Jumapili, 6 Machi 2022

WATUMISHI WANAWAKE DIVISHENI YA UHUJUMU UCHUMI WATOA MSAADA KWA WAZAZI SINZA

 Watumishi Wanawake wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakiongozwa na Jaji wa Divisheni hiyo, Mhe. Immaculata Banzi leo tarehe 06 Machi, 2022 wametoa msaada kwa wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Sinza Palestina jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vitu mbalimbali kwa wazazi, Jaji, Mhe. Immaculata alisema kuwa wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, kila mwaka.

“Lengo la kuja katika hospitali hii ni kuwakumbuka wanawake wenzetu angalau kwa kutoa mkono wa pole na pia kuwapongeza kwa kujifungua salama, hii ni katika kusherehekea Sikukuu ya Siku ya Wanawake Duniani,” alisema Jaji huyo.

Watumishi hao wametoa vitu mbalimbali kwa wazazi hao ikiwa ni pamoja na Vitenge, Kanga, Taulo za kike, dawa za meno, sabuni za kufulia na kadhalika.

Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Immaculata Banzi (wa pili kulia) pamoja na Watumishi wengine wa Divisheni hiyo wakiwa katika Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Sinza kutoa msaada kwa Wazazi waliojifungua katika Hospitali hiyo. Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 06 Machi, 2022. Wa tatu kulia ni Mtendaji wa Mahakama hiyo- Bi. Masalu Kisasila na kwanza kulia ni Muuguzi Kiongozi wa zamu wa Hospitali hiyo, Bi. Francisca Konyani.

Sehemu ya Watumishi Wanawake wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa Uchumi wakishusha vitu mbalimbali kwa ajili ya kutoa msaada kwa Wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Sinza Palestina jijini Dar es Salaam.

 Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Immaculata Banzi akimpatia baadhi ya vitu mmoja kati ya wazazi waliopatiwa mkono wa pole katika hopitali ya Sinza Dar es Salaam. 

 Muuguzi Kiongozi wa zamu wa Hospitali ya Sinza, Bi. Francisca Konyani akiwaeleza jambo Watumishi Wanawake wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kabla ya kuanza kwa zoezi la kutoa msaada kwa wazazi waliojifungulia katika Hospitali hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Immaculata Banzi akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi Wanawake wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (katikati) na Watumishi wa Hospitali ya Sinza. Wa tatu kulia ni Naibu Msajili wa Divisheni hiyo, Mhe. Magdalena Ntandu.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni