Na Tiganya Vincent-Mahakama
Mahakama ya Tanzania imeishukuru Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kuwapa fedha za kununua magari manne kwa ajili ya usafiri kwa watumishi wake.
Pongezi hizo zimetolewa jana tarehe 5 Agosti, 2022 jijini
Dar es salaam na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabliel wakati akipokea magari hayo kutoka kwa Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi
wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Chale.
Akipokea magari hayo, Mtendaji Mkuu alisema yatapelekwa katika Kanda nne za Mahakama
ambazo ni Morogoro, Shinyanga, Mwanza na Musoma.
Prof. Ole Gabriel alisema bado kuna baadhi ya Kanda
zenye changamoto ya usafiri lakini watumishi ambao bado hawajapata magari
wasivunjike moyo kwani ushirikiano wa Serikali na Mahakama ni mzuri na yapo
magari mengine yatakayonunuliwa.
Alisema jitihada za Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Profesa Ibrahim Juma ni kuona Watanzania wanapata haki kwa wakati, hivyo kama
watumishi wakiwa na usafiri wa uhakika itasaidia kutekeleza azima hiyo.
Prof Ole Gabriel aliwataka watumishi na madereva
watakaokabidhiwa magari hayo kuyatunza ili yaweze kufanya kazi kwa muda mrefu
na kusaidia katika uendelezaji wa mnyororo wa utoaji haki kwa wakati.
Kwa upande wake, mmoja wa madereva hao watakaoendesha
magari hayo, Bw. Juma Chikoti alisema usafiri huo utaongeza morali na tija kwa
watumishi kwa kuwa watafika kwa wakati kazini huku akiahidi kulitunza.
Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Chale akitoa maelezo mafupi wakati wa kukabidhi mabasi wanne kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabliel.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni