Na James Kapele - Mahakama, Katavi
Watumishi wa Mahakama mkoani Katavi wamehimizwa kujiunga
na Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama
Saccos) ili kujiwekea akiba na kupata sifa za kukopeshwa mikopo ya aina
mbalimbali inayotolewa na Saccos hiyo.
Wito huo umetolewa leo tarehe 11 Aprili, 2022 na
Mjumbe wa Usimamizi wa Bodi ya Saccos hiyo, Bw. Ewald Kilawe katika kikao
kilichohusisha watumishi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi na Mahakama ya
Wilaya ya Mpanda.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Kilawe amewasihi
watumishi wote kuona fahari ya kujiunga na Chama hicho cha ushirika ambacho
kinafuata taratibu zote na sheria za nchi na hutoa mikopo yenye riba nafuu kwa
wanachama wake ili kuinua vipato vyao, kuwawezesha kiuchumi na baadaye kuwa
wajasiriamali wakubwa.
“Hii Saccos ni yetu sote kama watumishi wa Mahakama
kwa kuwa inatusaidia katika kumaliza changamoto zinazotukabili, hasa za
kifedha. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa sasa tunatoa mikopo ya aina tano
kwa wanachama ambao tayari wamekidhi vigezo,” alisema.
Ametaja aina hiyo ya mikopo kama mikopo ya
maendeleo, mikopo ya ajira mpya, mkopo wa kiwanja, dharura na hata mkopo wa
sikukuu.
Awali akifungua
kikao hicho, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi,
Mhe Fredirick Shayo alitoa rai kwa watumishi kujiunga na Saccos hiyo ili
kuepuka kuchukua mikopo katika taasisi nyingine za fedha ambazo riba zake bado
zipo juu.
Aidha ameishauri Saccos hiyo kuangalia uwezekano wa kutumia
mfumo mzuri ili kuweza kuwavutia wanachama wengi ili kuleta mafanikio zaidi ya
kuanzishwa kwa chama hicho cha ushirika.
“Zipo Saccos katika taasisi nyingine ambazo
zimefanikiwa sana, angalieni namna mnayoweza kufanya ili kuwavutia wanachama
wengi kujiunga ili Saccos yetu ifanye vizuri zaidi. Mnaweza hata kufanya vikao
vya mara kwa mara na wanatumishi hata
kupitia Video conferencing ili kuwahamasisha zaidi,” alisema Mhe. Shayo.
Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Katavi, Mhe Fredirick Shayo (aliyesimama katikati) akiongea na watumishi wakati wa
kikao hicho. Aliyeketi kushoto ni Afisa utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Katavi Bw, Ayoub Nyalobi.
Mjumbe wa usimamizi wa bodi ya chama cha ushirika
cha akiba na mikopo, Mahakama Saccos Bw, Ewald Kilawe (aliyesimaman kulia) akifafanua
jambo katika kikao hicho Katavi.
Sehemu ya watumishi waliohudhuria kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni