Na Tiganya Vicent – Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Watumishi wa Mahakama nchini
kuongeza kasi katika kuwatumikia wananchi ili waweze kupata haki zao kwa wakati
unaostahili.
Alisema ni vema
uboreshwaji wa miundombinu ya Mahakama hapa nchini ikaendana na huduma bora
zinazotolewa kwa wananchi.
Mhe. Siyani ametoa kauli
hiyo leo tarehe 28 Januari, 2022 wakati wa kuzindua jengo linalojumuisha Mahakama
ya Wilaya na Mwanzo Bahi ambalo ujenzi wake umegharimu milioni 797.6 za
Kitanzania.
Alisema uzinduzi wa
Mahakama ya Wilaya ya Bahi na nyingine hapa nchini ni sehemu ya mpango wa
maboresho ya miundombinu uliojikita katika kuboresha utoaji haki na kusogeza huduma
karibu zaidi na wananchi.
Mhe. Siyani aliishukuru
Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi wa
miundombinu ya Mahakama.
Aidha, Jaji Kiongozi
aliwaeleza watumishi wa Mahakama hiyo kuwa wamepata jengo nzuri ambalo ni kama
vazi jipya kwao. Hata hivyo aliwataka kutambua kuwa wananchi wanatarajia uzuri
wa jengo hilo uendane na ubora wa huduma zitakazotolewa.
“Jengo hili na mengine
yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa kote nchini yanajengwa kwa kodi za
wananchi. Kwa hiyo tambueni kuwa wananchi ndiyo wenye mamlaka na watawapima kwa
ubora wa kazi zenu na kama nyinyi mnavyowahukumu wenye makosa mbele yenu,”alisema.
Kwa upande mwingine, Mhe.
Siyani aliwakumbusha wananchi wanaotumia huduma za Mahakama kujua kuwa vipo
vyombo maalum vilivyowekwa kisheria kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko dhidi
ya watumishi wa Mahakama na huduma wazitoazo.
Alitoa mfano kuwa
malalamiko ya kimaadili dhidi ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya
yanaweza kuwasilishwa kwenye kamati za maadili za Maafisa wa Mahakama ngazi ya
Wilaya na Mkoa ambazo wenyeviti wake ni Wakuu wa Wilaya na Mikoa kote nchini.
“Watumieni viongozi hawa
ambao mko karibu nao kuwasilisha kero za kimaadili. Kwa malalamiko dhidi ya
huduma za Mahakama, kuna madawati maalumu ya malalamiko katika kila Mahakama ya
Wilaya, Mkoa na Mahakama Kuu,”alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu alisema kukamilika kwa jengo hilo
litawezesha kutoa huduma kwa wakazi wapatao 271,000 kwa maoteo ya sensa ya
mwaka 2019.
Naye Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel alisema uongozi wa Mahakama utaendelea
kuhakikisha jengo hilo linatunzwa ili liweze kuwahudumia wananchi kwa kadri ya malengo na fedha inayotolewa na
Serikali.
Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma aliwataka wadau wa Mahakama kutoa ushirikiano
ili kesi ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na haki iweze kupatikana kwa
mhusika kwa wakati.
Aliuomba Uongozi wa
Wilaya ya Bahi kusaidia upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya
watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bahi.
Awali, Mtendaji wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dodoma, Bi Maria Itala alisema jumla ya shilingi milioni 797.6 za
Kitanzania zimetumika katika ujenzi wa mradi huo wa jengo la Mahakama ya Wilaya
ya Bahi.
Alisema ujenzi wa
Mahakama hiyo umelenga kusogeza huduma za kimahakama karibuni na wananchi ikiwa
sehemu ya mpango mkakati wa uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama nchini
Tanzania.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (mwenye tai nyekundu) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Bahi mkoani Dodoma katika hafla iliyofanyika leo tarehe 28 Januari, 2022.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akifunua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Bahi mkoani Dodoma. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bi. Mwanahamis Mkunda.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiongea na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Bahi mkoani Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme akitoa neno la utangulizi kumkaribisha mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bi. Mwanahamis Mkunda akitoa salamu za Serikali katika hafla hiyo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma akieleza jambo katika hafla ya uzinduzi wa jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Bahi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa nasaha kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Bahi katika hafla hiyo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bi. Maria Itala akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo hilo.
Sehemu ya maafisa wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria uzinduzi huo.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama na wananchi waliohuduria uzinduzi wa jengo hilo.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohuduria uzinduzi huo.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama Dodoma waliohuduria uzinduzi huo.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni