Na Innocent Kansha – Mahakama.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Wakandarasi
kuhakikisha miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini
inatekelezwa kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa.
Akizungumza
kwenye kikao kazi na Wakandarasi hao leo tarehe 22 Februari, 2022 katika Ukumbi
wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni Jijini Dar es
salaam, Prof. Ole Gabriel alisema Mahakama itaendelea kuwatizama kwa jicho la
karibu katika utendaji wao na haitovumilia wakandarasi watakaofanya kazi kwa mazoea.
“Mahakama
ya Tanzania inathamini sana kazi za wakandarasi wazawa, ni vema mkafanya kazi
kwa weledi kwani miradi hii sio ya mwisho. Mahakama ya Tanzania ina miradi
mingi inayoendelea na inayotarajiwa kutekelezwa, msitupe mbachao kwa msala
upitao …fanyeni kazi zenu kwa ubora na kwa kasi ili miradi mingine ikitokea tuweze
kuwapatia,”aliwasisitiza
Kadhalika,
Mtendaji Mkuu aliwataka wakandarasi hao kujali utaalamu wa fani zao ili kazi zinazofanyika
ziwe madhubuti na kuzingatia ubora kwa ufanisi unaokubalika, kwa vile kila
kitabu kina zama zake kwani Mahakama ya sasa ni ya watu waadilifu.
Prof.
Ole Gabriel aliwakumbusha wataalam hao kuwa hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya kilele cha siku ya
Sheria mjini Dodoma alisisitiza miradi inayoendelea kujengwa kwa ubora
unaozingatia fedha zinatolewa.
Aidha
alimnukuu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma ambaye
naye amekuwa akisisitiza ujenzi wa majengo yote ya Mahakama kujengwa kwa kasi
na kwa kuzingatia ubora unaotakiwa ili kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.
Hivyo,
Prof. Ole Gabriel aliwataka Wakandarasi wote kufanya kazi kwa karibu na wasaidizi
wake ili kutatua kero zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao,
mathalani masuala ya malipo.
Aliishukuru
Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi
wa miundombinu ya Mahakama na kuwaahidi Wakandarasi hao kuwalipa fedha zao kwa wakati
kwa wale watakaokamilisha taratibu kulingana na mikataba ya ujenzi.
Hata
hivyo, Prof. Ole Gabriel aliwakumbusha kuwa wakandarasi watakaochezea fedha za
umma zinazotumika kwenye utekelezaji wa miradi ya Mahakama hawataonewa haya. Alifafanuzi
kuwa sio tu wakandarasi hao watavunjiwa mkataba bali pia watachukuliwa hatua za
kisheria ikiwemo kushitakiwa kama watathibitika kujihusisha na vitendo hivyo.
“Msimamie
miradi yenu kwa ukaribu na kwa kuzingatia thamani ya fedha za serikali kwani
fedha hizo sio shamba la bibi”, alionya.
Mtendaji
Mkuu akawashauri wakandarasi wote kuajiri wataalamu wenye sifa katika
kutekeleza majukumu yao ya kimikataba, mfano kwenye maeneo ya masoko, waasibu,
mainjinia na washauri wa miradi wenye uzoefu wa kutosha ili kuimarisha kampuni
zao na kuondoa kasumba ya kutolipa watumishi kwa wakati, hivyo kuwajengea imani
kwa wateja wao.
“Natamani
wote twende pamoja na tushirikiane kwa hali zote, yaani Mahakama, Mkandarasi na
Mkandarasi Mshauri ili tuwe kitu kimoja na kutatua changamoto zetu kwa pamoja
ili kukamilisha miradi hii ndani ya wakati unao kubalika”, aliongeza.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama alitumia wasaa huo kuwakumbusha viongozi wa Mahakama
wanaoratibu tenda za miradi ya Mahakama kuajili wakandarasi wenye uwezo wa
kutekeleza miradi hiyo ili imalizike kwa wakati na kuangalia namna bora ya
kuwatumia wazabuni wenye gharama za chini.
Prof
Ole Gabriel alisema hadi hivi sasa Tanzania Bara ina Mahakama za Mwanzo 960, Mahakama
za Wilaya 120 , Mahakama za Hakimu Mkazi 30, Mahakama Kuu 18 , Mahakama ya Rufani
mmoja(1) na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika mikoa mitano.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel (katikati) akizungumza leo tarehe 22 Februari, 2022 jijini Dar es
salaam na Wakandarasi (hawapo katika picha) wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa
majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Wengine ni Mtendaji
wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania Solanus Nyimbi(kulia) na Mtendaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Leonard Magacha(kushoto).
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo wa Mahakama
ya Tanzania Mhandisi Khamadu Kitunzi akitoa mada kuhusu hali ya maendeleo ya
ujenzi wa miundombinu ya Mahakama katika maeneo mbalimbali wakati wa mkutano wa
siku moja wa Wakandarasi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.
Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha) uliofanyika leo tarehe 22 Februari,
2022.
Mhandisi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Moladi Tanzania
Limited Noel Sylvester akichangia wakati wa mkutano wa Wakandarasi hao.
Meneja Mradi wa Kampuni ya Ujenzi ya Charles Limited John Bogomba akichangia wakati wa mkutano huo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel (katikati) akimuhoji Mkandarasi mshauri wa miradi ya Mahakama Bw. Boniface Charles (aliyesimama) kuhusu maendeleo ya miradi wakati wa kikao hicho na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa
majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni