Alhamisi, 3 Machi 2022

KANDA YA TABORA YAWEKA MKAKATI WA KUSOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI

 

Na Aisha Abdallah- Mahakama Kuu Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamisi ameupongeza uongozi wa Kijiji cha Kipili kwa kutenga eneo hekari mbili kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama.

Aidha Jaji Khamisi ametoa pongezi hizo, ikiwa ni hatua ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama hiyo, wa kusogeza huduma kwa wananchi katika kata zisizokuwa na mahakama.

Eneo hilo limetolewa na uongozi huo, baada Jaji Khamisi kufanya ziara katika kata ya Kipili, iliyopo wilayani Sikonge ambapo aliambatana na viongozi wengine wa Mahakama wa kanda hiyo na kufanya mazungumzo na uongozi huo.

Katika ziara hiyo viongozi wa Mahakama wa kanda ya Tabora walikutana na viongozi wa kijiji cha kipili na kuwaeleza lengo la ziara hiyo.

‘‘Kata ya Kipili ni miongoni mwa kata ambazo Mahakama inaziangalia kwa jicho la karibu kwa kuwa zipo mbali na huduma za kimahama,’’ alisema Jaji huyo.

Aliongeza kuwa kata hiyo ipo umbali wa kilometa 360 kutoka makoa makuu ya Wilaya ya Sikonge na kuwa na wakazi takribani elfu ishirini na mbili kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, ambapo kwa hali ya sasa idadi hiyo ya watu itakuwa imeongezeka, hivyo kuhitaji huduma za kimahakama.

Katika mazungumzo hayo uongozi wa kijiji cha hicho, uliongozwa na Diwani wa kata hiyo, Daniel Salumu.

Diwani wa kata ya Kipili, Daniel Salumu(katikati aliyevaa koti) akiwa pamoja na viongozi wa serikali ya Kijiji hicho  wakijadili jambo na, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Mhe. Amour Khamisi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Amour (kushoto) Khamisi akijadiliana jambo na uongozi wa kijiji cha Kipili kuhusu eneo hilo la hekari mbili.

Baadhi ya viongozi wa Mahakama hiyo wakiwa  Tabora katika kiwanja kilichotegwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo wakijadiliana jambo kwenye eneo hilo.

 ( Picha na  Aisha Abdallah- Mahakama Kuu Tabora)

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni