Alhamisi, 15 Septemba 2022

MAJAJI WAPYA WATEMBELEA MAHAKAMA KUU TANGA

Na. Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto

Majaji wapya walioteuliwa hivi karibuni juzi wametembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo ubunifu uliofanyika unaochochea kwa haraka utoaji wa huduma za haki kwa wananchi, hatua iliyopelekea Mahakama hiyo kuwa ya mfano katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hapa nchini.

Katika ziara yao fupi, Majaji hao walioongozana na wenzao kutoka Mahakama Kuu Zanzibar walipokelewa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakamu Kuu katika Kanda, Mhe. Dkt. John Ubena ambaye aliwaeleza kwa kifupi jinsi TEHAMA inayorahisisha shighuli za kimahakama katika Mahakama hiyo.

Jaji Ubena alisema kuwa kupitia TEHAMA, Mahakama hiyo imeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mrundikano wa mashauri sambamba na kuwa na utaratibu mzuri na salama wa mgawanyo, uhifadhi na utafutaji wa majalada kwa wakati, jambo ambalo limepunguza kama sio kumaliza kabisa malalamiko toka kwa wadaawa.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Beda Nyaki aliwapitisha Majaji hao katika baadhi ya mifumo na kuonesha jinsi inavyofanya kazi ukiwemo mfumo wa kusajili mashauri “Judicial Statistical Dashboard System - JSDS 2” katika hatua zote, kuanzia kupokelewa na kufunguliwa jalada mpaka kutolewa uamuzi.

Aliongeza kuwa mfumo huo unafanya kazi masaa 24 kwa wiki, hivyo kuwarahisishia wadaawa kuweza kufungua mashauri wakati wowote na mahala popote pale walipo.

Akitoa maelezo ya mifumo mbalimbali inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania katika walisilisho lake mbele ya Majaji hao, Afisa TEHAMA, Bw. Mussa Mwinjuma alisema mifumo hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ambapo imewawezesha kutoa huduma kwa haraka kwa kadiri inavyohitajika.

Sambamba na mifumo ya kitaifa inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania, Afisa TEHAMA huyo aliwapitisha Majaji katika mifumo ya ndani inayotumiwa na Mahakama hiyo ambayo ndiyo hasa imeifanya kuwa ya mfano nchini, ukiwemo mfumo wa ukusanyaji taarifa za kumbukumbu tuli “Tanga Record Centre Database-TCRD”.

Alisema kuwa Kanda ya Tanga ilianza kutumia Kanzi data hiyo tangu mwaka 2017 kwa kusajili taarifa za majalada ya mashauri yaliyomalizika kusikilizwa na kupelekwa mahali yalipohifadhiwa kweye kituo cha kuhifadhia kumbukumbu tuli kwa lengo la kumsaidia mtumishi kutambua na kulichukuwa jalada stahiki kwa urahisi mahala lilikohifadhiwa.

Aliongeza kuwa kanzi data hiyo imewarahisishia Majaji na wadau kupata majalada yaliyosikilizwa kwa haraka na urahisi mkubwa pindi wanapoyahitaji kwa madhumuni mbalimbali. Pia Majaji walipitishwa kwenye mfumo unaokusanya taarifa za majalada yanayopokelewa kutoka Mahakama za chini “Lower Court Records” ambao umesaidia kuondosha kadhia ya upotevu wa taarifa za majalada. 

Taarifa zinazokusanywa na mfumo huo ni pamoja na namba ya kesi, majina ya wadaawa, jina la mtumishi aliyepeleka na kupokea jalada hilo. Afisa TEHAMA huyo aliongeza kuwa mfumo huo hutoa ripoti za majadala yaliyorudishwa na ambayo hayajarudishwa katika vituo vyake vya awali.

Majaji hao wapo kwenye mafunzo elekezi yanayoendelea Wilayani Lushoto  ambayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakam Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuwaandaa, kuwapatia uelewa mzuri, kuwajengea uzoefu wakutosha na kuwaweka tayari kuyakabili majukumu muhimu na mzito yaliyoko mbele yao.

Mafunzo hayo ambayo ni muendelezo wa mafunzo mbalimbali yanayoendelea kutolewa na Chuo hicho kwa watumishi wa Mahakama na wadau wa sekta ya sheria nchini yalianza tarehe 31 Agosti, 2022 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba, 2022 chuoni hapo.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakamu Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. John Ubena (aliyesimama) akiwakaribisha Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar waliofanya ziara fupi katika Mahakama hiyo.


Majaji wakifuatilia kwa makini maelezo mafupi kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama hususani matumizi TEHAMA.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Beda Nyaki akitoa maelezo kuhusu shughuli za usajili wa mashauri kwa kutumia TEHAMA zinavyofanyika.
Jaji Victoria Nongwa akichangia jambo wakati wa mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa ziara hiyo.
Afisa TEHAMA, Bw. Mussa Mwinjuma Mussa akitoa maelezo kuhusu mifumo mbalimbali inayotumiwa na Mahakaam ya Tanzania, Kanda ya Tanga.
Majaji wa Mahakama Kuu wakipokea maelezo toka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Beda Nyaki (kulia) walipotembelea Kituo cha zamani cha Utunzaji wa kumbukumbu Tuli.

Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu wakiwa ndani ya chumba cha kisasa cha kutunzia kumbukumbu tuli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni