Alhamisi, 3 Machi 2022

UCHELEWESHAJI MASHAURI SI TATIZO LA MAHAKAMA: MKUU WA WILAYA MTATIRO

Na Innocent Kansha – Mahakama, Songea.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mhe. Julius Mtatiro amesema utafiti mdogo uliofanyika katika wilaya yake unaonyesha malalamiko mengi katika eneo la ucheleweshaji wa mashauri sio la Mahakama bali ni sehemu ya wadau wa haki jinai kutotimiza majukumu yao kwa wakati hasa kwenye upelelezi.

Akizungumza Ofisi kwake alipokutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 2 Machi, 2022, Mjini Tunduru wakati wa ziara ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama Wilayani hapo, Mhe. Mtatiro alisema, zamani malalamiko makubwa ya wananchi kwa Mahakama ilikuwa ucheleweshwaji wa mashauri mbalimbali yanayofikishwa mahakamani.

“Lakini hivi sasa sisi tuliopo huku chini tunaoana hili tatizo mmelitafutia dawa hasa katika kipindi hiki cha uongozi wako kila mwaka umekuwa ukilifanyia kazi kwa uzito wa kipekee na hata kwa upande wa Mahakimu na Majaji tumekuwa tukifanya nao kazi katika Kanda yetu vizuri, hatupati malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kesi zinacheleweshwa na watendaji hao”, Mhe. Mtatiro alimweleza Jaji Mkuu.

Mhe. Mtatiro aliongeza kuwa, bado kuna mazingira na changamoto ambazo yeye binafsi amezishuhudia, hususani upande wa waendesha mashtaka na upelelezi, ambalo ni changamoto kubwa katika hilo eneo. Amesema wananchi wanapowasilisha malalamiko yao Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhusu ucheleweshaji wa mashauri na akiomba taarifa za kujua kiini cha ucheweshaji kutoka kwa viongozi wa Mahakama hubaini sababu kubwa ni za kiupelelezi kutokamilika kwa wakati na hilo ndiyo limekuwa tatizo kubwa.

“Nadhani wenzetu wa Jeshi la Polisi na viongozi wao bado wana kazi kubwa ya kufanya katika hili eneo kwa sababu haki ya mwananchi inapocheleweshwa ni wazi inaleta madhara mengine makubwa sana kiuchumi na kijamii kwa ujumla”, aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya

Akaupongeza uongozi wa Mahakama kwa jitihada kubwa za kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati, kwani matatizo mengi na malalamiko yanayofikishwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya yanayohusu mashauri yaliyoko mahakamani sio ya kimahakama bali ni upelelezi kutokamilika kwa wakati.

Kwa mujibu wa Mhe. Mtatiro, Mahakimu wanatumia kila mbinu kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa haraka kizingiti kinakuwa ni suala la upelelezi kutokamilika kwa wakati.

Aidha, kwa upande wa malalamiko dhidi ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru, Mhe. Mtatiro alimweleza Jaji Mkuu kuwa hakuna malalamiko makubwa dhidi yao kwa vile wanatekeleza majukumu yao vizuri kwa mujibu wa sheria na taratibu na kuendelea kuusaidia Mhimili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kikatiba.

“Tumekuwa tukikutana kwenye vikao mbalimbali ili kujadili kama kuna malalamiko makubwa yanayoelekezwa kwao kutoka kwa wananchi, ni kiri kuwa kwa Wilaya ya Tunduru hakuna malalamiko makubwa dhidi ya Mahakama na watendaji wake kiujumla” aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya

Mkuu wa Wilaya hiyo akatumia wasaa huo kuishauri Mahakama kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama kwani hata upande wa Serikali inamaslahi mapana katika eneo hilo, kwa sababu miundombinu bora inawahusu watu wote, watumishi na wananchi ambao ni watumia wa huduma za kimahakama. Alisema kuwa bado kuna changamoto ya aina hiyo kwenye Wilaya yake.

Mhe. Mtatiro akatoa ahadi mbele ya Jaji Mkuu kuwa ndani ya mwezi mmoja atakamilisha mchakato wa upatikanaji maeneo ya kujenga miundombinu ya majengo kwa kuhakikisha anashirikiana na Mkurugezi na uongozi wa Mahakama wa Wilaya kusaidia kupata maeneo mazuri na makubwa yenye hati kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la kutolea huduma na pengine kupata maeneo zaidi kwa ajili ya makazi ya watumishi kama Mahakama inavyofanya maeneo mengine nchini.

“Mahakama ya sasa imejikita zaidi kutoa huduma zake kwa kwa wananchi kwa kutumia mtandao, hivyo Serikali haina budi kutoa ushirikiano kwa kuboresha miundombinu ya majengo ili mifumo hiyo iweze kuwa katika maeneo salama ya kutolea huduma kwa wananchi”, alisema Mkuu wa wilaya hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimpa maelezo ya jinsi ya kutumia kalenda ya mezani Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro wakati alipomtembelea Ofisini kwake akiwa ziarani wilayani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama leo tarehe 2 Machi, 2022.

 

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro akitolea ufafanuzi mambo kadhaa ya kimahakama mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) wakati alipomtembelea Ofisini kwake akiwa ziarani wilayani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama (hawapo pichani) Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro wakati alipomtembelea Ofisini kwake akiwa ziarani wilayani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea maelezo na utambulisho wa Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Tunduru kutoka kwa mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro wakati alipomtembelea Ofisini kwake akiwa ziarani wilayani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Tunduru wengine mstari wa mbele ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe. Sekela Moshi (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro (wa pili kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Marin Chuma (wa kwanza kulia).

 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro wakati alipomtembelea Ofisini kwake akiwa ziarani wilayani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni