Na Innocent Kansha – Mahakama, Lushoto
Jaji
wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija amewaasa Majaji Wapya wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kufuata misingi ya kanuni, Sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa
ili kurahisisha utendaji kazi wa kila siku.
Akizungumza
wakati wa mafunzo elekezi ya Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayoendelea
katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Mwarija
amewasisitiza Majaji kuwa waadilifu na imara wanapotekeleza majukumu yao na pia kuzingatia misingi
ya haki wanapotoa uamuzi katika mashauri.
“Mwananchi
hatarajii kusikia au kuona Jaji anakosea kwa makusudi ama bahati mbaya kwa kuzingatia
mamlaka aliyokasimiwa, hivyo hakuna bahati mbaya kwa mwananchi, mnapaswa
kuzingatia misingi inayokubalika wakati wa kuwasikiliza na kutoa uamuzi ulio sahihi kwa wateja wenu,” aliongeza Jaji Mwarija.
Jaji Mwarija alisema, sheria ni nyingi, kanuni na miongozo mbalimbali inayotumika katika kazi za Majaji hivyo ni wajibu wa kila Jaji kuhakikisha anatimiza jukumu lake kikamilifu kwa kufuata misingi hiyo. Katika hali hiyo Majaji wanapaswa kuzingatia masuala muhimu wakati wa kusikiliza na kuamua mashauri ili kulinda hadhi ya kazi yao.
“Jaji anapaswa kuwa mtu huru wakati wote anaposikiliza na kuamua mashauri, na uhuru huo umeainishwa kwenye sheria mama yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mara kwa mara, katika Ibara ya 107B”, aliongeza Mhe. Mwarija.
"Ili kulinda uhuru wa Mahakama Jaji anapaswa kuwajibika kwa kufuata Katiba na sheria.
Kwa mujibu wa kanuni za Jumuiya ya Madola za uwajibikaji na mahusiano ya
Mihimili mitatu ya dola “Majaji wanapaswa kuwajibika kwa kuzingatia Katiba na
Sheria wanazozitumia kwa uaminifu, kwa uhuru na kwa kuzingatia uadilifu. Kanuni
hii ni msingi unaoleta imani kwa Umma, kwa Mahakama na kuimarisha
umuhimu wa Mahakama kama moja ya mihimili ya dola ikiashiria msingi wa
uwajibikaji kwa umma,” mwisho wa nukuu.
Jaji
Mwarija, pia alielezea njia zinazotumika kulinda matumizi mabaya ya uhuru wa
Mahakama kuwa ni kulinda uhuru wa Mahakama usitumike vibaya, kuna kanuni mbalimbali
za kimaadili zilizoratibiwa na nyingine hazijaratibiwa zinazolinda uhuru huo, kanuni za mwenendo na kanuni za maadili za Maafisa wa Mahakama
zilizoainishwa za mwaka 2020 chini ya kifungu namba 66 (2) (c) cha Sheria ya
Uendeshaji wa Mahakama Sura ya 237 (Judiciary Administration Act Cap. 237).
Sheria
hii inaelezea viwango vya kanuni za kimaadili anavyopaswa kuwa navyo na
kuonyeshwa na Afisa wa Mahakama dhidi yake na kwa wengine, kwa uadilifu, usawa
na kwa kutokuonyesha upendeleo.
Mafunzo
hayo elekezi kwa Majaji ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya mafunzo ya Mahakama ya
mwaka 2019 inayoratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na
Mahakama ya Tanzania kwa watumishi wa Mahakama na Taasisi zingine za nje.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza na sehemu ya Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakati apokutana nao kwenye Mafunzo Elekezi yanayoendelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija (hayupo pichani) akizungumza na sehemu ya Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakati apokutana nao kwenye Mafunzo Elekezi yanayoendelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto
Sehemu ya Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakimsikiliza Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija (hayupo pichani) wakati apokutana nao kwenye Mafunzo Elekezi yanayoendelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni