Jumanne, 8 Machi 2022

WANAWAKE MAHAKAMA WAPONGEZA UONGOZI KUZINGATIA USAWA WA KIJINSIA

-Wakiri kuridhishwa na idadi ya Wanawake kwenye madaraka

Na Mary Gwera, Mahakama

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma ameupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kutambua na kuwapa nafasi Wanawake kufanya kazi katika Idara mbalimbali zilizopo ndani ya Mhimili huo hali inayoonyesha kuzingatiwa kwa haki zao.

Akizungumza leo tarehe 08.03.2022 katika hafla ya kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Mahakama kwa Wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam, Jaji Maruma ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuwa mwanamke anao uwezo na ujasiri katika kuthubutu kufanya na kuleta mabadiliko hivyo kupewa kwake nafasi ni dhahiri kunachangia katika safari ya uboreshaji wa huduma za utoaji haki kwa wananchi.

“Kwa niaba ya wanawake wa Mahakama ya Tanzania napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Jaji Mkuu na Tume ya Utumishi ya Mahakama kwa kuwezesha teuzi za nafasi mbalimbali kwa kuendelea kuzingatia misingi ya haki na usawa,” alisema Mhe. Maruma.

Mhe. Maruma alibainisha kuwa hadi kufikia leo katika siku ya wanawake Duniani, Mahakama ya Tanzania ina idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wanawake 10 ambayo ni sawa na 40% ya Majaji wote 25 wa Mahakama ya Rufani, katika ngazi ya Mahakama ya Kuu Majaji wanawake 32 ambayo ni sawa na 38% ambao Majaji 84 waliopo.

Aliongeza kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama pia chini ya uongozi wa Mhe Jaji Mkuu wa Tanzania imeendelea kuteuwa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi. Na hii imewezesha kuwa na Msajili 1 mwanamke kati ya Wasajili 3 waliopo, Naibu Wasajili wanawake 25 ambao ni sawa na 11% ya Naibu wasajili 62 waliopo.  Mahakimu wanawake Wafawidhi 15 katika Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakimu wafawidhi wa Mahakama za wilaya 58 na Mahakama za Mwanzo  zaidi ya 50%.

“Katika ajira za watumishi wa Mahakama bado misingi ya haki na usawa imeendelea kuzingatiwa katika kuajiri ambapo kwa sasa Mhimili huo una jumla ya Mahakimu Wakazi wanawake 556 sawa 50% ya Mahakimu Wakazi 1096 pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo 115 sawa na 43% ya Mahakimu 265 waliopo na katika ngazi za Utawala na kada nyingine pia Wanawake pia wapo katika idadi inayoridhisha,” alieleza Jaji huyo.

Aidha, Jaji Maruma aliongeza kwa kutoa rai kwa Watumishi wanawake wa Mahakama ya Tanzania kuwajibika katika nafasi zao ili kuendeleza azma ya Mhimili huo ya kuboresha huduma zake kwa wananchi.

Hakuna shaka kuwa katika safari ya uboreshaji wa huduma za Mahakama
imeonyesha dhahiri nafasi ya wanawake wa Mahakama inavyoendelea kuchangia katika mafanikio tunayoyaona. Ni rai yangu kwa wanawake wenzangu kupitia nafasi zetu tuendelee kutambua kusudio la Mwenyezi Mungu kutuumba wanawake na uwezo aliotupa ili tuutumie katika kuwa na ujasiri katika kuthubutu kufanya na kuleta mabadiliko,” alisema Mhe. Maruma.

Katika hatua nyingine, Mgeni huyo rasmi aligusia kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani inayosomeka “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu” ambapo ameeleza kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya Kitaifa, Mahakama ya Tanzania katika kuonyesha mchango wake katika kuleta haki na usawa kwa maendeleo endelevu kupitia kauli mbiu yake inayosema "Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Ushiriki wa wanawake katika Maboresho ya Mahakama"

Katika kaulimbiu tajwa, Mhe. Maruma amewasisitiza Wanawake kuelekeza nguvu zao katika matumizi ya TEHAMA ili azma ya Mahakama ya kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’ itimie.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Mstaafu, Mhe. Joaquine De Mello ametoa rai kwa Watumishi Wanawake wa Mahakama kusimamia nafasi yake kikamilifu ili kuchangia si tu katika kuboresha shughuli za Mahakama bali kuboresha na kutimiza malengo ya Taifa kwa ujumla.

“Kumekuwa na mashirikiano ya kimkakati kati ya Serikali yetu na Wadau wa Washirika wa Maendeleo kama vile ‘UN Global Compact’, ‘IFCUN Women’ kuhakikisha malengo endelevu 17 ya Umoja wa Mataifa yaliyoasisiwa tangu mwaka 2015 yanafikiwa na kwa ukamilifu, malengo hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa Serikali inaondosha kabisa madhila ya njaa, maradhi, umasikini, ujinga, ukosefu wa ajira, ubaguzi wa kijinsia na ukatili,” alisema Mwenyekiti huyo.

Katika Sherehe hiyo, Watumishi Wanawake kutoka ngazi zote za Mahakama za jijini Dar es Salaam wamekutana na kusherehekea kwa pamoja katika Viwanja vya Mahakama vilivyopo Mtaa wa Chimara- ‘Ocean Road’ jijini humo.

Siku hii ya Tarehe 08 mwezi Machi ilipitishwa na umoja wa mataifa mwaka 1975 kuwa siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake. Harakati za kupigania haki za wanawake zilianza mwaka 1908 wakati wanawake katika mji wa NewYork-Marekani wapatao 15,000 walipoandamana wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura.

Sehemu ya Watumishi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika maandamano maalum ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani leo tarehe 08 Machi, 2022. Maandamano hayo yaliyohusisha Watumishi wa ngazi mbalimbali na Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania yalianzia katika viwanja vya Mahakama Kuu hadi Viwanja vya Chimara ‘Ocean road’ jijini Dar es Salaam ambapo imefanyika hafla ya kusherehekea Siku ya Wanawake.

 Baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika maandamano ya kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

 Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo akizungumza na Watumishi Wanawake wa Mahakama (hawapo katika picha) waliohudhuria katika sherehe ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyojumuisha Watumishi hao kutoka mkoa wa Dar es Salaam.

Sehemu ya Wanawake wakimsikiliza Mgeni rasmi, Mhe. Maruma (hayupo katika picha).

Sehemu ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo katika picha) wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama wanawake walioshiriki katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Mstaafu, Mhe. Joaquine De Mello akizungumza na Watumishi wanawake wa Mahakama walioshiriki katika hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya sherehe hiyo, Mhe. Martha Mpaze akitoa neno la utangulizi katika shughuli hiyo.
Mgeni Rasmi, Mhe.Maruma (wa pili kulia) akikata keki maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya sherehe hiyo.
Katika picha ni sehemu ya Watumishi Wanawake wa Mahakama walioshiriki katika hafla hiyo katika Viwanja vya Chimara 'Ocean Road' jijini Dar es Salaam.


 

 



Maoni 1 :

  1. taarifa ni nzuri ila takwimu ni za wanasheria pekee wakati mwingine ni vyema awepo mtendaji au afisa utumishi mwanamke nae awasilishe taarifa za watumishi ambao sio wanasheria. Kama mwasilishaji ni mmoja basi awe na takwimu za pande zote mbili. Hii itaondoa hali ya wengine kujisika wanyonge na kuona sherehe haikua inawahusu.

    JibuFuta