Alhamisi, 3 Machi 2022

MKUU WA WILAYA APALILIA UMUHIMU KAMATI ZA MAADILI MAHAKAMANI

 Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema amewashauri Watanzania kutumia Kamati za Maadili za Mahakama ya Tanzania kutatua malalamiko waliyonayo dhidi ya maafisa wa Mahakama pale wanapohisi hawakutendewa haki wanapotafuta huduma za utoaji haki mahakamani.

Akizungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma walipokutana Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma leo tarehe 3 Machi, 2022 katika siku yake ya mwisho ya ziara ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea Mhe. Mgema amesema kuwa mbali na uwepo wa Mahakama ambayo ndiyo inayotoa haki, kuna Kamati za Maadili za Mahakama ambazo husikiliza malalamiko dhidi ya maafisa wa Mahakama.

“Mkuu wa Mkoa ameshatoa maelekezo kupitia kwa Mwanasheria katika ofisi (yake) aweze kwenda kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani kuwafahamisha uwepo wa Kamati za Maadili za Mahakama kwenye ngazi ya Wilaya na Mkoa ili kama kuna mwananchi anafikiri amefanyiwa jambo ambalo anaona ni la ukiukwaji wa maadili aweze kutoa malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya, kwa maana ngazi zile za Mahakama ya Mwanzo, lakini pia kwa Mkuu wa Mkoa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwa maafisa kwenye Mahakama anazozisimamia,” amesema.

Amesema kuwa Kamati hizo ni chombo na silaha muhimu ambayo itasaidia kuondoa malalamiko kwa wananchi. “Tunahitaji wananchi wakihudumiwa waone kwamba kile ambacho wamepata ni stahiki yao. Vinginevyo, tutaendelea kushirikiana. Tunao ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi zile za chini mpaka kwa Jaji Mfawidhi,” Mkuu huyo wa Wilaya alimweleza Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Mgema aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua nzuri iliyochukua kuboresha miundombinu ya majengo ya Mahakama, ikiwemo kujenga Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika Kanda ya Songea, ambacho kitatoa huduma za kimahakama kutoka ngazi ya Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.

“Hili la ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki tunalisubiri kwa hamu sana. Jengo hilo litatatua ile changamoto ya wananchi kusafiri mwendo mrefu kwenda Iringa kufuata huduma za Mahakama ya Rufani,” alisema.

Awali, Mkuu huyo wa Wilaya alimwomba Jaji Mkuu kuangalia uwezekano wa kuwa na huduma zote za utoaji haki kupatikana sehemu moja ili haki iweze kupatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Kathalika, Mhe. Mgema alibainisha kuwa wanatambua mabadiliko makubwa ndani ya Mahakama, hasa kwenye eneo la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kusikiliza na kuamua mashauri mbalimbali. Alisema kuwa kama Serikali wanaipongeza Mahakama kwa hatua hizo, ingawa bado kuna changamoto, lakini anauhakika zitashughulikiwa.

“Tunashukuru sana Jaji Mkuu kwa mchakato huo ambao umeuanzisha na umeshaanza kufanya kazi na umeonyesha mafanikio chanya na makubwa. Kadri tunapoboresha huduma za utoaji haki tunaifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani,” amesema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Songea. Katika ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru. Katika maeneo yote aliyopitia, Mhe. Prof. Juma amekagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema akifafanua jambo alipokuwa anaongea na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akieleza jambo alipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akiwa katika ziara ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea.
Viongozi wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Ruvuma wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wakati Jaji Mkuu  wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipotembelea ofisi hiyo.
Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.  Kutoka kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina. 

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina akitambulisha viongozi walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye ziara yake ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema zawadi ya kalenda ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema pamoja na viongozi wengine wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Ruvuma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni