Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 6 Agosti, 2022 amewaongoza Majaji wa Mahakama ya Rufani na watumishi wote wa Mahakama hiyo kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, tukio ambalo limeacha historia ya kipekee tangu kuanzishwa kwa hifadhi hiyo 1964.
Msafara wa Jaji Mkuu ulianza safari kutoka Hoteli ya Nashera mjini Morogoro majira ya saa moja na nusu hivi kuelekea Mikumi mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, safari ambayo ilichukua takribani saa moja.
Ujumbe huo wa Mahakama uliwasili katika lango la hifadhi ya Mikumi takribani saa tatu kasorobo na kupokelewa na Mhifadhi Mkuu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Ignas Gara ambaye alimpeleka mgeni wake na maafisa wengine wa Mahakama hadi sehemu iliyokuwa imeandaliwa kwa mapumziko mafupi.
Msafara wa Jaji Mkuu ulianza utalii majira ya saa tatu hivi na kuongozwa na Mhifadhi Mkuu ambaye alikuwa wakati wote yupo bega kwa bega kuelekeza maeneo mbalimbali yenye vivutio pamoja na Wanyama mbalimbali katika hifadhi hiyo ambayo ni maarufu sana hapa nchini Tanzania.
Kwa takribani masaa matatu msafara wa Mkuu wa Muhimili wa Mahakama ulitembelea maeneo kadhaa ndani ya hifadhi na kufanikiwa kujionea Wanyama wengi wa kuvutia, wakiwemo Simba, Twiga, Nyati, Tembo, Nyumbu, Swala, Pundamilia, Viboko na Mamba.
Mtembeza Watalii mmoja aliueleza msafara huo kuwa Simba wawili walioonekana walikuwa wa kike na walikuwa wametoka kuwinda Nyati na maafisa hao waliweza kujionea jinsi walivyokuwa wanamshambulia mnyama huyo ambaye alikuwa tayari alishakufa ili kujipatia chakula.
Msafara wa Mhe. Prof. Juma pia ulipata bahati ya kutembelea bwawa la Viboko ambao walikuwa wamejianika juani na kupata maelezo ya kina jinsi viumbe hao wanavyoishi na tabia walizonazo. Inasadikika Kiboko ndiye mnyama hatari zaidi anayeongoza kuua binadamu. Jaji Mkuu na ujumbe wake ulimaliza shughuli hiyo ya utalii majira ya saa saba mchana na kurejea hotelini kwa mapumziko.
Hifadhi ya Taifa Mikumi, ni moja ya hifadhi kubwa na mashuhuri nchini. Eneo kuu na muhimu katika hifadhi hii ni uwanda wa mafuriko pamoja na safu za milima ambazo zinapakana na hifadhi hii. Mbuga za wazi ndizo zinashamiri katika uwanda wa mafuriko na kuishia katika misitu ya miombo inayofunika mabonde yaliyo chini ya hifadhi.
Katika Hifadhi ya Mikumi wanapatikana Simba, Tembo, Nyati na Chui kati ya wanyama watano maarufu zaidi duniani wajulikanao kama the big five. Mikumi wanapatikana mbwa mwitu pia ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka. Ni hifadhi rahisi kifikika kwa njia zote za usafiri. Ikiwa na ukubwa la kilomita za mraba 3,230, Mikumi ni ya tano kwa ukubwa nyuma ya hifadhi nyingine za Taifa ambazo ni Serengeti, Ruaha, Katavi na Mkomazi.
Simba wawili majike yakiwa yamejipumzisha baada ya mawindo.
Simba mmoja jike akielekea kwenye kitoweo walichokuwa wamewinda huku mwingine akiwa amejipumzisha.
Simba mmoja jike akiwa kwenye kitoweo.
Simba mmoja jike akijipatia kitoweo.
Twiga akiwa kwenye ubora wake.
Mamba akiwa pembezoni mwa bwawa la maji.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipata picha ya kumbukumbu mbele ya Mamba huku watumishi wengine wa Mahakama wakishuhudia.
Kundi ya Viboko ndani ya bwawa.
Kundi la Nyumbu.
Kundi la Pundamilia.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na askali wa Wanyamapori wakiongozwa na Mhifadhi Mkuu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Ignas Gara (wa pili kushoto).
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Ignas Gara akiagana na mgeni wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma baada ya kutalii kwenye hifadhi yake.
Msafara wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma ukitoka kwenye eneo la hifadhi kuelekea Morogoro mjini.




















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni