Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.
Serikali
ya Tanzania imeingia makubaliano na Benki ya Dunia kuendelea kuifadhili
Mahakama ya Tanzania katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo awamu ya pili
ambapo Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vingine tisa pamoja na Mahakama za Mwanzo
60 zitajengwa kote nchini.
Akizungumza
leo tarehe 28 Februari, 2022 na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa na
Mahakama za Mwanzo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya kimahakama,
Kanda ya Songea, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema
kuwa uwezeshaji huo kutoka Benki ya
Dunia na Serikali ya Tanzania utasaidia kupunguza changamoto zilizopo.
“Tayari
Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia wameingia katika makubaliano ya
kuendelea kuifadhili Mahakama ya Tanzania katika awamu ya pili ya uboreshaji na
wapo katika hatua za mwisho za kukubaliana, kiasi kwamba tutajenga Vituo Jumuishi
vya Utoaji Haki vingine tisa katika mikoa ambayo haina Mahakama Kuu,” alisema.
Alibainisha
pia kuwa ufadhili huo utaiwezesha Mahakama ya Tanzania kujenga Mahakama za
Mwanzo 60, hatua ambayo itakamilishwa ndani ya miaka mitano ijayo, hivyo
kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya miundombinu ya aina hiyo iliyopo kwa
sasa.
Vile
vile, Mhe. Prof. Juma aliwaambia watumishi hao kuwa Mahakama ya Tanzania
imepanga katika bajeti ijayo kujenga jengo la kisasa linaloendana na karne ya
21 la Mahakama ya Wilaya ya Nyasa, ambapo ujenzi huo ulichelewa kutokana na
ufinyu wa bajeti. Alisema kuwa ingawa Wilaya ya Nyasa ina miaka 10 tangu
kuanzishwa kwake, bado ni mpya kimahakama kwa vile haina huduma za Mahakama za
Wilaya.
“Tulikuwa
tumepanga mwaka jana tuwe tumejenga Mahakama za Wilaya 25 ikiwemo Mahakama ya
Wilaya ya Nyasa, lakini hali ya kibajeti haikukaa vizuri. Lakini
nimehakikishiwa katika bajeti ijayo Mahakama ya Wilaya ya Nyasa ni moja kati ya
Mahakama ambazo zitajengwa. Zitajengwa Mahakama za kisasa ambazo zinaendana
na karne ya 21 ambayo inategemea teknolojia,” alisema.
Jaji
Mkuu amewapongeza watumishi kwa kukubali dhana ya uboreshaji na kuanza kuitekeza,
ambapo usajili wa mashauri kwa sasa
unafanyika kwa njia ya mtandao katika Mahakama zote hapa nchini. “Leo asubuhi
nilikuwa napitia mtandao wetu wa kusajili mashauri, hakuna Mahakama Tanzania
ambayo inasajili mashauri kwa mtu kwenda mahakamani. Kwa hiyo, tumepiga hatua
kubwa sana na safari ya Mahakama Mtandao ndiyo tumeanza na ninawaomba tuwe
pamoja,” alisema.
Katika
ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu atatembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya
ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kuhitimisha ziara hiyo kwa
kutembelea Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na
Mahakama Kuu Songea. Katika maeneo yote atakayopitia, Mhe. Prof. Juma atakagua
shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na
watumishi wa kada zote.
Katika
ziara hiyo, Jaji Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu,
wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mtendaji wa
Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Bw. Leonard Magacha.
Wengine
ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe.
Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw.
Jovin Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice
Patrick na mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes
Mombury.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela
Moshi, Naibu Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda,
Bw. Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Songea, Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian
Haule, Mhasibu, Bw. Japhet Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza leo tarehe 28 Februari, 2022 na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa na Mahakama za Mwanzo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya kimahakama, Kanda ya Songea,
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa , Mhe Osmund Ngatunga akieleza taarifa ya utendaji ya Mahakama yake.
Viongozi waliofuatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye ziara yake (picha juu na chini) kutoka Makao Makuu na Kanda wakimsikiliza wakati alipokuwa anaongea na watumishi.Sehemu ya watumishi wa Mahakama (picha juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu (picha ya juu) na watumishi (picha ya chini) wa Mahakama ya Wilaya na Mwanzo. Wengine waliokaa kulia kwa Jaji Mkuu ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni