Na Evelina Odemba - Morogoro
Wananchi mkoani Morogoro
wamejitokeza kwa wingi katika mabanda mbalimbali yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, kupata elimu na huduma za kisheria kutoka kwa
Majaji, Mahakimu na wadau mbalimbali.
Mabanda hayo yameandaliwa kama
sehemu ya Wiki ya Sheria inayoadhimishwa kote nchini. Maadhimisho hayo
yanafanyika kitaifa jijini Dodoma. Baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye
mabanda hayo wameonyesha kufurahia namna walivyopokelewa na hatimaye kupata
huduma za kisheria walizokuwa wakihitaji.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe.
Albert Msendo alikuwa ni miongoni mwa wana Morogoro waliofika katika mabanda
hayo kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa yanayohusu Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande mwingine, maafisa wa
Mahakama, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro,
Mhe. Paul Ngwembe wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya kisheria kwa
wananchi kwa njia mbalimbali.
Mhe. Ngwembe alitembelea katika
kituo cha Televisheni cha Abood mjini Morogoro ambapo alizungumzia masuala
mbalimbali ya kisheria, huku Jaji mwingine kutoka katika Kanda hiyo, Mhe. Said
Kalunde akashiriki kutoa ufafanizi wa mambo ya kisheria kupitia kituo cha Radio
cha Abood.
Mahakimu mbalimbali pamoja na
wasaidizi wa sheria wa Majaji nao hawakusita kutembelea maeneo kadhaa, ikiwemo
katika mashule hapa mjini Morogoro kwa lengo la kutoa elimu ya kisheria kwa
wananchi.
Mahakama ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro, ilizindua Wiki ya Sheria tarehe 24 Januari, 2022 ambapo Mhe.
Ngwembe aliwahakikishia Watanzania kuwa hawatabaki nyuma katika kutekeleza
jukumu la utoaji haki na wapo tayari kwenda na mabadiliko yatokanayo na
Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
Alisema kuwa Mahakama
Mkoani Morogoro haipo nyuma kwenye mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea
hivi sasa ambapo tayari wamefunga televisheni tatika gereza la Mahabusu ambapo mashauri
mbalimbali yameanza kusikilizwa kupitia mtandao (video conference).
Aidha Jaji Mfawidhi
huyo aliongeza kuwa kwa sasa nakala za hukumu hutolewa siku ya kusomwa kwa
hukumu na ili kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa Mahakama imenunua Kompyuta
Mpakato kwa Waheshimiwa Mahakimu kote nchini kuwarahisishia kuandika hukumu kwa
wakati.
Mhe. Ngwembe alitumia
fulsa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kufika katika vituo vya kutolea elimu
ili waweze kujifunza maswala mbalimbali yanayohusu Mahakama pamoja na wadau wake.
Alivitaja vituo hivyo
kuwa ni viwanja vya Mahakama Kuu- Kituo Jumuishi( IJC)- Kihonda -Morogoro,
viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha Ndege, Soko kuu la Kingalu, stendi kuu
ya mabasi Msamvu na soko la Chamwino.
Iwe endelevu kazi nzuri a ana. Inaonesha jinsi wananchi wa mkoa wa Morogoro walivyo na kiu ya kupata huduma za kisheria
JibuFutaPia mahakama itoe nafasi kwa wadau na wananchi kutoa maoni
JibuFutaElimu iwe endelevu kila baada ya muda Fulani ili wananchi waendelendee kufaidika na elimu
JibuFuta