Jumatano, 2 Machi 2022

WATUMISHI MAHAKAMA TUNDURU WAMKOSHA JAJI MKUU

 Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.

Ziara ya kikazi ya kimahakama, Kanda ya Songea anayofanya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma imeingia siku ya tatu ambapo leo tarehe 2 Machi, 2022 ametembelea Mahakama ya Wilaya Tunduru na kuwasifu watumishi wa Mahakama hiyo na Mahakama za Mwanzo kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, ikiwemo kutoa haki kwa wakati.

Akiongea na watumishi wa kada mbalimbali kutoka katika Mahakama hizo, Jaji Mkuu amesema kuwa watumishi kwa sasa wamebadilika kitabia na kimtazamo, hatua iliyotokana na faida kubwa ambayo imepatikana kutoka kwenye uboreshaji wa huduma za kimahakama. Amesema kuwa utoaji wa huduma unaotolewa na watumishi wa Mahakama wa leo ni tofauti kabisa.

Mhe. Prof. Juma amewaomba watumishi hao kuendelea kusimamia zile nguzo tatu ambazo zimesaidia mabadiliko yaliyopo, ikiwemo nguzo ya kwanza ambayo ni Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali. Jaji Mkuu amebainisha kuwa kumekuwepo na uwajibikaji mzuri na utumiaji wa rasilimali ndogo iliyopo uliopelekea kutoa haki kwa mafanikio makubwa.

Vile vile, aliwaomba watumishi hao kuendelea kusimamia nguzo ya pili ya kutoa haki kwa wakati ambapo taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe.Cosmas Kando imeonesha jinsi walivyoshiriki katika kutoa haki kwa wakati na pale haki imechelewa haikuwa ni makosa yao. Aliwaeleza nguzo nyingine ya tatu ambayo pia ni muhimu ni kuendelea kuaminiwa na wananchi.

“Leo asubuhi nimeongea na Mkuu wa Wilaya, amewasifu sana. Ana imani kubwa na Mahakama na amesema malalamiko yanayopelekwa kwake hayatokani na watumishi wa Mahakama, yanatokana na upelelezi na uendeshaji wa mashauri ambayo hayapo kwenye eneo lenu. Kwa hiyo, mwelekeo wenu wa kuhakikisha imani inaendelea kuimarishwa ni muhimu katika shughuli za kila siku,” amesema.

Kadhalika, Jaji Mkuu aliwapongeza watumishi hao kwa namna walivyoshiriki kwenye eneo jingine la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) baada ya kubaini lugha yao kwa sasa ni asilimia 100 ya mashauri kusajiliwa kwa njia ya mtandao.

“Hiyo ni hatua ambayo ni ya kupongezwa kwa sababu tayari mpo katika barabara ya matumizi ya TEHAMA ambayo tunaelekea kwenye Mahakama Mtandao. Hilo ndiyo lengo letu, ifikapo mwaka 2025 tuweze kufanya shughuli zetu zote kupitia mitandao na nyinyi mpo katika nafasi nzuri zaidi kufika safari hiyo,” alisema.

Kabla ya kuongea na watumishi hao wa Mahakama, Mhe, Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo alibainisha kuwa mlundikano uliopo kwenye Mahakama ya Wilaya ya Tunduru unatokana na mashauri ambayo Mahakama haina mamlaka.

Alisema kuwa mashauri hayo yamechelewa kutokana na kutokamilika kwa upelelezi, hatua ambayo inasababisha ule mzigo kushindwa kuutua na kuupeleka Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuyasikiliza. Hivyo aliwaomba wote wanaohusika na upelelezi, uendeshaji wa mashitaka kutumia takwimu za Mahakama ili waweze kujua wapi kuna ucheleweshaji mkubwa.

“Vile vile naomba Hakimu Mfawidhi pakitokea mlundikano ambao unasababishwa na upelelezi, peleka (taarifa) kwa wahusika na kwa kuwa nchi yetu kuna ngazi za viongozi, kama hakuna majibu nenda katika mkoa na kama mkoa hautoi majibu nenda kwa (Mkurugenzi wa Mashitaka) DPP mwenyewe Dar es Salaam,” Jaji Mkuu alishauri .

Mhe. Prof. Juma alitoa pongezi za dhati kwa DPP Silyvester Mwakitalu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa muda mfupi, ambapo amepunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa mashauri. “Yeye (DPP) ni msikivu sana, ukimjulisha tu huwa anachukua maamuzi ya haraka,” alisema.

Katika ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu atatembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kuhitimisha ziara hiyo kwa kutembelea Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na Mahakama Kuu Songea. Katika maeneo yote atakayopitia, Mhe. Prof. Juma atakagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.

Jaji Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama ya Rifani, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick na mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela Moshi, Naibu Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda, Bw.  Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Songea, Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian Haule, Mhasibu, Bw. Japhet Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongea na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru na Mahakama za Mwanzo leo tarehe 2 Machi, 2022 alipokuwa katika ziara ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi akimkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuongea na watumishi hao.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru, Mhe.Cosmas Kando akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama hiyo.


Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na watumishi baada ya kusomwa taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Wilaya ya Tunduru.



Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikifuatilia taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Wilaya ya Tunduru katika kikao cha watumishi. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe, Wilbert Chuma. 

Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Wilaya ya Tunduru. Picha ya juu kutoka kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina, Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Warsha Ng’umbu, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi na Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin Constantine. Picha ya chini kutoka kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick.


Sehemu ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania (picha ya juu na chini) na watumishi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).




Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tunduru na Mahakama za Mwanzo (picha mbili za juu na moja chini). Waliokaa kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe, Wilbert Chuma. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni