Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema
gharama ya uchunguzi kwa kipimo cha vina saba anachochukuliwa mtu mmoja ni
shillingi 100,000 za Kitanzania na siyo vinginevyo.
Dkt. Mafumiko ametoa ufafanuzi huo leo tarehe 29
Januari, 2022 alipotembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Mahakama ya
Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kama
sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
“Mara nyingi nimekuwa nikisikia gharama za Mkemia Mkuu
wa Serikali za kuchukua hivi vipimo ni shillingi millioni mbili, shillingi
500,000, shillingi 700,000, hiyo ni taarifa ambayo siyo sahihi,” amesema
alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari kwenye viwanja hivyo.
Amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imebeba sehemu kubwa ya gharama za uchunguzi wa vina saba, hivyo
kuwezesha gharama ya uchunguzi kwa
kipimo anachochukuliwa mtu mmoja kwa sasa kuwa shilling 100,000 za Kitanzania
pekee.
“Kwa mfano, unataka kujua mahusiano ya baba, mama na
mtoto. Pale tutachukua sampuli kutoka kwa watu watatu na gharama yake ni
shilling 300,000 za Kitanzania, lakini kukiwa kuna watoto wanne, watano, gharama
yake itaongezeka hivyo hivyo. Lakini, kwa kila tunayemchukua sampuli gharama
yake ni shilling 100,000 za Kitanzania,” Dkt Mafumiko amesema.
Kwa mujibu wa Mkemia Mkuu wa Serikali, kuna wakati fulani
waliwahi kusema kuwa kwa kuangalia vitenganishi vyake, gharama y kipimo ingeweza
kuwa kati ya 700,000 hadi 800,000 kama Serikali isingebeba sehemu ya gharama
hizo, lakini mpaka sasa bado ofisi yake inatoza gharama ile ile ya shillingi
100,000 za Kitanzania kwa kila wanayemchukua sampuli.
Dkt Mafumiko pia ametoa wito kwa wananchi wanapotaka
kufanya kipimo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kinachohusiana na masuala ya kijinai
kutumia mamlaka zilizopo badala ya wao wenyewe kama wateja kwenda moja kwa moja
katika ofisi hiyo.
“Kuna mamlaka
zilizowekwa kwa ajili ya kumwomba Mkemia Mkuu wa Serikali vipimo. Kama ni suala
la kijamii kuna maafisa ustawi wa jamii, kuna Mawakili walioandikishwa, kama ni
suala lipo mahakamani kuna Mahakama na wenzetu wa Jeshi la Polisi, kama ni
suala la kimatibabu kuna Madaktari, kama suala la majanga, kuna Wakuu wa
Wilaya,” amesema.
Baadhi ya mabanda aliyotemebelea ni RITA, Kitengo cha
Uboreshaji cha Mahakama ya Tanzania, Magereza, Polisi, Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi yake ya Mkemia Mkuu wa
Serikali.
Dkt Mafumiko amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.
Ibrahim Hamis Juma kwa kuandaa maonesho yanayotoa fursa kwa watoa huduma na
elimu mbalimbali ya kisheria kwa wananchi. Amewashukuru pia waandaaji wa maonesho
hayo kwa kuipa nafasi ofisi yake kama moja ya taasisi ambazo ni wadau wakubwa wa
Mahakama ya kushiriki kwenye Wiki ya Sheria.
“Nawapongeza wote ambao wanashiriki kwenye kuonesha
nini taasisi zao zinafanya na uhusiano wao kwa Mahakama. Hii ni mara yangu ya
tatu, lakini naona maandalizi ya mwaka huu yamekuwa mazuri sana. Kwa hiyo
nawapongeza wote,” amesema.
Mkemia Mkuu wa Serikali ameeleza majukumu makubwa ya
taasisi yake ni kuchunguza sampuli zinazotokana na vilelelezo mbalimbali vya
masuala ya kijinai, masuala ya kijamii, kimazingira na masuala mengineyo.
Amesema mamlaka ya ofisi yake pia yamejikita kutekeleza
jukumu la usimamiaji na uthibiti wa shughuli zote za kemikali zisizo za kitiba
ambazo zinaingia nchini, zile zinazokwenda nje ya nchi na zile zinazosafirishwa
ndani na nje ya nchi, lengo ni kulinda afya za binadamu na mazingira.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko
akiupongeza uongozi wa Mahakama kwa jitihada kubwa za kuboresha mifumo ya
TEHAMA inayorahisisha utoaji wa haki kwa wananchi kwa wakati, kulia ni Afisa
TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Othman
Kanyegezi, akimsikiliza alipotembelea banda lao leo tarehe 29 Januari, 2022 kwenye maadhimisho ya
Wiki ya Sheria nchini katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Charles
Magesa akimkabidhi Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko nakala ya Kitabu cha Mpango Mkakati wa
Mahakama wa 2021/22 hadi 2024/25 ikiwa ni dira ya Mahakama ya miaka tano ijayo
ya utekelezaji wa shughuli zake.
Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko akielezea umuhimu wa Jeshi la Polisi katika
kufanikisha shughuli za kiuchunguzi katika Mamlaka ya Maabala ya Mkemia Mkuu wa
Serikali wakati alipokuwa akikagua shughuli mbalimbali zinazoendelea katika
maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko
akielezea jambo wakati alipotembelea banda la Jeshi Uhamiaji Tanzania na kupewa
maelezo mafupi ya majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Jeshi hilo ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni