Alhamisi, 3 Februari 2022

JAJI MRUMA: ATAKA BAADHI YA SHERIA ZIFANYIWE MAREKEBISHO KUPUNGUZA MLUNDIKANO WA MAHABUSU

 

Na Magreth Kinabo -Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma ametoa maoni kuwa ni wakati wa muafaka kwa mihimili ya Bunge na Serikali kuangalia upya baadhi ya sheria zifanyiwe marekebisho ili mtuhumiwa aweze kukamatwa upelelezi ukishakamilika kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa mlundikano wa mahabusu katika magereza.

 Akizungumza leo Februari 2, mwaka 2122 katika kilele cha Siku ya Sheria Nchini kwa Kanda ya Dare s Salaam, kilichofanyika kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Mruma, ambaye ni mgeni rasmi alisema kuna baadhi ya washtakiwa wanaletwa mahakamani ili upelelezi ukamilike wakiwa mahakamani.

‘‘Hii si haki na ni kucheza na haki za watu. Ukiondoa mashauri machache mfano yale ya mauaji ambayo hata usalama wa mtuhumiwa unaweza kuwa hatarini, na yale yanayohatarisha usalama wa nchi,’alisema Jaji Mruma huku akihoji kwamba kuna haraka gani kumkamata mtuhumiwa na kumfungulia kesi kabla ya upelelezi kukamilisha upepelezi dhidi yake? Je, kama baada ya upelelezi kukamilika na akaonekana hana hatia nani atamfidia?

 Alisema kama wadau wote watafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo hakutokuwepo na mlundikano wa mahabusu katika magereza na hakutakuwa na mashauri yaliyokaa muda mrefu.

Jaji Mruma aliongeza kwamba sasa Mahakama inatoa nakala za bure ndani ya siku 21 na mwenendo wa shauri unatakiwa kupatikana ndani ya siku 30. Hivyo katika kipindi cha Januari hadi Desemba,  mwaka 2021 kanda hiyo imeweza kutoa nakala za hukumu zipatazo 3,615.

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imewezesha maisha kuwa mepesi zaidi kwani kwa sasa wanapata takwimu sahihi na kwa wakati sahihi, ambapo awali walikuwa wanategemea karatasi na kutuma posta.

Alifafanua kuwa kwamujibu wa taarifa kutoka Masjala Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 mashauri yaliyofunguliwa ni 1,594, yaliyomalizika ni 2,356 na yanayoendelea ni 2,896. Aidha kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya mashauri yaliyofunguliwa kipindi hicho ni 1,1790, yaliyomalizika 5,594 na yanayoendelea ni 2,997.

Alisema taarifa ya Mahakama za Mwanzo zinasema mashauri yaliyofunguliwa ni 11,790, yaliyomalizika ni 12,813 na yanayoendelea ni 2,997.

‘‘Nachukua fursa hii kuwapongeza Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kwani hawana mlundikano wa mashauri na wamemaliza mashauri yao zaidi ya asilimia 100,’’alisisitiza.

Aliitaja changamoto uliyopo katika Mahakama Kuu ni ni kuwepo kwa mashauri yenye umri mrefu kutokana na uchache wa majaji, kwa kuwa mahakama hiyo ina majaji saba. Hivyo mashauri yaliyopo hayaendani na idadi ya majaji waliopo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Amos Makala ambaye alikuwa mgeni maalum alisema aliipongeza Mahakama kwa hatua iliyofikia ya Mahakama Mtandao kile kisingizio faili limepotea hakuna. Hivyo changamoto iliyopo kwa wananchi ni kuwepo kwa elimu ndogo ya sheria, ambapo alisema ataendelea kushirikiana na mahakama kutoa elimu hiyo kwa kuwa ni jambo la muhimu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria (TLS) mkoa wa Dar es Salaam Mzizima, Bw.James Marenga alisema chombo hicho kina kazi ya kutatua migogoro  bila malipo ili  kupunguza migogoro inayoletwa mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma akijiandaa kugakugua gwaride ikiwa ni ishara za kuanza shughuli za mahakama na kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini, kilichofanyika kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma akitoa hotuba yake katika maadhimisho hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Amos Makala ambaye alikuwa mgeni maalum katika maadhimisho hayo, akizungumza jambo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria (TLS) mkoa wa Dar es Salaam Mzizima, Bw.James Marenga akizungumza jambo.

 Baadhi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala(watatu kusho, wakiwemo wakuu vyombo vya ulinzi na usalama.









 kupunguza migogoro inayoletwa mahakamani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni