Jumapili, 7 Novemba 2021

MABADILIKO YATAKIWA KWENYE VITUO JUMUISHI

Na Stanslaus Makendi – Mahakama Kuu Dodoma

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. George Masaju amewahimiza viongozi wenzake wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini kusimamia shughuli za kimahakama na utawala katika maeneo yao kwa kuzingatia maadili na viwango vinavyotakiwa ili huduma zitakazotolewa zitapatikane kwa urahisi na haraka zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali kabla ya kuanzishwa kwa Vituo hivyo.

Jaji Masaju alitoa wito huo tarehe 04 Novemba, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya viongozi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vya Temeke, Morogoro na Dodoma yaliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.

Alisema kuwa Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake imefanikiwa kuboresha miundombinu ya majengo na vitendea kazi na kuweka mifumo ya kisasa ya TEHAMA katika majengo hayo. “Hivyo, ni jukumu letu sote kama viongozi kuendelea kuwajengea uwezo wadau na watumishi katika maeneo yetu ya kazi ili waweze kutoa huduma zenye viwango vyenye ubora ziendane na majengo na miundombinu tuliyonayo,” Jaji Masaju alisema.

Alisisitiza umuhimu wa kusimamia maadili na viwango vya utendaji ili wananchi wapate huduma wanazozihitaji kwa  haki na wakati, hatua ambayo kama watafanikiwa itabadili mitizamo ya watumishi, na kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wale watakaokiuka maelekezo na viwango vya huduma wanavyopaswa kuvitoa.

Mafunzo hayo ya viongozi ni mwendelezo wa yale yanayotolewa kwa watumishi wa Mahakama pamoja na wadau yanayoendelea katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma ambayo yameanza kutolewa tangu tarehe 01 Novemba, 2021 kwa lengo la kufahamishana na kujenga uelewa wa pamoja juu ya dhana na malengo halisi ya uanzishwa wa Vituo hivyo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Elizabeth Nyembele (aliyesimama) akiwakaribisha Viongozi wa vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Temeke, Morogoro na Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa vituo hivyo yaliyofanyika tarehe 04 Novemba, 2021. Katikati ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. George Masaju, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi. 


Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyesimama) akitoa mada kwa viongozi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Temeke, Morogoro na Dodoma.


Sehemu ya viongozi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Temeke, Morogoro na Dodoma wakiwa kwenye Mafunzo hayo.

Sehemu ya watumishi na wadau wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma waliokuwa kwenye mafunzo hayo.

Picha ya pamoja kati ya viongozi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vya Temeke, Morogoro na Dodoma wakiwa na watumishi na wadau mbalimbali.


Maoni 1 :