Na Francisca Swai, Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, leo tarehe 02 Februari 2022, amesema kuwa ili Taasisi yoyote iweze kuendelea kukua katika zama hizi za matumizi makubwa ya teknolojia inabidi kuendana na matumizi ya TEHAMA.
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Sheria nchini yenye kaulimbiu ‘‘Zama za Mapinduzi ya nne ya Viwanda: Safari ya maboresho kuelekea Mahakama Mtandao’’ Mhe. Jaji Mtulya alisema kuwa ni muhimu kwenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia
Aidha, Mhe. Jaji Fahamu Mtulya, amewahimiza wananchi na wadau kujitahidi kuendana na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA ili kupunguza gharama na muda unaotumika kufuatilia mashauri na huduma mbalimbali za Mahakama ili kupata muda wa kutosha katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.
Mhe.Jaji Mfawidhi aliongeza kuwa huduma zinazopatikana kwa njia ya mtandao mahakamani ni pamoja na ufunguaji wa mashauri, usikilizwaji wa mashauri, kujua taarifa za shauri husika mfano siku ya kesi kusikilizwa, imepangwa kwa Hakimu/Jaji nani, nakala za hukumu, mjue wakili wako n.k
Naye Mwenyekiti wa Mawakili (TLS) Musoma Wakili, Ostack Mligo amesema, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika matumizi ya TEHAMA na kutoa wito kwa vijana kutumia teknolojia ili wasibaki nyuma. Alisema pamoja na maboresho hayo makubwa bado wananchi walio wengi hasa wa maeneo ya vijijini hawana simu wezeshi kwa ajili ya kupata huduma hizi kwa mtandao ikiwa ni pamoja na changamoto ya mtandao katika maeneo yao, hivyo huduma hizo ni vema zikaboreshwa na kupatikana kwa bei nafuu ili wote waweze kufaidi huduma za Mahakama mtandao.
Aidha, Wakili Mligo aliendelea kwa kutoa rai kuwa maboresho haya yaangalie pia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba yaliyopo kwani yana uhaba mkubwa wa watumishi na yako nyuma sana katika matumizi ya TEHAMA licha ya kuwa wanahudumia wananchi wengi wa hali ya chini wanaotoka vijijini wenye migogoro mikubwa katika rasilimali muhimu ya ardhi.
Akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Dkt. Halfani Haule, ameishukuru Mahakama kwa wiki ya sheria ambayo imewanufaisha wananchi wengi walikuwa na matatizo mbalimbali ya kisheria na wasijue wapi waelekee kupata msaada.
Ameshukuru pia kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali za Mahakama unaoendelea kufanyika na ambayo tayari yamekamilika ikiwemo upatikanaji wa jengo la Mahakama Kuu Musoma huku akitoa rai kuwa kuwa uboreshaji wa huduma ufanyike pia katika Mahakama nyingine mkoani humo ikiwemo ya Hakimu Mkazi , Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akizungumza na wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika leo tarehe 02 Februari, 2022.
Mwenyekiti wa chama cha mawakili (TLS) Musoma, Wakili Ostack Mligo akisoma hotuba yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini Mahakama-Dodoma.
Pichani ni Mhe. Jaji Mfawidhi Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akijiandaa kwa ajili ya ukaguzi wa gwaride.
Picha ya pamoja na Viongozi wa Dini, aliyekaa katikaki, kushoto kwake ni Mhe. Frank Mahimbali, Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, kushoto ni Wakili Ostack Mligo, kulia kwa Jaji Mtulya ni Mkuu wa Wilaya Musoma, Dkt. Halfani Haule pamoja na Wakili, Kitia Toroke, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwa na na viongozi wa dini waliohudhuria maadhimisho ya siku ya sheria nchini 2022 Kanda ya Musoma.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni