Na Castilia Mwanossa (SAUT)
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu, Mhe. Elimo Massawe amesema kitendo cha mtuhumiwa
kuachiwa huru na kukamatwa tena kinatokana na mazingira yanayozunguka usikilizaji
kabla au baada ya kuhitimishwa kwa shauri husika, ikiwemo uwasilishaji wa ushahidi
mahakamani.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo tarehe 2 Septemba, 2022 ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Naibu
Msajili huyo amesema kuwa pale upande wa mashtaka unaposhindwa kuthibitisha
shitaka bila kuacha shaka yoyote hupelekea Mahakama kumwachia huru mshitakiwa.
Amesema katika mazingira hayo mshitakiwa hawezi kukamatwa tena na kushitakiwa
kwa makosa yale yale aliyokuwa nayo hapo awali.
Hata hivyo, Mhe. Massawe
alifafanua kuwa Mahakama inaweza kumwachi huru mshitakiwa kwa baadhi ya mashitaka
pale upande wa mashtaka unaposhindwa kukamisha upelelezi ndani ya siku 60.
Amebainisha kuwa katika mazingira hayo mshitakiwa anaweza kukamatwa tena na
kushitakiwa kwa makossa hayo hayo pale upande wa mashitaka unapokamilisha
upelelezi.
Kadhalika, Naibu Msajili huyo
alieleza kuwa pale upande wa mashtaka unapoamua kuondoa shitaka linalomkabili
mshitakiwa kabla ya shauri dhidi yake halijafikia mwisho wa kusikilizwa, mfano
baadhi ya makosa ambayo hayana ukomo wa siku 60 kama ya uhukumu uchumi, Mahakama
inaweza kumwachia huru mshitakiwa na anaweza kukamatwa tena na kufunguliwa
mashitaka hayo hayo.
“Ili mtu aambiwe hana
hatia ni lazima kwa shauri la jinai liwe limesikilizwa na Mahakama ijiridhishe ushahidi
uliopelekwa mahakamani haukidhi matakwa ya kisheria, huyo ndiye anayeambiwa
yuko huru na hana hatia na hawezi kukamatwa tena. Kuna wengine wanaachiwa huru
bila Mahakama kutamka kuwa hana hatia, tafsiri yake ni kwamba shauri lake
halijasikilizwa kufika mwisho.
“Kifungu namba 225 cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinataja aina ya mashauri ya jinai kuanzia siku
yamefunguliwa kwa muda wa siku 60 upelelezi usipokamilika Hakimu ana mamlaka ya
kuondoa shauri hilo mahakamani na kumwachia huru mshitakiwa, lakini haioneshi
hana hatia. Jamhuri ikienda kukamilisha upelelezi, basi mshitakiwa atakamatwa
tena na kushitakiwa kwa kosa lilelile,” alisema.
Akizungumzia mchakato wa usajili wa mashauri
mahakamani, Mhe. Massawe amesema kila
Mahakama kuanzia ngazi ya Mahakama ya Mwanzo huwa na utaratibu wake. Alisema
katika Mahakama ya Mwanzo, mlalamikaji anapofika mahakamani huwasilisha madai na
kujaza fomu na utaratibu ukikamilika shauri litasajiliwa na mhusika hupewa hati
ya wito kwa upande wa pili.
Naibu Msajili huyo ameeleza
kuwa mchakato wa usajili wa shauri la madai katika Mahakama ya Wilaya au
Mahakama ya Hakimu Mkazi unaanzia kwa mlalamikaji kuandika hati ya madai kwa
kuzingatia mamlaka ya Mahakama dhidi ya lalamiko lake na kuiwasilisha mahakamani
ama kwa nakala ngumu au laini kupitia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
ambao kwa sasa ndio unaosisitwa na Mahakama ya Tanzania kutumika.
Amesema mfumo huo umerahisisha
usajili, hivyo mtu anaweza kusajili shauri lake popote alipo bila ya kufika
mahakamani na pale ambapo Hakimu Mfawidhi pamoja na watu wa masijala wakiridhika
baada ya kupitia nyaraka zinazohusika kama zimekamilika na kukidhi matakwa ya kisheria,
Mahakama itapanga tarehe ya kuanza mchakato wa kusikilizwa kwa shauri hilo.
Kwa upande wa mashauri ya
jinai katika Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi,
Naibu Msajili huyo alisema mchakato huanzia kituo cha polisi na baadaye hati ya
mashitaka huandaliwa ambayo huletwa mahakamani na baada ya kusajiliwa shauri hilo
litakuwa tayari kusikilizwa.
Mhe. Massawe pia ameeleza
kuwa mashauri yanapofika Mahakama ya Mwanzo hayatakiwi kuzidi miezi sita na kwa
sasa hayazidi miezi mitatu yanakuwa yameisha, lakini kwa Mahakama ya Wilaya na Mahakama
ya Hakimu Mkazi hutakiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kwa mashauri ambayo Mahakama
hizo zina mamlaka ya kuyasikiza.
Kwa upande wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Naibu Msajili huyo alibainisha kuwa mashauri hutakiwa kumalizika kwa wastani wa kipindi cha miezi 24.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu, Mhe. Elimo Massawe (katikati) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni