Ijumaa, 9 Septemba 2022

JAJI MFAWIDHI KANDA YA MBEYA AFANYA ZIARA SONGWE

Na Mohamed Kimungu- Mahakama, Songwe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Songwe na kuwapongeza watumishi kwa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao licha ya kuwa wapo wachache.

Katika ziara yake, Mhe. Ebrahim alianza kwa Mahakama Mwanzo Kamasamba iiliyopo katika Wilaya ya Momba na kushuhudia watumishi waliopo jnisi wanavyofanya kazi kwa kujituma pamoja na uchache wao.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alitembelea Mahakama ya Mwanzo Ndalambo na kuahidi kusitisha huduma kwa muda katika Mahakama hiyo kutokana na kutokuwepo kwa mashauri kwa kipindi cha Januari hadi Septemba na kumshauri Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Songwe, Bw Sostenes Mayoka kuwabadilishia vituo watumishi waliopo katika Mahakama hiyo.

Mhe Ebrahim alihitimisha ziara yake ya kikazi kwa kutembelea mradi wa ujenzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe ambao umekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kuanzia tarehe 19 Agosti, 2022. Aliwataka watumishi katika Mahakama kulitunza jengo hilo ambalo limetumia fedha za Serikali.

Alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof Elisante Ole Gabriel kwa uboreshaji mkubwa ya majengo ya Mahakama unaoendelea nchi nzima ambao unapelekea mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa watumishi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (aliyekaa) akijiandaa kusaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbozi, Mhe. Nemes Chami. 

Viongozi wa Mahakama wakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu (kulia) wakiwa katika ofisi ya Mahakama hiyo ya Songwe.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim akiwa katika picha ya pamoja viongozi wa Mahakama Mbeya na Songwe katika lango kuu la kuingilia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni