Na Festor Sanga- Mahakama Kuu Kigoma
Shirika la
Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) kupitia ofisi ndogo ya Kigoma limetoa vifaa vya kielektroniki kwa lengo
la kuunga mkono jitihada za zinazofanywa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Kigoma kuelekea Mahakama Mtandao ili kuwezesha utoaji wa huduma za haki kwa
wakati na kwa wote.
Vifaa
vilivyopokelewa na Mahakama hiyo katika hafla iliyofanyika hivi karibuni ni seti
tatu za kompyuta-Desktop, Printer tatu (Multifunctional) na UPS tatu.
Akikabidhi
vifaa hivyo kwa uongozi wa Mahakama hiyo, Mwakilishi wa UNHCR ofisi ndogo ya
Kigoma Bw. Peter Muriyuki alisema kuwa wakimbizi wananufaika na huduma
zitolewazo na Mahakama hivyo wameona ni vyema kuunga mkono juhudi za uboreshaji
ili kurahisisha huduma za utoaji wa haki.
“Tunatambua
kuwa mahitaji ya huduma ya haki yameongezeka kutokana na uwepo wa kambi za
wamkimbizi za Nduta- Kibondo na Nyarugusu-Kasulu hivyo tumeona tuunge mkono uboreshaji
unaoendelea ndani ya Mahakama hususan, matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ili huduma za Mahakama ziweze kutolewa kwa wakati.Tutaendelea
kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa vifaa vya TEHAMA, mafunzo na maeneo
mengine ya ushirikiano” alisema Bw. Muriyuki.
Wakati
huohuo, Mahakama hiyo ilikabidhi vifaa vya TEHAMA zikiwemo Laptop mbili (2) kwa
Uongozi wa Gereza la Kwitanga (Kigoma) na Ilagala (Uvinza) ili kuwezesha
usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.Vifaa hivyo vilivyonunuliwa na
Mahakama ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa ndani wa kuhakikisha kila gereza
linakuwa na huduma ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.
Awamu ya kwanza Mahakama hiyo, ilitoa vifaa
kama hivyo katika Magereza ya Kasulu na Kibondo na kufanya hadi sasa Magereza
yote matano katika Kanda kuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri kwa njia ya
matandao.
Akitoa
neno la shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Magereza Mkoa, Kamishna Msaidizi wa
Magereza Bw. Edwin Kusiluka alisema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo kutatua malalamiko
ya wafungwa wanaotoka nje ya Mkoa wa Kigoma ambao wako Magereza ya Kwitanga na
Ilagala (Magereza ya Kilimo) ambao awali walilazimika kusafirishwa kwenda
Gereza la Bangwe ambalo lina miundombinu wezeshi kwa mifumo ya TEHAMA kwenda
kusikiliza rufaa za kesi zao kwa njia ya Mtandao.
“Tunaishukuru
Mahakama kwa vifaa hivi tulivyokabidhiwa. Vifaa hivi vitasaidia katika utoaji
wa haki kwa wakati,kupunguza gharama za kutoa wafungwa Gereza la Kwitanga na
Ilagala hadi Kigoma na kuongeza utulivu na amani magerezani, hivyo tunaahidi
kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhudi za uboreshaji huo kuelekea Mahakama
Mtandao,” alisema Kusiluka.
Naye
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Lameck
Mlacha aliushukuru uongozi wa UNHCR ofisi ndogo ya Kigoma kwa kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao.
Aidha
alitoa rai kwa Uongozi wa Magereza kupaza sauti ya pamoja ili uboreshaji unaoendelea
ndani ya Mahakama uende sambamba na uboreshaji wa magereza kimiundombinu ili
kuruhusu matumizi ya TEHAMA.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck
Mlacha(kushoto) akipokea baadhi ya vifaa vya TEHAMA kutoka kwa Mwakilishi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Wakimbizi UNHCR ofisi ndogo ya
Kigoma Bw. Peter Muriyuki (katikati) na kulia ni Bi Rehema Msami wa UNHCR.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Lameck Mlacha (kushoto)akimkabidhi
kompyuta mwakilishi kutoka Gereza la Ilagala Inspekta Mangole.
Wadau
wa Mahakama na watumishi wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Lameck Mlacha (hayupo pichani)
Kamishna
Msaidizi wa Jeshi la Magereza Edwin Kusiluka akitoa neno la shukrani kwa niaba
ya Uongozi wa Jeshi la Magereza Mkoani Kigoma.
Jaji
mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Kigoma Mhe Jaji Lameck Mlacha(wa pili kulia)
pamoja na Mwakilishi wa UNHCR Ofisi Ndogo ya Kigoma Bw. Peter Muriyuki( wa pili
kushoto) wakiweka sahihi hati ya makabidhiano. Wa Kwanza kulia ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma
Mhe. Rose Kangwa na wa kwanza kushoto ni Bi Rehema Msami kutoka UNHCR
wakishuhudia tukio hilo la uwekaji sahihi hati ya makabidhiano.
(Picha
na Festor Sanga- Mahakama Kuu Kigoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni