Na Evelina Odemba - Morogoro
Wakazi Zaidi ya 30,000
mkoani Morogoro wamenufaika na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kupatiwa elimu
mbalimbali juu ya haki za watoto na mambo mbalimbali ya kisheria.
Hayo yalielezwa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, alipokuwa
akizungumza katika kilele cha maazimisho ya Siku ya Sheria tarehe 2 Februari,
2022 yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani
hapa.
Mhe. Ngwembe alisema kuwa
maelfu hayo ya wananchi waliojitokeza kwenye vituo vilivyoandaliwa kwa ajili ya
kutolea elimu katika kipindi chote cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria ili kupata
ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sheria, Mahakama na wadau wake.
Alivitaja vitaja vituo hivyo
kuwa ni stendi ya mabasi ya Msamvu, Soko la Kingalu, Soko la Chamwino, viwanja vya
shule ya Msingi, kiwanja cha Ndege pamoja na viwanja vya Mahakama Kuu- Kituo Jumuishi
cha utoaji Haki (IJC -Morogoro).
Mhe. Ngwembe alieleza kuwa
Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake waliwafikia wananchi kupitia vyombo vya
habari 11 ikiwemo Televisheni tatu vilivyoko mkoani hapa, elimu kwa shule saba
za msingi na pia Magereza mawili ya Mkoa
wa Morogoro, chuo cha ualimu Kigurunyembe pamoja na chuo Kikuu cha Mzumbe.
Jaji Mfawidhi huyo
amesema kuwa maboresho ya Mahakama kwa sasa yanasaidia kufanikisha shughuli za kimahakama
kwa wakati sahihi na tayari teknolojia imeanza kutumika kwenye usikilizaji wa mashauri
na kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.
Akitoa salamu kwa niaba
ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha
Wanasheria Morogoro, Bi Mariam Kapama alisema kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa
na Mahakama ya Tanzania ni ya mfano, hivyo wanasheria wanaomba Mahakama inapojenga
majengo yake izingatie pia kuweka ofisi za mawakili wa kujitegemea, jambo litakalorahisisha
utoaji haki kwa wakati.
Kwa upande wake, Wakili
wa Serikali Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Xavier Masalu kutoka ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali alisema kuwa Mahakama imesaidia kupambana na rushwa kwa kuweka
mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao, jambo ambalo limeleta uwazi na linaokoa
gharama na muda.
Ametoa rai kuwa maboresho
hayo pia yafanyike kwa wadau wa Mahakama ili nao waweze kwenda na kasi ya utendaji
wa Mahakama.
Naye mgeni maalumu, Mkuu
wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando alitoa pongezi kwa Mahakama kwa kuweza
kutoa elimu ya sheria kwa wananchi.
Ameagiza Wakurugenzi kutenga
maeneo kwa ajili ya kuweka miundombinu ya Mahakama na ofisi zote zinazohusika na
utoaji haki , huku akizitaka ofisi hizo zenye uhitaji wa maeneo kuandika barua kwa
Mkurugenzi wa Manispaa ili waweze kupatiwa maeneo ya kujenga ofisi hizo.
Wiki ya sheria nchini ilizinduliwa
mnamo tarehe 23 Januari 2022 jijini Dodoma ambapo kwa Kanda ya Morogoro
uzinduzi huo pia ulifanyika katika viwanja vya Jamuhuri, ukifuatiwa na uzinduzi
wa vituo vya kutolea elimu ya sheria tarehe 24 Januari 2022 ambapo ndani ya muda
huo shughuli mbalimbali za utoaji elimu ya kisheria kwa wananchi ulifanyika.
Kilele cha Siku ya Sheria
kinaashiria kuanza rasmi kwa shuguli za Mahakama nchini. Ikumbukwe kuwa Mahakama
itatembea na kauli mbiu isemayo “zama za mapinduzi ya nne ya viwanda: safari ya
maboresho kuelekea Mahakama Mtandao.”
Wadau mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akipokea salamu za heshima kutoka kwa kiongozi wa gwaride.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe( katikati aliyekaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Morogoro (juu na chini). Wengine waliokaa kutoka kushoto kwa Mhe. Ngwembe ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Said Kalunde ambao wanafuatiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Foutunatus Muslim. Kulia kwa Mhe. Ngwembe ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Xavier Masalu na Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Wanasheria Morogoro, Bi Mariam Kapama (kushoto).
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe( katikati aliyekaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa (juu) na watumishi wa Mahakama (chini). Wengine waliokaa kutoka kushoto kwa Mhe. Ngwembe ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Said Kalunde ambao wanafuatiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Foutunatus Muslim. Kulia kwa Mhe. Ngwembe ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Xavier Masalu na Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Wanasheria Morogoro, Bi Mariam Kapama (kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni