Ijumaa, 16 Septemba 2022

UTEUZI WENU UNATARAJIWA KUONGEZA UFANISI, UBORA WA UAMUZI: JAJI KIONGOZI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Lushoto

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewambia Majaji Wapya waliomaliza mafunzo elekezi ya utayari kuwa uteuzi wao umebeba matarajio kwa Umma, mamlaka ya uteuzi na Mahakama ya Tanzania. 

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo elekezi ya namna bora utendaji kazi wa Majaji leo tarehe 16 Septemba, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto yaliyodumu kwa muda wa wiki tatu, Mhe. Siyani alisema, kwa upande wa eneo la usikizaji wa mashauri ujio wao unatarajiwa kushusha mzigo kazi (workload) kwa kila Jaji. Mtakumbuka kabla ya kuteuliwa kwenu kila Jaji alikuwa na wastani wa mashauri 340 kwa mwaka, kufuatia kuteuliwa na kuapishwa kwenu, idadi hiyo ilishuka mpaka wastani wa mashauri 265.

Kushuka kwa idadi hiyo ya mashauri ambayo kila Jaji anapaswa kuwa nayo ni nafuu kwa Majaji, lakini nini Mahakama na watanzania wanatarajia kuhusu ujio wenu. Wananchi wanasubiri kuona kasi ya usikilizwaji wa mashauri na utoaji wa maamuzi kwa wakati ukiongezeka, wanataraji kuona ufanisi na ubora wa maamuzi ukiongezeka.

“Hata hivyo, kwa sasa na hasa baada ya majaji 3 kustaafu mmoja mwezi uliopita na wawili mwezi Septemba, mzigo kazi kwa kila Jaji umeongezeka kufikia wastani wa mashauri 275 kwa mwaka, kulingana na hali ya Kituo, hiki ndicho kiasi cha chini cha mashauri ambayo mnapaswa kukitarajia mtakapokwenda kwenye vituo vyenu. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na wastani wa mashauri 411 ambayo kila Jaji alikuwa nayo mwaka 2021”, alisema Jaji Kiongozi.

Kwa hiyo mtaona, hata kabla ya uteuzi wenu idadi ya wastani wa mashauri ambayo kila Jaji alipaswa kuwa nayo kwa mwaka, ilipungua. Tafsiri pekee ya kupungua kwa mzigo kazi kabla ya uteuzi wenu, ni kuwa kazi kubwa ilifanywa na Majaji wenzenu.

Kuhusu mlundikano wa mashauri Jaji Kiongozi akasema, kufikia Juni 2022, Mahakama Kuu ya Tanzania, ilikuwa na jumla ya mashauri ya mlundikano, 1433 ambayo ni wastani wa asilimia 10 ya mashauri yote 14,719 yaliyokuwepo kwenye masjala zote za Mahakama Kuu. Mahakama imejiwekea mkakati kuhakikisha inaondokana na mashauri haya ya muda mrefu.

“Kila Kanda na Divisheni ya Mahakama Kuu, ina mkakati wake wa kupambana na mashauri haya. Mtakapokwenda kwenye vituo vyenu hakikisheni mnashiriki utekelezaji wa mikakati hiyo kwa pamoja na mambo mengine; kuyapa kipaumbele mashauri ya mlundikano na kuzuia mashauri mapya yasipevuke na kuwa mlundikano. Kwa kufanya hivyo pekee mtatimiza dira ya Mahakama ya kutoa haki kwa wakati na kujenga imani ya wananchi kwa Taasisi yetu”, alisisitiza Jaji Kiongozi kwa Majaji hao.

Jaji Siyani akawakumbusha Majaji kuwa, ni vyema wakafahamu kuwa mfumo uliorithiwa kutoka kwa wakoloni, umewafanya Majaji kuwa wasikilizaji zaidi na umechangia kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mashauri na hivyo kusababisha mlundikano. Kwa hiyo zama za Majaji kuwaachia wadaawa kuiongoza Mahakama na Majaji kubaki kama wasikilizaji, ni zama zilizopitwa na wakati.

Aidha, Jaji Kiongozi aliwapongeza Majaji wote kwa kuonyesha juhudi kubwa, nidhamu ya hali ya juu na kwa kutambua kuwa watatumia elimu kubwa waliyoipata ili iwasaidie kuwatumikia vema wananchi katika vituo vyao vya kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo alisema, “katika mafunzo haya tumeyaboresha na kuongeza nguvu zaidi katika eneo la utaratibu wa namna bora ya kuendesha mashauri mahakamani “Procedures” kwa upande wa kesi za Madai na Jinai kwa kutumia kesi mbalimbali za mfano ili kuimarisha uwezo wa Majaji”. Aliongeza 

Jaji Kihwelo, akalisifia kundi hilo la Majaji waliomaliza mafunzo kuwa ni wachapakazi, wanakiu ya kupenda kujifunza, wanatoa michango mizuri ya kuboresha kazi zao hasa wawapo darasani, wachangamfu na wanapenda kujamiika. Mahakama ya Tanzania imepata Majaji wazuri watakao kuwa wachapakazi hodari.

Naye, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina akatoa pongezi na shukrani kwa niaba ya Majaji wenzake, alisema walijifunza mambo mengi, elimu waliyoipata ni kubwa kutoka kwa wawezeshaji mahiri na wabobevu. Hivyo mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa sana kwao.

“Tunatoa ahadi ya kutekeleza yote tuliyojifunza wakati wote wa utendaji kazi na utoaji haki kwa wananchi. Msingi mkuu ikiwa ni kusimamia maadili ya ndani na nje ya Mahakama ikizingatiwa kuwa sisi ni Nyara za Serikali”, aliongeza Jaji Mhina.

Jaji Mhina akasema kwa niaba ya Majaji wengine, akatoa ahadi ya kwenda kusikiliza mashauri kwa weledi na kutoa maamuzi ndani ya muda unaokubalika na pia kushiriki kikamilifu katika shughuli za uboreshaji wa huduma za Mahakama unaendelea.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiongea na Majaji wapya waliomaliza mafunzo ya wiki tatu (hawapo pichani) katika ukumbi wa mafunzo, wakati wa kufunga mafunzo hayo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto tarehe 16 Septemba, 2022.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo (aliyenyoosha mikono) akifafaua jambo wakati wa kufunga mafunzo hayo mbele ya meza Kuu ilyoyopo kulia na Majaji waliomaliza mafunzo (hawapo pichani)

Sehemu ya Majaji waliomaliza mafunzo hayo ya wiki tatu wakimsikiliza Mgeni wa heshima Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani) wakati wa hotuba ya kufunga mafunzo hayo.

Sehemu ya Majaji waliomaliza mafunzo hayo ya wiki tatu wakimsikiliza Mgeni wa heshima Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani) wakati wa hotuba ya kufunga mafunzo hayo.

Sehemu ya Majaji waliomaliza mafunzo hayo ya wiki tatu wakimsikiliza Mgeni wa heshima Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani) wakati wa hotuba ya kufunga mafunzo hayo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wapya wanawake mara baada ya kumaliza mafunzo ya wiki tatu, wengine Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Stella Mugasha (wa pili kushoto), Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo (wa kwanza kushoto), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Edward Rutakangwa (wapili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. Ubena Agatho (wa kwanza kulia)

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wapya mara baada ya kumaliza mafunzo ya wiki tatu, wengine Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Stella Mugasha (wa pili kushoto), Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo (wa kwanza kushoto), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Edward Rutakangwa (wapili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. Ubena Agatho (wa kwanza kulia)

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wapya wawili (2) ambao ni alumni (wanachuo wa IJA) mara baada ya kumaliza mafunzo ya wiki tatu, wengine Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Stella Mugasha (wa pili kushoto), Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo (wa kwanza kushoto), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Edward Rutakangwa (wapili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. Ubena Agatho (wa kwanza kulia)

Mkurugenzi wa Mafunzo ya Majaji wapya na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Edward Rutakangwa akieleza jambo wakati wa kufunga mafunzo hayo

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. Ubena Agatho akitoa pongezi kwa Majaji wapya waliomaliza mafunzo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe Latifa Mansoor


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Majaji wenzake wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa wiki tatu 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiendelea na zoezi la akikabidhi vyeti kwa Majaji waliomaliza mafunzo na pichani ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ruth Massamu (kulia) akipokea cheti

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akimkabidhi nishani Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo ikiwa sehemu ya zawadi zilizoandaliwa na Majaji wapya kwa viongozi mbalimbali waliyoshirikiana nao kwa kipindi cha mafunzo hayo.


sehemu ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika hafla ya kufunga Mafunzo ya Majaji Wapya (katikati) ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe, Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mafunzo Bi. Patricia Ngungulu. 

(Picha na Innocent Kansha na Ibrahim Mdachi)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni