Jumatatu, 8 Agosti 2022

WATUMISHI WAPYA WA MAHAKAMA WATAKIWA KUTEKELEZA KWA VITENDO MAFUNZO WALIYOPATA

Na Mary Gwera, Mahakama

Watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania walioajiriwa hivi karibuni wametakiwa kuyaishi kwa vitendo maelekezo ya Watoa mada mbalimbali yaliyotolewa katika Mafunzo elekezi yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto ili kufanikisha dira ya Mahakama ya kutoa haki kwa wote na kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kufunga Mafunzo hayo kwa nyakati tofauti tarehe 06 na 07 Agosti, 2022, Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick alisema kuwa, nia na malengo ya Mahakama kufanya mafunzo hayo ni kuendelea na kuwekeza katika kuwajengea uwezo watumishi wake wote sio tu kwenye maeneo ya utaalamu kwa kada na utaalamu wao, bali hata kwa kuwajengea ujuzi (yaani soft skills) ili kuwa na timu nzuri za utendaji kazi zenye sifa na uwezo unaotakiwa.

“Napenda mtambue kuwa, mafunzo mliyoyapata, endapo mtayazingatia kwa ufasaha, yatawatambulisha vema kwa wananchi kwa kuwa ninaamini mmeandaliwa vizuri na mmejengewa misingi ya utendaji wa kazi mzuri na mtashiriki na kuchangia katika kutekeleza malengo yaliyopo kwenye mpango mkakati na vipaumbele vya Mahakama,” alisema Bi. Beatrice.

Amesema, ana imani kuwa kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wawezeshaji wenye maarifa na weledi mkubwa katika maeneo mahsusi, yamewapa maarifa ambayo yatawafanya kuwa watumishi wema wenye haiba, tabia, mienendo na maadili ya kimahakama ambayo yatawasaidia katika kudhibiti maisha binafsi yasiweze kuathiri kazi zao au Maisha ya kazini yasiweze kuathiri maisha ya kawaida.

Aliongeza kuwa, kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wanayalalamikia ni kama vile ucheleweshwaji wa huduma, uwepo wa rushwa, huduma kuwa duni, kauli zisizoridhisha, majivuno, matumizi mabaya ya vyeo. Hivyo amewataka kuyaondoa kwa kusaidiana na watumishi wenzao watakaowakuta vituoni walikopangiwa kusaidia kurejesha imani na mtazamo chanya kwa jamii.

Mkurugenzi huyo aliwahakikishia Watumishi hao kuwa, Uongozi wa Mahakama utawapa ushirikiano ili kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira mazuri kwa kuendeleza uboreshaji wa miundombinu na vitendea kazi ikiwemo mazingira ya kufanya kazi pamoja na maslahi.

“Tumesikia mapendekezo mliyoyatoa ya Mahakama kuhakikisha kuwa watumishi wengine wanapata mafunzo kama haya ili Mahakama nzima iwe na mtazamo mmoja wa kiutendaji. Naomba niwafahamishe kuwa ni matarajio yangu kuwa, wakati Mahakama inaendelea kuwekeza kwetu kwa kiwango kikubwa, wajibu wetu kama watumishi uwe ni kuendelea kujifunza ili tuzifahamu mbinu mpya zaidi zinazoweza kuleta mabadiliko kiutendaji ili tuwahudumie na kuwajibika vyema kwa wananchi,” alisisitiza.

Wakitoa neno la Shukrani, Wawakilishi wa Watumishi hao wameishukuru Mahakama ya Tanzania pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wamekiri kufaidika nayo kufuatia mada mbalimbali walizofundishwa na kuahidi kuwa watatekeleza kwa vitendo yote waliyofunzwa.

Wameahidi kuwajibika kwa wateja wa ndani na nje kwa kuondosha au kupunguza malalamiko baina ya wafanyakazi wa ndani ya Taasisi na wananchi kwa ujumla ili kuleta matokeo chanya na kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati.

Aidha, Watumishi hao wamependekeza kuwa, Mafunzo yafanyike mara kwa mara ili kujikumbusha na kuongeza ufanisi kazini, mada ya Saikolojia iwe endelevu kwa watumishi wote kwakuwa inachukua nafasi kubwa katika utendaji kazi wa kila siku, kufanyika vikao baina wa Viongozi na watumishi ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ndani ya Taasisi.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na yalihusisha Watumishi wapya wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja, Makatibu Mahsusi na Madereva.

Sehemu ya Watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania walioajiriwa hivi wakimsikiliza mgeni rasmi Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bi. Beatrice Patrick (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa hotuba ya kufunga Mafunzo elekezi kwa Watumishi hao yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama kuanzia tarehe 01 Agosti, 2022 hadi tarehe 07 Agosti, 2022.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akizungumza na Watumishi wapya wa Mahakama alipokuwa akifunga rasmi Mafunzo Elekezi yaliyotolewa kwa Watumishi hao katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto.


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni