Jumatatu, 12 Septemba 2022

JAJI WA MAHAKAMA KUU MBEYA AWAPIGA MSASA MAHAKIMU

Na Mohamed Kimungu- Mahakama, Songwe

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. David Ngunyale amewasihi Mahakimu kutunza maadili, afya na kuipenda kazi yao na kuwa mfano bora wa kuigwa kwa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na uandilifu.

Mhe Ngunyale alitoa rai hiyo alipokuwa akiwapatia mafunzo ya siku moja Mahakimu wa ngazi mbalimbali yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Songwe, kuwajengea uwezo ili kuweza kumudu utekelezaji wa majukumu yao.

Kadhalika, Jaji huyo aliwashauri Mahakimu hao, pamoja na mambo mengine, kushiriki katika shughuli zingine za kujiongezea kipato ili kuepuka uwezekano wa kujihusisha na vitendo vya uvunjaji wa maadili ikiwemo rushwa.

Mafunzo hayo yalitolewa kupitia Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT), Tawi la Mkoa wa Songwe, mada ikiwa ni kanuni za maadili kwa maafisa wa Mahakama (Code of Conduct for Judicial officers).

Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. David Ngunyale (katikati). Wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube (kulia) na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Momba, Mhe. Timothy Lyon (kushoto).
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ileje, Mhe. Shughuli Mwambashi, ambaye pia ni Katibu wa JMAT Mkoa wa Songwe (aliyesimama) akieleza jambo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. David Ngunyale (katikati waliokaa) pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mkoa wa Songwe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni