Na Innocent Kansha – Mahakama, Songea
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema katika ziara yake
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea amehimiza sana matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na azma ya kuwa na Mahakama Mtandao katika
ngazi zote za Mahakama ili kusogeza huduma karibu na wananchi hii itasaidia
kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa kuhitimisha ziara yake ya
kikazi Kanda ya Songea leo tarehe 3 Machi, 2022, Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma
alisema, Mahakama za Mkoa wa Ruvuma zimejitahidi katika matumizi ya TEHAMA
hususani katika ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na ujazaji wa takwimu
za mashauri kwa mtandao.
“Nimefarijika
kuona majengo na viwanja vinavyomilikiwa na Mahakama vina hati miliki na
vimewekwa katika mfumo wa kielekitroniki wa utambuzi wa majengo na mazingira
yanayozunguka majengo (JMAP)”, alisema Jaji Mkuu
Aidha,
Prof Juma alisema, Mkoa wa Ruvuma una changamoto kubwa ya miundombinu ya
Mahakama. Hali hiyo alijionea mwenyewe na imebainishwa pia na viongozi wa
Serikali na wananchi wakati wa ziara hiyo. Ziara yake Mkoa wa Ruvuma ilimkumbusha
kuwa, pamoja na hatua kubwa ambayo Mahakama imepiga katika maboresho ya
miundombinu, mahitaji ya majengo ya Mahakama bado ni makubwa.
Mhe.
Jaji Mkuu alitoa takwimu za Mkoa wa Ruvuma kuwa una jumla ya vituo vya Mahakama
54 vya ngazi mbalimbali kuanzia Mahakama Kuu (Songea), Mahakama ya Hakimu Mkazi
(Songea), Mahakama za Wilaya 5 (Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru), na
Mahakama za Mwanzo.
Kati
ya vituo hivyo 54, ni majengo 15 tu ambayo hali yake inatajwa katika mipango ya
Mahakama kuwa ni “nzuri”, na vituo 35 hali ya majengo yake imetajwa kuwa sio
nzuri. “Yapo majengo ya Mahakama za Mwanzo yaliyofungwa kwa ajili ya uchakavu
uliofikia hatua ya hatarishi kwa watumiaji. Kati ya Majengo 54, ni majengo 39
tu ndio yanamilikiwa na Mahakama, Majengo 15 ni ya kuazimwa kutoka Serikali za
Mkoa, Wilaya, Kata, Vijiji au zinalipiwa pango kwa wanananchi. Kwa mfano,
majengo yanayotumiwa na Mahakama ya Wilaya Songea, na Mahakama ya Mwanzo Songea
Mjini, yameazimwa kutoka Sekreterieti ya Mkoa wa Ruvuma”, aliongeza Jaji Mkuu.
Kwa
upande wa miundombinu ya Majengo nchini Jaji Mkuu, alisema Mahakama imejipanga
kupunguza changamoto ya miundombinu ya majengo ya Mahakama kwa nchi nzima
ikiwemo Mkoa wa Ruvuma.
“Tunao
Mpango Mkakati wa Miundombinu na sasa tunauboresha ili kuzingatia uhalisia wa
maeneo na changamoto mahususi za maeneo husika. Kwa mfano katika mwaka ujao wa
fedha 2022/2023 mpango wetu ni kujenga maeneo yafuatayo ya mkoa wa Ruvuma.
Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki cha kisasa hapa Songea kitakachokuwa na Mahakama ya
Wilaya ya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Sehemu ya Mahakama
ya Rufani. Aidha, kituo hicho kitakuwa pia na ofisi za Wadau muhimu wa utoaji
wa huduma ya haki, pia tutajenga Mahakama ya Wilaya ya Nyasa na Mahakama za
Mwanzo nne (4) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma”, alitoa ufafanuzi
huo Jaji Mkuu.
Prof.
Juma alisema, kwa ujumla, kuanzia mwaka ujao wa fedha yaani 2022/2023 Mahakama
ya Tanzania inategemea kujenga majengo ya Mahakama za Mwanzo 60 kwa kutumia
fedha za mradi wa Benki ya Dunia na majengo ya Mahakama za Mwanzo 10 yatajengwa
katika maeneo magumu kufikika. Katika maeneo hayo kutajengwa jengo la Mahakama
na nyumba za mahakimu.
Vile
vile majengo ya Mahakama Kuu, Vituo Jumuishi 12 vitajengwa ambapo kati ya hivyo
vituo 9 ni vya Mikoa isiyokuwa na Mahakama Kuu na vituo 3 ni Mikoa yenye
Mahakama Kuu ambayo majengo yake ni chakavu na hayakidhi mahitaji muhimu ya
kutolea huduma kama jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Songea, aliongeza Prof. Juma
Kwa
upande mwingine Jaji Mkuu huyo alisema, Mahakama inatambua kuhusu upungufu
mkubwa wa watumishi iliyonao. Mahitaji halisi ya watumishi ni takribani elfu
kumi. Lakini watumishi waliopo ni takribani 5,830. Kwa Kanda ya Songea,
mahitaji yao ya watumishi ni 336 lakini waliopo ni 179. Kwa hiyo kuna upungufu
wa watumishi 157. Hivyo Mahakama itaendelea kushirikiana na Serikali kutatua
changamoto hiyo kwa awamu.
Jaji
Mkuu alitolea mfano kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mahakama imeajiri
watumishi 340. Ni lengo la Mahakama pia mwaka ujao wa fedha itapata kibali cha
ajira mpya kutoka Serikalini.
“Kwa
sababu hizo Mahakama inasisitiza matumizi ya TEHAMA kama namna moja wapo ya
kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi. Tunahimiza pia watumishi
kujiendeleza kusoma taaluma zaidi ya moja (multi skilled personnel) ili waweze
kufanya kazi kwa tija kubwa,” alisema.
Amesema
kuwa kuna uboreshaji mkubwa unaofanyika ndani ya Mahakama kama ilivyo kwa upande
wa Serikali na Bunge. Hata hivyo, amebainisha kuwa pamoja na maboresho ya
miundombinu, Mahakama inasisitiza mabadiliko ya mitazamo na fikra chanya kwa
watumishi wa Mahakama na wadau wetu. Amesma watumishi na wadau wakiwa na fikra
chanya na kufikiri kimkakati, changamoto kwenye mnyororo wa utoaji haki
zitatatuliwa kwa uharaka na hatimaye wananchi kupata huduma zilizo bora.
“Mahakama
imejipanga kuendelea kuboresha usikilizaji wa mashauri kwa lengo la kumaliza
mashauri kwa wakati. Kwa Kanda ya Songea kasi ya usikilizaji wa mashauri ni
nzuri na kwa asilimia kubwa wamefikia malengo ya kumaliza mashauri. Yako
mashauri machache yalibaki mwaka jana lakini ni kutokana na sababu zilizo nje
ya Mahakama kama mashahidi kutofika mahakamani na upelelezi kutokamilika mapema.
Tutawasiliana na wenzetu ili kuondoa changamoto hii ambayo inaweza kuchelewesha
haki kutolewa,”amesema.
Kwa
mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama pia imeweka mipango madhubuti ya kusikiliza kwa
haraka mashauri ya Mirathi na Ndoa. Amesema katika eneo hilo wanaoathirika sana
ni wanawake na watoto, hivyo watafanya kila linalowezekana kuhakikisha mashuri
ya mirathi na ndoa yanamalizika mapema.
Kwa
sababu hiyo tumeanzisha kituo jumuishi cha masuala ya Mirathi na Ndoa pale
Temeke. (kama Pilot Centre). Tutakachojifunza katika kituo hiki kitasaidia kuenezwa
sehemu zingine hapa nchini,” amesema.
Mhe.
Prof. Juma amesema pia kuwa katika ziara ya Mkoa wa Ruvuma amepata fursa ya
kuona uhalisia wa mazingira ya kutolea haki ikiwemo miundombinu ya majengo,
ukubwa wa maeneo yanayohudumiwa na Mahakimu na umbali wa vituo vya kutolea
haki.
“Nimepokea
maoni na mapendekezo ya wadau wetu kuhusu utendaji wa kazi za Mahakama na maoni
yao ya namna ya kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa haki. Nimefariji kwa
maoni na mapendekezo yao. Niliwaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale yanayohusu
Mhimili wa Utawala (Serikali) tutayawasilisha kwa wahusika na naamini watayafanyia
kazi,”amesema.
Aidha,
Jaji Mkuu alibainisha kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa na uongozi wa Mahakama
kwa kushirikiana na Serikali ili kutatua changamoto ya uchache wa watumishi
kadri bajeti itakavyoruhusu.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni