Jumatano, 7 Septemba 2022

JAJI NGWEMBE ALONGA NA WADAU WA HAKI MOROGORO; WAAHIDI USHIRIKIANO

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka wadau wa haki katika Kanda hiyo kutosita kuelezea changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao ili jukumu la utoaji haki liweze kutekelezeka ipasavyo.

Akizungumza na Wadau hao jana tarehe 06 Septemba, 2022 alipokutana nao katika kikao kilichoitwa 'Breakfast Meeting', Mhe. Ngwembe alisema kuwa, lengo la kikao hicho ni kufahamishana na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa usikilizaji wa mashauri.

“Ni wakati sasa wadau kuwa wawazi kushauri na kuelezea changamoto mnazokutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yenu, hata zinapotokea msisite kuwasiliana na Mahakama ili kikao cha namna hii kiitishwe na changamoto husika ipatiwe ufumbuzi,” alisema Jaji Ngwembe.

Jaji Ngwembe alisema kila mdau wa haki afanye kazi yake kwa usahihi ili kesi zilizopo mahakamani ziweze kufikia katika uamuzi mzuri kwani wakati mwingine kesi haifikii katika hitimisho linalostahili kutokana na kuwa na ushahidi hafifu. “Ni vibaya sana kumuachia mtu ambaye ametenda kosa au kumfunga mtu ambaye hajatenda kosa hivyo wote kwa Pamoja tumekubaliana kwamba kila mmoja afanye kazi yake kwa usahihi” alisisitiza.

Akichangia hoja hiyo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Rash Meela alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazoikabili Jeshi hilo likiwemo suala la Ushahidi litafikia ukomo hivi karibuni na tayari Jeshi la Polisi mkoani humo limeanza kutoa mafunzo kwa Askari wake ili kuwajengea uwezo mzuri wa namna ya kukusanya Ushahidi pia wamekuwa wakishirikiana na Ofisi ya Waendesha Mashtaka wa Serikali.

Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni uwepo wa watu magerezani ambao tayari wameshamaliza kutumikia vifungo vyao ambapo idadi kubwa ya watu hao ni wahamiaji haramu ambao bado wapo magerezani wakisubiri kukamilika kwa taratibu za kurudishwa katika nchi zao. Akitoa takwimu ya watu hao Kamishna Msaidizi wa Magereza Mkoa wa Morogoro, (ACP) Dkt. Wilson Rugamba alisema kuwa mpaka sasa kuna wahamiaji haramu 256 katika magereza ya Morogoro ambao tayari wameshamaliza kutumikia adhabu yao.

Wakichangia ajenda hiyo wajumbe wa kikao hicho, walipendekeza kuwa, ili kuondoa mrundikano magerezani na kuipunguzia gharama Magereza kuwe na sehemu ya kuwaweka wahamiaji haramu hao ambao wameshamaliza kutumikia adhabu zao Gerezani wakati wakisubiria taratibu za kurudishwa nchini mwao na sehemu hiyo ihudumiwe na Ubalozi wa Nchi husika.

Kikao hicho hicho kilichohitimishwa kwa makubaliano ya kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha dhima ya Mahakama ya kutoa Haki kwa Wakati. Wajumbe wa kikao hiko walitoka katika ofisi za Uhamiaji, Magereza, Polisi, Waendesha Mashtaka wa Serikali, Meneja TTCL, Pamoja na viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Haki wa Mkoa wa Morogoro walioshiriki katika kikao kilichoitwa 'Breakfast Meeting' kilichofanyika jana tarehe 06 Septemba, 2022 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika Kanda hiyo. 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni