·Mada
yake ya kiwango cha lami yasisimua
·Asema
Tanzania hakuna kurudi nyuma matumizi ya TEHAMA, Mahakama Inayotembea
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashauri Majaji na Mahakimu katika nchi za
Jumuia ya Madola kutumia changamoto wanazokabiliana nazo kama fursa
wanapotekeleza majukumu ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma alitoa
wito huo jijini Accra nchini Ghana alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Mahakama
Zinazotembea na Mahakama Mtandao “Mobile and Virtual Courts” katika Mkutano
Mkuu wa Umoja wa Mahakimu na Majaji katika Jumuiya ya Madola (Commonwealth
Magistrates and Judges Association-CMJA), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Naibu Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi.
Alieleza kuwa nchi yake
(Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ni nchi kubwa ambayo ina kilometa za mraba
zaidi ya laki tisa na watu zaidi ya milioni sitini, huku akiwatania washiriki
kuwa Tanzania ni kubwa kuliko baadhi ya nchi za Jumuia ya Madola zikichanganywa
na kubainisha, hata hivyo, kuwa ukubwa wa changamoto unapaswa uendane na ukubwa
wa jitihada za kuzitatua.
“Tanzania imefanikiwa
kutumia changamoto zake kubwa kama fursa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za
Mahakama kwa jamii kubwa zaidi. Somo kubwa hapa ni kwamba, tunapokuwa na
changamoto nyingi na kubwa, jitihada zetu za kuzitatua nazo zinatakiwa kuwa
kubwa na siyo kinyume chake,” alisema kwenye Wasilisho lake la “kiwango cha
lami”.
Jaji Mkuu aliieleza hadhira
yake kuwa Mahakama ya Tanzania inatumia dhana ya Mpango Mkakati kama nyenzo
muhimu ya kushirikiana na Serikali pamoja na kubainisha mahitaji halisi ya
Mahakama. Alisema Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania umeiwezesha taasisi
hiyo kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zake yenyewe ikiwemo kupunguza
mlundikano wa mashauri.
Kwa mujibu wa Mhe. Prof.
Juma, mmoja wa wataalam nguli wa utawala na mpango mkakati wa karne ya 20, Peter
Drucker huenda asingeamini kuwa Mahakama zingekuwa vinara wa taaluma ya Mpango Mkakati.
Akabainisha, hata hivyo, kuwa Wahenga walisema, kushindwa kupanga ni kupanga
kushindwa.
“Ni wazi kabisa kwamba
Mahakama ya Tanzania haipangi kushindwa! Somo muhimu hapa ni kwamba siku zote
usipopanga utapangiwa na kwamba usipopanga mapema, hutajua tofauti ya
unachohitaji na unachokitaka,” alisema.
Jaji Mkuu aliwaeleza
washiriki wa Mkutano huo waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuwa Mahakama
Inayotembea ni nyenzo ya kulinda haki za jamii za pembezoni na kwa kupitia
Mahamaka hiyo jamii zilizo pembezoni zimejengewa uwezo wa kulinda haki zao.
Alitanabaisha kuwa katika
maeneo magumu kufikika na ambayo hapo awali hayakuwa na huduma za Mahakama
kabisa, kuliibuka Miunguwatu ambao waliamini hawashikiki na kwamba mkono wa
sheria usingeweza kuwafikia.
“Tunachojifunza hapa ni
kwamba kuna hali fulani ya kiusalama na kujiamini inajitokeza pale jamii za
pembezoni zinapokuwa na huduma za Mahakama,” alisema.
Katika Wasilisho lake,
Jaji Mkuu aliileza hadhira ya Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola kuwa
Tanzania ilijifunza kuhusu Mahakama Zinazotembea kutoka nchini Guatemala na
ikaufanyia uboreshaji mpango huo ili uendane na mahitaji yake.
Mhe. Prof. Juma hakuweza
kuficha furaha yake pale alipoieleza hadhira hiyo kwamba Tanzania ina mpango wa
kupanua wigo na kuwa na Mahakama Inayotembea katika ngazi ya Mahakama ya Wilaya
na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Sote tunapata somo
kwamba kujifunza kutoka kwa wenzetu ni jambo jema. Kila mmoja ni mwalimu wa
mwenzake kwa lile analojua,” alisema.
Jaji Mkuu alikubaliana na
watoa mada wenzake kwamba “wakati tuliousubiri ndiyo sasa”. Alitanabaisha
kwamba, ijapokuwa Mahakama mtandao zilitumika zaidi wakati wa Janga la Korona,
hakuna uwezekano wa kurudi nyuma katika matumizi ya TEHAMA.
Mhe. Prof. Juma anaamini
kuwa baada ya muda mfupi Mahakama zake zote nchini Tanzania zitakuwa
zimeunganishwa na mtandao ili kurahisisha ufunguaji wa kesi na shughuli
nyingine.
Alisisitiza kwamba kasi
ya mtandao ni muhimu pia kuongezeka kwani wale wasio tayari kwa mabadiliko
hutumia matatizo ya mtandao kama kisingizio cha kutokusonga mbele. Kwa mujibu
wa Jaji Mkuu, watu wa aina hii hawachelewi kusema “Si tulisema? Mambo haya ya
Mtandao hayafanyi kazi!”
“Hapa tunajifunza kwamba
siku zote katika safari ya mabadiliko, kuna wanaotamani kurudi nyuma na kufanya
vitu kwa mazoea. Kiongozi anapoonyesha kurudi nyuma hakupo, sote tunasonga
mbele kuifikia nchi ya ahadi! “alisema.
Mkutano huo ambao
hufanyika kila baada ya miaka mitatu ulihudhuriwa na Majaji Wakuu 25 na wajumbe
350 (Mahakimu na Majaji) kutoka nchi mbalimbali za Jumuia ya Madola ulimalizika
jana tarehe 9 Septemba, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni