Alhamisi, 3 Machi 2022

JAJI MLACHA AZINDUA KAMATI YA MAWAKILI MKOA WA KIGOMA

 

 Na Festor Sanga – Mahakama Kuu- Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amezindua Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma,huku akiwataka wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.

Uzinduzi huo, ulifanyika katika ofisi za Mahakama hiyo tarehe 02 Machi, 2022.

“Tendeni majukumu yenu kwa mujibu wa sheria na msiende nje ya mipaka yenu” alisema Jaji Mlacha.

 Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanabuni njia za kuifanya ijulikane kwa Umma ili wenye malalamiko dhidi ya wakili wajue pa kuyapeleka na kusema kuwa kamati hiyo ijiweke kwenye nafasi ya ulezi wa mawakili.

Baada ya uzinduzi, kamati hiyo ilianza kazi kwa kujengeana uwezo kwa kupitia sheria iliyoianzisha (The written laws (Miscellaneous Amendments) (No.3) Act, 2021 na kujua muundo na majukumu yake.

Akitoa mada katika mafunzo hayo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kuwa sheria iliyoiunda ilianza kutumika rasmi tarehe 11 Oktoba, 2021 tangu ilipotangazwa na Gazeti la Serikali na kuongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kamati hizo za mikoa kulikuwepo na kamati moja tu ya kitaifa ikishughulika na mawakili wote.

Kutokana na idadi ya mawakili kuongezeka kila mwaka, ililazimu kuanzishwa kwa kamati hizo za mikoa ili kuratibu na kusimamia maadili na mienendo ya mawakili katika maeneo husika.

Kwa mujibu wa sheria hiyo wajumbe wanaounda kamati hiyo ni pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ambaye ni Mwenyekiti, Wakili wa Serikali au Mwendesha Mashtaka wa Mkoa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili(Chapter Convener)  ambao ni wajumbe. 

Aidha sheria hiyo inaitaka kamati hiyo kuteua Afisa yeyote mwenye taaluma ya sheria ambaye atakuwa Katibu wa Kamati. Kwa kuzingatia kifungu cha 4 A (2) cha sheria hiyo kamati ilimteua Mhe. Anna Kahungu kwa Katibu wa Kamati.

Aidha, Kamati hizo za Mikoa zinapaswa kutuma taarifa ya Utendaji kazi za kila robo mwaka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Lameck Mlacha(katikati) akifafanua jambo mbele ya wajumbe Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma.

Wajumbe wa Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma wakichukua nasaha za Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Mlacha. (hayupo pichani)

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma Mhe Gadiel Mariki(katikati) na Katibu wa Kamati ya Mawakili Mhe. Anna Kahungu wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Mlacha.

Picha ya Pamoja ya Kamati ya Mawakili Mkoa wa Kigoma (wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Gadiel Mariki, wa pili kulia ni Katibu wa Kamati Mhe. Anna Kahungu, (wa kwanza kushoto) ni Mjumbe Bw. Daniel Rumenyela na wa kwanza (kulia) ni mjumbe Bw. Riziki Matitu.
(Picha na Festor Sanga- Mahakama Kuu -Kigoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni