Na Stephen Kapiga, Mahakama Mwanza
Wananchi
wa Kata Buswelu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wameishukuru Mahakama ya
Tanzania kwa kuwasogezea huduma ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)
kilichojengwa katika eneo hilo huku wakikiri kunufaika na uwepo wake ikiwemo kuziwezesha
familia takribani 100 kupata maji safi na salama yanayopatikana katika kisima cha
Kituo hicho kilichozinduliwa hivi karibuni.
Akizungumza
na Diwani wa Kata ya Buswelu, Bi. Sarah Ng’wani aliyetembelea Kituo hicho hivi
karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza alimueleza
Diwani huyo namna ambavyo Mahakama zilipo ndani ya jengo la ‘IJC’ zinavyoshirikiana
na jamii inayowazunguka.
“Kwakuwa
sasa tuna uhakika wa kupata maji mengi na yanayokidhi mahitaji yetu ndani ya
jengo hili na bado tunabaki na ziada, tumeona ni bora pia maji haya kugawa kwa
wananchi wanaoishi nyumba za hapa jirani na IJC na maji haya yatatumika kwa
matumizi ya nyumbani tu na si kwa jili ya kufanyia biashara” alisema Mhe. Kahyoza.
Nao
wananchi wanaozunguka kituo hicho jumushi kwa nyakati tofauti waliwashukuru Viongozi
wa Mahakama Kanda ya Mwanza kwa kuwakumbuka na kuweza kuwasaidia kuondokana na
kadhia hiyo kwani maji ndio kila kitu katika maisha na kazi za kila siku
majumbani.
“Kwa
kweli bila maji huwezi kufanya jambo lolote lile ukiwa nyumbani. Kwa jambo hili
waliloamua Mahakama kutusaidia maji bure bila ya kulipa chochote kwa kweli tunawashukuru
sana Viongozi wa Mahakama kwani inaonesha kweli wanatoka katika mazingira na
familia ambazo kwao kushirikiana na watu ni jambo la muhimu na sio kujitenga na
jamii kwa sababu ya nafasi zao ndani ya Mahakama” alisema Mzee Sufiani Juma.
Ikumbukwe
kuwa eneo la Buswelu limekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ya
bomba hivyo kufanya kuwa ngumu kupata maji kwa familia ambazo hazina huduma ya
maji ya kisima. Kufuatia kadhia hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel alifanya zoezi la uchimbaji wa kisima chenye urefu
wa mita 180 na kufunga pampu ya kusukuma maji kwa kutumia nguvu ya jua ili
kuwezesha upatikanaji wa maji ndani ya jengo la IJC Mwanza kwa gharama nafuu.
Akitoa
shukrani zake kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo alipotembelea Kituo hicho hivi
karibuni, Diwani wa Kata ya Buswelu, Bi. Sarah Ng’wani aliipongeza Mahakama kwa kuweza
kuikumbuka jamii inayozunguka jengo hilo.
“Kwanza
kabisa kwa niaba ya wananchi wangu tunaishukuru Mahakama ya Tanzania, Jaji Mfawidhi
wa hapa na Mtendaji kwa kuweza kudumisha uhusiano huu na wananchi. Hii
inanifanya nijivunie kutoa eneo hili la kujenga jengo hili kwani hapo awali
eneo hili lilikuwa limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule, lakini niliposikia
uhitaji wa Mahakama kuhitaji eneo niliweza kuishawishi ‘ODC’ (Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya) ya Ilemela na hatimaye eneo hili kutolewa kwa Mahakama” alisema Bi. Sarah.
Naye,
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Mwanza alimtembeza Diwani huyo katika ofisi zote
zilizopo katika jengo hilo na kumuelezea namna kila Ofisi inavyotenda kazi
katika jengo hilo jambo ambalo lilimvutia diwani huyo.
“Kwakweli
nimefurahia mazingira namna yalivyo bora, kuanzia Mahabusu hasa Mahabusu ya
watoto jinsi yalivyo rafiki kwa watoto na hivo kufanya kila ofisi kuwa rafiki
kwa watumiaji na wateja wake. Hii kwa kweli inatupa imani sisi jamii kweli haki
inaonekana inaenda kutendeka ndani ya jengo hili,” aliongeza Diwani huyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza (mwenye suti nyeusi) akiwa katika picha ya pamoja na Diwani wa Buswelu, Bi. Sarah Ngw'ani (mwenye nguo ya kitenge) aliyetembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Kata ya Buswelu mkoani Mwanza. Wengine ni Viongozi Mahakama wanaofanya kazi katika Kituo hicho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza (kushoto) akimfafanulia jambo Diwani wa Buswelu, Bi Sarah Paul Ng’wani (katikati) alipotembelea na kukagua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Mwanza hivi karibuni.
Hongera sana Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kwa kuweka uhususiano mzuri na jamii inayozungukama Mahakama. Kitendo tu Cha kutoa maji kwa wananchi ni utu wa kutosha kwa mwanadamu . Mungu ibariki Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mwanza na viongozi wake kwa ujumla pamoja na watumishi wake.
JibuFuta