Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma
Menejimenti
ya Mahakama ya Tanzania imeridhishwa na miradi miwili ya ujenzi wa nyumba za
Majaji na Makao Makuu ya Mahakama Tanzania ilizopo katika maeneo ya Iyumbu na NCC
jijini Dodoma.
Hayo
yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel wakati wa ziara fupi iliojumuisha Menejimenti ya watumishi wa Mahakama
waliotembea maeneo hayo ili kuona ujenzi unavyoendelea.
Alisema
majengo hayo yanatarajiwa kukabidhiwa Desemba 31, 2022 ili yaanze kutumika kama
walivyokubaliana na Wakandarasi.
"Makao
Makuu na haya majengo yanatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2022, naamini Wakandarasi
watatimiza makubaliano yaliyowekwa. Ujenzi wa Makao Makuu umefikia asilimia
zaidi 68 na ujenzi wa nyumba za Majaji wa Mahakama ya Rufani umefikia asilimia
27,"alisema Prof. Ole Gabriel.
Alifafanua
zaidi kuwa wanafanya hivyo kwa lengo la kutimiza ahadi ya Mahakama kuhamia
Dodoma kama zilivyofanya Taasisi na Wizara mbalimbali. Mtendaji Mkuu huyo
alisema kuwa wanatarajia kutumia shilingi bilioni 129.7 hadi kukamilika kwa
ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
"Tunaishukuru
sana serikali kutokana kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa Makao Makuu ya
Mahakama na majengo ya makazi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, tunaamini
Majaji watafanya kazi wakiwa katika mazingira rafiki yanayoendana na kazi
zao,"alisema.
Alisema
nyumba za makazi ya Majaji zikikamilika zitakuwa na uwezo wa kuchukua familia
26 katika jengo mmoja. Naye Msanifu Majengo Rose Nestory aliwasihi wajumbe
kutoka Mahakama ya Tanzania kutokuwa na wasiwasi wowote kwa sababu majengo hayo
yatakamilika kwa wakati uliopangwa.
Alisema
wao kama wasanifu wanaishukuru Serikali kutokana na kutoa ushirikiano katika
ujenzi huo ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa katika suala zima la
ukamilisha nyumba za majaji pamoja na Makao Makuu ya Mahakama.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasimali Watu wa Mahakama ya Tanzania
Beatrice Patrick alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kutokana na usimamizi
mzuri wanaofanya katika ujenzi huo.
Alisema
wao kama wajumbe wa Menejimenti kutoka Mahakama ya Tanzania wameridhishwa na ujenzi
huo, hivyo wanaishkuru Serikali kutokana na juhudi inayofanya ili kuhakikisha
Mahakama hiyo inahamia jijini Dodoma.
Beatrice
alitoa wito kwa wakandarasi hao kutobweteka badala yake waongeze bidii katika
ujenzi wanaofanya ili wakamilishe kwa wakati.
Msanifu Majengo Rose Nestory akitoa maelezo kuhusu miradi ya ujenzi wa nyumba za Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu na Makao Makuu ya Mahakama jana wakati wa ziara ya Menejimenti ya Mahakama kwenye Makao Makuu ya Ofisi zao zinazojengwa.
(Picha
na Tiganya Vincent-JOT)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni