Na Tiganya Vincent-Mahakama –Dodoma
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ametembelea miradi
miwili ya Mahakama ya Tanzania Jijini Dodoma kukagua maendeleo ya utekelezaji
wake.
Mhe.
Siyani ameongozana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na viongozi
wengine wa Mahakama ambapo alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya
Mahakama Tanzania ambao ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Mradi wa
pili ambao umetembelewa na Jaji Kiongozi ni ujenzi wa nyumba za Majaji ambapo
nyumba za Majaji wa Mahakama ya Rufaa zinatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu
na zile za Majaji wa Mahakama Kuu zitakamilika mapema mwakani.
Akizungumza
mara baada ya kutembelea miradi yote, Mhe. Siyani ameelezea kufurahishwa kwake
na ujenzi wa ofisi mbalimbali zikiwemo za Majaji ambazo zitawapa mazingira
mazuri ya kutekeleza majukumu yao na nyumba za Majaji zinatoa mazingira mazuri
ya kuishi.
Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania amesema Mkandarasi anayejenga Makao Makuu ya Mahakama
ndiyo anayejenga nyumba za Majaji na kuongeza kuwa kasi yake inaridhisha na
ataweza kumaliza kwa muda waliokubaliana.
Amesema
lengo ni kutaka kuhakikisha kuwa watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania ambao
wako Dar es salaam wanahamia Dodoma kama walivyoahidi.
Prof. Ole
Gabriel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa uwezeshaji ambao umesaidia kuboresha miundombinu ya majengo na
kujenga jengo la kisasa la Mahakama ya Tanzania Jijini Dodoma.
Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kushoto) akitoa mchango wake wakati wa ziara ya Jaji Kiongozi na Viongozi wengine kutembelea mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na nyumba za Majaji jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika na Jaji Kiongozi Mustapher Siyani wakati walikuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akimwonyesha kitu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe.Dkt. Gerald Ndika na Jaji Kiongozi Mustapher Siyani wakati walikuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
(Picha na
Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni