Na Innocent Kansha – Mahakama, Songea
Mkuu
wa Wilaya ya Namtubo, Dkt. Julius Ningu leo tarehe 1 Machi, 2022 amesisitiza kuwa
ataendelea kutenda haki kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, hasa katika nyanja ya
kuendeleza utamaduni wa kutenda haki kwa wananchi.
Ameyasema
hayo alipokutana na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma
ofisini kwake alipomtembelea akiwa katika ziara yake ya kikazi ya Mahakama,
Kanda ya Songea.
“Ofisi
ya Mkuu wa Wilaya imekuwa imara katika kuendelea kutoa ushirikianao wa karibu
na Mahakama ya Wilaya hususani maeneo yote ya kumsaidia mwananchi kufikia haki
na endapo kunakuwa na jambo lolote huwa tunawasiliana kwa karibu kutatua
changamoto kwa pamoja na haishangazi kuona mihimili yote inachapa kazi bega kwa
bega,”alisema.
Akiongelea
suala la ukiukaji wa haki za binadamu, Mkuu huyo wa Wilaya alitanabaisha kuwa
hakuna ukiukwaji wa maadili kwa kiwango kikubwa katika Wilaya yake unaopelekea
uvunjivu wa amani wa kutisha.
“Katika
jamii yenye mchanganyiko wa tamaduni na desturi mbalimbali matukio ya ukiukwaji
wa haki na masuala ya kujichukulia sheria mkononi halikwepeki, kwa uchache
yanapojitokeza huchukua hatua stahiki mara moja ili kuthibiti hali hiyo,”alisema.
Aidha,
Dkt. Ningu alisifia Mahakama ya Tanzania kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya ya
kiuntendaji ambayo yamerejesha imani na taswila chanya kwa wananchi.
“Ni
kweli Mahakama imebadilika sana, tunaweza kusema mfumo wake ni mfumo jumuishi
wa kuwafanya wananchi waweze kuielewa Mahakama kwa sababu hapo awali ‘psychological
space’ kati ya Mahakama na wananchi. Mtazamo aliokuwa nayo mwananchi ni kwamba
ukienda mahakamani wewe ni kuhukumiwa, lakini kumbe ni kusikilizwa haki zake,”alisema.
Alibainisha
kuwa mfumo ambao Mahakama ya Tanzania inaotumia hivi sasa ni nzuri, lakini mbinu
inayotumika inabidi iboreshwe zaidi. Amesema kuwa kitu ambacho wamejaribu
kupanga katika Wilaya yake ya Namtumbo wameamua kupitia vikao vyao kuiomba
Mahakama ya Wilaya Namtumbo kuanza utekelezaji kwa kuanziasha klabu za sheria mashuleni
ili kuwajengea uwezo wanafunzi kupitia elimu hiyo waweze kujua na kupata uelewa
wa pamoja.
“Tunatafuta
namna bora ya kuwafanya wananchi waielewe Mahakama kama chombo rafiki cha
utoaji haki kwa wananchi, hii itaongeza pia kujenga imani chanya na kuepuka kuona Mahakama
kama chombo kisichokuwa karibu na mwananchi,” alisema.
Mkuu
huyo wa Wilaya alipendekeza Maafisa wa Mahakama pale inapowezekana wanaweza kutoa
elimu kwenye mikutano ya hadhara inayoandaliwa na Ofisi yake ili kutatua
changamo za ukosefu wa ufahamu wa mambo mbalimbali yanayomgusa mwananchi na
majukumu ya msingi ya Mhimili.
“Maafisa
wa Mahakama wanaweza pia kutumia matukio kama vile Mahafali ya shule za
sekondari na Msingi kuelezea wajibu na haki alizonazo mwananchi na jinsi
anavyoweza kuitumia Mahakama kupata haki hizo kwa wakati bila kucheleweshwa kwa
namna yoyote,” alisema.
Kwa
mujibu wa Dkt. Nungi, viongozi hao pia wanaweza kutumia hadhara kubwa inayokuja
mahakamani kuwaelimisha wananchi nini wanapaswa kufanya kupitia Mahakama ili
haki ionekane kutendeka wanapokuwa na mashauri mahakamani.
“Tutahakikisha
tunatumia njia mbalimbali kupitia mikusanyiko halali ya wananchi kupenyeza
elimu hata ya muda mfupi kuwajengea uwezo wananchi wazione Mahakama zetu ni
rafiki na ni chombo cha haki na wala sio sehemu ya kuhukumiwa”, alisisitiza
Mkuu huyo wa Wilaya.
Mkuu
wa Wilaya akatoa ushauri wa kutumia utaratibu wanaoutumia Shirika la Hifadhi ya
wanyapori TANAPA la kutumia njia ya uwajibikaji wa kijamii “Corporate
Responsibility” ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa elimu ya
shughuli za Mahakama.
Baada ya mazungumzo hayo, Jaji Mkuu alielekea katika Mahamaka ya Wilaya ya Namtumbo kuzungumza na watumishi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Julius Ningu Kitabu cha Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania Awamu ya pili 2021/2022 hadi 2024/2025, alipomtembelea Ofisini kwake, Leo tarehe 1 Machi 2022.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo hawapo pichani wakati wa ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Leo tarehe 1 Machi 2022.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo, Mhe. Gloria Lwomile akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo ichani) wakati wa ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama Wilayani Namtumbo
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyenyoosha mkono) akijadili jambo na Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Moladi Limited wakati wa kukagua Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo lililokatika hatua za mwisho za kukamilika kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo wakati wa ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma
Picha na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni