Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 1 Machi, 2022 ametangaza
kuanzishwa kwa kituo kipya cha Huduma kwa Mteja, ‘Call Centre’ kinachowezesha
wananchi kupiga simu masaa 24 ili kujua huduma zote zinazotolewa na Mahakama ya
Tanzania.
Habari
hizo njema zimetangazwa na Mhe. Prof. Juma alipokuwa anaongea na Mkuu wa Wilaya
ya Namtumbo, Dkt. Julius Ningu alipomtembelea ofisini kwake katika siku yake ya
pili ya ziara ya kikazi ya kimahakama, Kanda ya Songea. Amesema kuwa Kituo
hicho kimeanza kufanya kazi leo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni
ambapo mwananchi akipiga simu atajibiwa hapo hapo.
“Tunawaomba wananchi wasilalamike sana, wafikishe
malalamiko yao na sisi tutayashughulikia. Tunawaomba watusaidie kuifahamu Mahakama. Kwa mfano, hata mimi naweza pengine
siifahamu Mahakama vizuri kwa sababu sina uwezo wa kujua yanayotokea katika
Mahakama za Mwanzo zilizo mbali. Lakini mwananchi ambaye anatafuta zile huduma
atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi,” amesema.
Jaji
Mkuu pia alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa Mahakama ya Tanzania inathamini
sana mrejesho kutoka kwa wananchi kwa vile huduma ya Mahakama ni huduma ya
umma. Alisisitiza kuwa licha ya kulalamikiwa, lazima Mahakama inatakiwa kusikiliza
na kushughulikia suala linalolalamikiwa.
“Tumetoa
utaratibu wa kupokea hayo malalamiko ambao tunauita mrejesho wa huduma kwa
mteja. Fomu za mrejesho huo zipo kwenye tovuti ya Mahakama. (Fomu hizo)
zinaainisha namna ya kuzijaza ili kujua nani anayelalamikiwa, hatua
itakayowezesha uongozi wa Mahakama kujua tatizo lilipo,” Mhe. Prof. Juma
amesema.
Alitoa
mfano fomu hiyo inauliza jina la Mahakama inayolalamikiwa, ngazi ya Mahakama,
kama ni Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama Kuu. Pia fomu hiyo inauliza kama mwananchi
anakumbuka namba ya kesi yake na ni namba ngapi, nani unayemlalamikia, kama ni
Jaji, Hakimu, Karani, Mtendaji au Mlinzi maana wakati mwingine mtu anaweza kukutana
na mlinzi na asipopata huduma nzuri huondoka na picha hasi dhidi ya Mahakama
yote kuwa haitoi huduma nzuri kwa wananchi.
“Hivyo,
hizi fomu zinatusaidia sana sisi kujua lalamiko lako ni nini, (kama ni) usikilizaji
wa shauri, kuchelewa kupata nakala ya hukumu au hukumu imeahirishwa mara kwa
mara, amri ya Mahakama haitekelezwi au kuna huduma nyingine ambayo unaona wewe inakugusa
(kama) mwananchi. Sisi tunaona siyo
vizuri kwa mwananchi kuwa analalamika tu, lakini lalamiko lake halipatiwi
ufumbuzi,” amesema.
Baada
ya kuongea na Mkuu wa Wilaya, Dkt. Ningu, ambaye aliisifia Mahakama ya Tanzania
kwa kazi nzuri inayofanya kwa wananchi, Jaji Mkuu alitembelea mradi wa ujenzi
wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo ambalo litagharibu zaidi ya millioni
630 za Kitanzania. Utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 18 Februari, 2021 na
unatarajia kukamilika tarehe 16 Agosti 16, 2022.
Mtendaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Bw. Geofrey Mashafi alitoa taarifa fupi ya ujenzi
inayoonyesha kuwa hadi sasa Mkandarasi M/S Moladi Tanzania Limited ameshalipwa zaidi
ya millioni 420 za Kitanzania kwa ajili ya kazi alizotekeleza. Alisema ujenzi
wa msingi, tofali, kupiga lipu, kuezeka bati, kuweka 'ceiling board' na upigaji
rangi katika jengo kuu la Mahakama na choo cha nje umeshakamilika na kwamba uwekaji
wa milango na madirisha unaendelea.
Katika
ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu atatembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya
ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kuhitimisha ziara hiyo kwa
kutembelea Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na
Mahakama Kuu Songea. Katika maeneo yote atakayopitia, Mhe. Prof. Juma atakagua
shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na
watumishi wa kada zote.
Katika
ziara hiyo, Jaji Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu,
wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mtendaji wa
Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Bw. Leonard Magacha.
Wengine
ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe.
Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw.
Jovin Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice
Patrick na mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela
Moshi, Naibu Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda,
Bw. Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Songea, Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian
Haule, Mhasibu, Bw. Japhet Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Namtumbo. Mbali na Mkuu wa Wilaya, Dkt. Julius Ningu(wa pili kulia), wengine kushoto kwa Jaji Mkuu ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kushoto) akipokea taarifa ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kutoka kwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Bw. Geofrey Mashafi (kulia). Kutoka kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dkt. Julius Ningu.
Muonekano kwa nje wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni