Jumatatu, 12 Septemba 2022

MAHAKAMA YA TANZANIA YAUPIGA MWINGI MKUTANO WA MAJAJI JUMUIYA YA MADOLA ACCRA

•Jaji Ilvin Mugeta achaguliwa kuongoza Afrika Mashariki, Kati na Kusini

•Jaji Mambi atamba kwa umahiri wa TEHAMA

Na Faustine Kapama-Mahakama

Washiriki kutoka Tanzania katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola (CMJA) uliofanyika jijini Accra nchini Ghana hivi karibuni wamerudi salama nchini huku wakiwa na nyuso za bashasha baada ya “kuupiga mwingi” katika nyanja mbalimbali, ikiwemo Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta kuchaguliwa kuiongoza Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Katika uchaguzi uliofanyika wakati wa Mkutano huo, Mhe. Mugeta aliibuka kidedea kama Makamu Mwenyekiti wa Kanda hiyo baada ya ‘kumgalagaza’ vikali Jaji mwenzake kutoka Mahakama ya Rufani na kumshinda kwa kura nyingi.

Mhe. Mugeta aliwaeleza wajumbe wa Mkutano huo kiu yake ambayo ni kuona Bendera ya Tanzania inapeperushwa katika medani za Kimataifa. “Nimeshakuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, kiu yangu siku zote imekuwa kuiona Tanzania iking’ara zaidi kimataifa,” alieleza.

Mhe. Mugeta anaamini kuwa Tanzania ina mambo mengi mazuri ya kuigwa na nchi zingine za Afrika. “Mahakama ya Tanzania inaheshimiwa sana kimataifa. Tumeweza kuwa karibu na wananchi tunaowahudumia huku watumishi wengi wa Mahakama wakiwa na maadili na taaluma ya kutosha,” Jaji Mfawidhi huyo alisema kwa sauti ya kujiamini.

Alipoulizwa ni mambo gani anataka kuwafanyia wapiga kura wake ambao ni Majaji na Mahakimu kutoka nchi zote za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, Mhe. Mugeta alitumia mfano wa Mwenge wa Uhuru na kusema, “Watanzania tunaijua vizuri dhana ya kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro. Umulike nje ya mipaka yetu, kuleta haki na matumanini pasipo na matumaini.”

Jaji Mugeta anaamini kuwa kuchaguliwa kwake kuziongoza nchi zaidi ya 20 ni fursa kwa Tanzania kuangaza na kuleta haki kwa vitendo. Kadhalika, anaamini kuwa wajibu wake huo mpya hautaathiri utendaji kazi wake kama Jaji. “Nafasi hii siyo kazi ya kila siku. Tutakuwa na vikao mara chache na mambo mengine tutafanya kwa njia ya mtandao. Nitaendelea na kazi zangu vizuri,” aliwahakikishia wajumbe wa Mkutano huo.

Uwekezaji mkubwa wa Mahakama ya Tanzania uliweza pia kuchomoza katika Mkutano huo uliowaleta pamoja Majaji Wakuu 25 na wajumbe 350 (Mahakimu na Majaji) kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola. Hatua hiyo ilidhihirishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi ambaye alitamba kwa umahiri wake wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) alipopangiwa kuratibu mawasilisho ya mada za Utatuzi Mbadala wa Migogoro “Alternative Dispute Resolution.”

Mhe. Mambi, ambaye ni Mwandishi wa Kitabu cha Sheria za TEHAMA “The ICT Law Book” na mmoja wa Mwanazuoni Nguli katika eneo hilo, alikonga nyoyo za wajumbe wa Mkutano huo na kupokea pongezi nyingi kwa kurahisisha kazi yake ya uratibu kupitia TEHAMA.

Naye Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu cha Tanzania (Judges’ and Magistrates’ Association of Tanzania-JMAT), Mhe John Kahyoza, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, aliwapongeza maafisa wa Mahakama wenzake kwa mwamko wao kuhudhuria mikutano ya kimataifa.  Aliongeza kuwa kadri siku zinavyokwenda, Watanzania wanapata hamasa ya kwenda kujifunza kwa wenzao kutoka nchi zingine.

Katika Mkutano huo wa kimataifa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma alitoa mada ya kusisimua kuhusu Mahakama Zinazotembea na Mahakama Mtandao. Katika wasilisho lake la kiwango cha lami, Mhe. Prof. Juma ‘alishusha nondo’ tano muhimu, ikiwemo kwa Majaji na Mahakimu kutoka nchi za Jumuiya ya Madola kugeuza kuwa fursa changamoto wanazokabiliana nazo wanapotekeleza majukumu ya utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mkuu aliieleza hadhira yake kuwa Mahakama ya Tanzania inatumia dhana ya Mpango Mkakati kama nyenzo muhimu ya kushirikiana na Serikali pamoja na kubainisha mahitaji halisi ya Mahakama. Alisema Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania umeiwezesha taasisi hiyo kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zake yenyewe ikiwemo kupunguza mlundikano wa mashauri.

Mhe. Prof. Juma aliwaeleza washiriki wa Mkutano huo kuwa Mahakama Inayotembea ni nyenzo ya kulinda haki za jamii za pembezoni na kwa kupitia Mahamaka hiyo jamii zilizo pembezoni zimejengewa uwezo wa kulinda haki zao.

Kadhalika, Jaji Mkuu alitanabaisha kuwa ijapokuwa Mahakama Mtandao zilitumika zaidi wakati wa Janga la Korona, hakuna uwezekano kwa Mahakama ya Tanzania kurudi nyuma katika matumizi ya TEHAMA. Mhe. Prof. Juma anaamini kuwa baada ya muda mfupi Mahakama zake zote nchini Tanzania zitakuwa zimeunganishwa na mtandao ili kurahisisha ufunguaji wa kesi na shughuli nyingine.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma  akihutubia katika moja ya mikutano aliyowahi kuhudhuria
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta akisisitiza jambo.

Huyu ndiye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi,  Mwanazuoni Nguli katika eneo la TEHAMA.

Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu cha Tanzania (Judges’ and Magistrates’ Association of Tanzania-JMAT), Mhe John Kahyoza, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, akieleza jambo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni