Jumanne, 6 Septemba 2022

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AELEZA FAIDA ZA TEHAMA

.

Na Castilia Mwanossa

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama imeanzisha Kituo cha Kupokea maoni na malalamiko (Call Center) kwa lengo la kuhakikisha huduma ya utoaji haki inaendelea kuwa ya uwazi, utawala bora na yenye tija ili Mtanzania apate haki yake kwa wakati.

Prof. Gabriel amesema hayo tarehe 5 Septemba, 2022 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Jaji Mkuu Prof .Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitiza uwepo wa uwazi, utawala bora na tija katika  huduma ya utoaji haki kupitia kituo hicho, ili kuweza kupokea taarifa moja kwa moja kutoka kwa wananchi kwa saa 24.

"Mahakama ina mifumo takribani tisa ambayo imeleta faida kubwa kwa kuwa taarifa zote sasa zinapatikana kiurahisi kupitia mfumo wa Ofisi Mtandao kuliko hapo awali ambapo matumizi ya makaratasi yalikuwa makubwa na imesaidia kupunguza gharama kubwa ya malipo kwa watumishi kwa sababu ilihitaji watu wengi na ilichukua muda mwingi na matumizi makubwa ya karatasi ambapo hivi sasa hayapo,” alisema Prof.
Gabriel.

Akizungumzia kuhusu  mfumo wa Mahakama ya Tanzania unaochapisha maamuzi, sheria na kanuni(TanzLII) Mtendaji huyo alisema  mfumo huo umekuwa wa  kwanza duniani kutembelewa na watu wengi kwa asilimia 82.7 ambapo nchi inayofatia ina asilimia 2.4, ukilinganisha na mifumo mingine ulimwenguni kote.

 Alisema mfumo huo unafuatiliwa kwa kuwa ni mfumo unao onyesha hukumu kwa uwazi pindi inapotolewa na ina uwezo wa kuonyesha kesi zingine takribani 30 zinazoendelea duniani.

Mtendaji huyo aliitaja baadhi ya mifumo mingine ya Mahakama kuwa ni Ofisi Mtandao (E-office), TanzLII,  Mfumo wa Kusajili na Kuhufadhi  kwa njia ya Kielektroniki (JSDS),  Mfumo wa Kutambua Majengo yote yanayomilikiwa na Mahakama kidijitali(J-Mapping) na Mfumo wa Kuwasajili na Kuwatambua Mawakili (e-Wakili), alisema mifumo hiyo imeleta matunda  kwa  Mahakama kwa kuwa imeiwezesha kutekeleza majukumu yake kiurahisi na kuwafikia wananchi.

Alitoa wito kwa viongozi wengine mbalimbali kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na waandishi wa habari tarehe 5, Septemba 2022 ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni