Jumanne, 9 Agosti 2022

CHUO CHA MAHAKAMA LUSHOTO MWAROBAINI WA MALALAMIKO MAHAKAMANI

Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto

Mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania yamechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji kazi kwa watumishi katika maeneo yote ya utoaji haki, hivyo kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko kwa Mhimili huo wa Dola kutoka kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo cha IJA na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa watumishi wa Mahakama 56 kwa ngazi ya Makatibu Muhtasi yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022 katika Chuo hicho.

“Tunaamini na tunaridhika kuwa mafunzo tunayoyatoa yameboresha sana utendaji wa kazi.  Hata wateja wa ndani wanafarijika kwa kiasi kikubwa, huduma zimeboreshwa kwa maana ya utendaji kazi kati ya sisi wenyewe, wahudumu wa kawaida, makarani au makatibu muhtasi umeboreka kutokana na mafunzo ambayo wanapata,” amesema.

Mkuu wa Chuo huyo amebainisha kuwa inafahamika kwa sasa uondoshaji wa mashauri unafanyika kwa kasi kubwa na hatua hiyo inatokana na matunda ya mafunzo ambayo wanayatoa kwa kada mbalimbali ndani ya Mahakama, ikiwemo Majaji na Mahakimu.

“Malalamiko ya watu kupotezewa haki zao mahakamani yamepungua sana. Rushwa na vitendo vyote ambavyo vilikuwa vinaichafua Mahakama, kama matumizi ya lugha mbaya, vimepungua kwa kiasi kikubwa na mahali pengine vimeisha kabisa kutokana na mafunzo ambayo tumekuwa tunayatoa tangu tulipokuwa tunatekeleza mpango mkakati wa kwanza na mradi wa uboreshaji awamu ya kwanza,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo amewaambia watumishi hao kuwa kwa muda mrefu Mahakama imekuwa kwenye uboreshaji ambao unagusa katika maeneo mengi na kubwa  ambalo linaonekana wazi ni lile linalohusu miundombinu ya majengo ambayo yameboreshwa ili kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira bora.

Mkuu wa Chuo huyo akabainisha pia kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali kwa muda mrefu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ili kuwajengea uwezo katika kutenda haki kila mmoja kwa nafasi yake na kuna matokeo chanya ambayo yanaonekana kutokana  na hatua hiyo.

“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.

Amewakumbusha washiriki hao wa mafunzo kuwa wao ni watumishi wa Mahakama ambao jamii inawachukulia kama Mahakimu ambao kila mmoja hutoa haki kwa namna yake, ikiwemo kutoa taarifa sahihi kwa mteja anayetaka kujua kesi yake inakuja lini, ambayo pia ni haki ya mtu kuifahamu.

“Tunawaomba na nyinyi mkatende haki kwa nafasi yenu ya Katibu Muhtasi. Ukiharibu wewe hakuna mtu anayejua kuwa ni wewe, yeye anajua ni Mahakama. (Mtu huyo atatoka) mahakamani akiwa amekasirika na (kulalamika) majengo mazuri lakini huduma ni mbaya. Hivyo, nyinyi ni kioo cha Mahakama,” amesisitiza.

Mhe. Dkt. Kihwelo anamini kuna changamoto ambazo watumishi hukumbana nazo wanapotekeleza majukumu yao na ndiyo maana mafunzo kama hayo hutolewa ili kuwasaidia namna ya kuzikabili. Akawakumbusha pia kuwa wao ni watumishi wa umma na utumishi wa umma mwisho wa siku ni kuwasaidia wananachi.

Mkuu wa Chuo huyo hakuficha furaha yake kwa jinsi Kurugenzi ya Mafunzo inayoongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Bi Patricia Ngungulu ilivyopata washiriki kwenye mafunzo hayo ambao wametoka katika Mahakama mbalimbali nchini, hatua ambayo inaondoa dhana kwamba IJA ni ya watu wa upande wa Majaji na Mahakimu tu.

“Chuo chetu ni cha kipekee kabisa, kuna vyuo vingine vya Mahakama vinatoa mafunzo kwa Majaji na Mahakimu tu. Lakini sisi tuna bahati kwa kweli, tunatoa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu, wadau na watumishi wengine wote wa Mahakama na ndiyo hilo lingine ambalo tunalifanya,” alisema.

Akitoa neno la kumkaribisha Mkuu wa Chuo ili kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali.

“Hatua hii ni katika utekelezaji wa azma ya Mahakama kuhakikisha watumishi wake wanajengewa uwezo kwa kuwaendeleza kwenye kada zao na kuwa na (ujuzi mpana kwenye maeneo yao ya kazi. Jitihada) hii imeanza na itaendelea taratibu kadri bejeti itakavyokuwa ikiruhusu,” amesema.

Bi. Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za pembezoni katika Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, huku wengine sita wakiwa ni waajiriwa wapya.

Amesema watumishi hao wameitwa ili wakumbushwe upya majukumu yao juu ya shughuli za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi kwa ujumla, uzalendo na protokali, mipango ya Mahakama na uboreshaji, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.

Washiriki pia watapitishwa kwenye maeneo mbalimbali kuhusu utoaji wa huduma kwa ujumla kwa kuzingatia mkataba wa huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na ushauri, usalama serikalini na upekuzi, kudhibiti msongo wa mawazo pamoja na mambo mengine.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akizungumza kwa ufupi kumkaribisha Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kufungua mafunzo hayo.
Mratibu wa Mafunzo Mahakama, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiwasili kwenye ukumbi.


Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika ukumbi wa mafunzo. Kushoto ni Hakimu  Mkazi Mfawidhi katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka na kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi Patricia Ngungulu (kulia) akifuatilia jambo katika mafunzo yanayotolewa na wawezeshaji mbalimbali akiwemo Mkufunzi Msaidizi Masomo ya Uhazili kutoka Utumishi, Bi Juliana Mwalusamba (katikati). Kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama, Bw. Rajabu Singana.

Sehemu ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo (picha mbili juu na moja chini) ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.

Sehemu nyingine ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo (juu na chini) ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi kutoka katika Mahakama ya Wilaya Lushoto.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo (picha mbili juu na picha tatu chini).



Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa secretarieti ya mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.
Mkufunzi Msaidizi Masomo ya Uhazili kutoka Utumishi, Bi Juliana Mwalusamba akiwasilisha mada kwenye mafunzo ambayo yamewaleta pamoja Makatibu Muhtasi 56 kutoka Mahakama mbalimbali nchini.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni