Alhamisi, 3 Machi 2022

JAJI MKUU AMALIZA ZIARA KANDA YA SONGEA NA KUAHIDI NEEMA KWA WATUMISHI

 Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Songea kwa kutembelea Mahakama ya Mwanzo Songea, Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na Mahakama Kuu Songea kabla ya kuongea na watumishi kwenye kikao cha majumuisho na kuahidi kuchukua hatua zitakazosaidia kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Baadhi ya hatua hizo ni kuzitazama Mahakama za Mwanzo kwa jicho la kipekee kibajeti, kuimarisha miundombinu mbalimbali katika ngazi zote ikiwemo ujenzi wa majengo ya Mahakama, hususani Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi kwa lengo la kuimarisha ufanisi kazini. Aidha, Mhe. Prof. Juma amewapongeza watumishi wote katika Kanda hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.

Akiwa katika Mahakama hizo, Jaji MKuu alipokea taarifa za utendaji kutoka kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi, kabla ya kupata taarifa jumuishi iliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea katika Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Sekela Moshi.

Katika taarifa yake iliyosheheni mambo mengi, Mhe. Moshi amesema, pamoja na mambo mengine, “Mkoa wa Ruvuma unasimamiwa na Mahakama Kuu moja, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea moja, Mahakama za Wilaya tano (Songea, Nyasa, Namtumbo, Mbinga na Tunduru) na Mahakama za Mwanzo 47 katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama katika utoaji haki kwa wananchi. Kati ya Mahakama za Mwanzo 47, zinazofanya kazi ni 35.”

Akizungumzia usikilizaji wa mashauri, Jaji Mfawidhi huyo amemweleza Jaji Mkuu kuwa katika ngazi ya Mahakama Kuu kati ya Januari na Desemba 2021 mashauri 214 yalifunguliwa, mashauri 233 yaliamuliwa na yaliyobaki yalikuwa 94, wakati katika kipindi cha Januari hadi Februari, 2022 mashauri 23 yamefunguliwa, yaliyoamuliwa ni 32 na yaliyobaki ni 85.

Amesema katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, kati ya Januari  na Desemba mwaka 2021 yalifunguliwa mashauri 32, yaliyoamuliwa yalikuwa 40 na yaliyobaki yalikuwa 36, ambapo katika kipindi cha Januari  na Februari 2022, mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa sita, yaliyoamuliwa ni mashauri nane na  yaliyobaki yalikuwa 34, huku mashauri mawili yakionekana ni ya mlundikano.

Kwa upande wa Mahakama za Wilaya, Mhe. Moshi amesema kuwa kati Januari  na Desemba mwaka 2021 yalifunguliwa jumla ya mashauri 1,048, yaliyoamuliwa yalikuwa 969 na yale yaliyobaki ni 479, wakati katika kipindi cha  Januari  na Februari 2022, jumla ya mashauri ambayo yamefunguliwa ni 132, yaliyoamuliwa ni 127 na yamebaki mashauri 510.

Hata hivyo, Jaji Mfawidhi huyo amemweleza Mhe. Prof. Juma kuwa Mahakama Kanda ya Songea ina mashauri mengi ya uhujumu uchumi kutokana na baadhi ya Wilaya kuzungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere (zamani ikiitwa Selous Game Reserve) na kwamba Kanda hiyo inapakana na nchi jirani, jambo linalosababisha wahalifu kuingia nchini pamoja na mashahidi na washtakiwa kukimbilia kwenye nchi hizo.

“Tumejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mashauri ya muda mrefu mahakamani yanaisha na kuzuia mlundikano (Backstopping). Mikakati hiyo ni usikilizwaji mfululizo na kuahirisha kwa muda mfupi mashauri yaliyokaa muda mrefu, kuwa na  kikao maalum cha kuondosha mashauri ‘special clean up session’ kila baada miezi miwili,” amesema.

Mhe. Moshi ametaja mikakati mingine ni kupanga mashauri mengi ya kusikiliza kupitia kwa Majaji waliopo na Mahakimu wanne wenye mamlaka ya ziada waliopo (extended jurisdiction), kuwa na vikao vya Kamati za Kusukuma Mashauri ya jinai (Case Flow Management Meetings) na Kamati za Kusukuma Mashauri ya madai (BenchBar Management Meetings).

Katika kikao hicho cha majumuisho, Jaji Mkuu alitoa fursa kwa watumishi wa kada zote kueleza changamoto zinazowakabili wakati wanapotekeleza majukumu yao ambapo viongozi walioambatana naye katika ziara yake waliweza kutoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na kuamsha furaha kutoka kwa watumishi hao mara kwa mara kufuatia majibu mazuri na ya kina yaliyotolewa.

Kabla ya kutembelea Mahakama hizo, Mhe. Prof. Juma alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema na kufanya naye mazungumzo mafupi. Mkuu huyo wa Wilaya amemhakikishia Jaji Mkuu kuwa Serikali katika Mkoa huo itaendelea kushirikiana na Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Katika ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru. Katika maeneo yote aliyopitia, Mhe. Prof. Juma amekagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.

Jaji Mkuu aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama ya rufani, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick na mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela Moshi, Naibu Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda, Bw.  Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Songea, Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian Haule, Mhasibu, Bw. Japhet Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma leo tarehe 3 Machi, 2022 katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo alipokuwa akiongea na watumishi wa Mahakama, Kanda ya Songea leo tarehe 3 Machi, 2022 katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya kikazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akidokeza jambo katika kikao cha majumuisho ya ziara aliyoifanya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Kanda ya Songea.

Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi akijibu moja ya hoja zilizoibuliwa na watumishi katika kikao hicho.

Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba akitoa taarifa kwa watumishi namna Mahakama ya Tanzania inavyoshughulikia changamoto ya ukosefu wa mtandao ili kurahisisha shughuli za kimahakama.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Songea wakiwa ofisini wakati Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipotembelea Mahakama hiyo.
Sehemu ya watumishi (picha ya juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).

Sehemu nyingine ya watumishi (picha ya juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni