katika lugha ya Kiswahili ili kuepusha migongano ya kilugha, baadaye sheria hizo hupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye naye hupeleka kwa Mwandishi wa Sheria wa Serikali, tayari kwa kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

 “Sisi tunatakiwa kushughulikia sheria, kwa hiyo ile ofisi ya Mwandishi wa Sheria wa Serikali itatusaidia na nadhani anafanya kazi hiyo kutafsiri zile sheria ili kazi yetu iwe kutumia sheria hizo kutatua migogoro ambayo ipo kwetu,” amesema.

Kwa upande wa Mahakama, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa wanatafsiri kanuni zote ambazo zipo katika lugha ya Kiingereza zilizopo chini ya mamlaka ya Jaji Mkuu kuzitunga na Kamati ya Kanuni tayari imeshatafsiri sheria zaidi ya 50, ambazo zitapelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutoa tafsiri za kisheria.

Taarifa iliyowasilishwa mbele yake na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Mhe. Jacob Barakazi inaeleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuanzia tarehe 01 Januari, 2021 hadi tarehe 30 Septemba, 2021, ikiwemo  kutoa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri kwa wakati na kutafsiri hukumu kwa lugha ya Kiswahili.

Hivyo, Jaji Mkuu aliwataka viongozi wa Mahakama hiyo kuwasiliana na kitengo cha TEHAMA cha Mahakama ambacho kwa sasa kinakusanya misamiati ya Kiswahili na kuilinganisha na Kiingereza ambayo itatumika kutengeneza benki ya maneno yatakayowekwa kwenye ‘software’ hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti (hawapo katika picha) alipowasili katika Mahakama hiyo katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ndani ya Kanda ya Musoma iliyoanza jana tarehe 26 Oktoba 2021.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Makao makuu ya Mahakama na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao alipowasili katika Mahakama hiyo kwa ziara ya kikazi leo tarehe 27 Oktoba, 2021.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Mhe. Jacob Ndira akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika) picha wakati alipowasili katika Mahakama hiyo kwa ziara ya kikazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti. Aliyeketi kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. John Kahyoza na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.
Picha ya pamoja na Watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Wilaya Serengeti.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Musoma)
 

 

 

 

Maoni 1 :