Ijumaa, 28 Oktoba 2022

MSAJILI MKUU AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI, UTAMADUNI WA MAHAKAMA

Na Mwandishi wetu-Mahakama ya Tanzania

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewahimiza watumishi wa Mahakama kuzingatia maadili na kuenzi utamaduni wa Mahakama, ikiwemo kuvaa mavazi (dress code) yanayokubalika na yaliyoelekezwa na nyaraka mbalimbali za utumishi wa umma.

Mhe. Chuma alitoa agizo hilo jana tarehe 27 Oktoba, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha Mahakama ya Mwanzo Manundu iliyopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

"Watumishi wa Mahakama wanapaswa kuvaa mavazi ambayo yanazingatia utamaduni wa Mahakama na mwongozo wa mavazi kwa watumishi wa umma, wanapokuwa kazini wakitekeleza majukumu yao ya utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi,"alisisitiza.

Mhe. Chuma alisema kuwa watumishi wa Mahakama wanatakiwa kuwa kioo katika jamii katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuepuka kuvaa mavazi yasiyostahili sehemu za kazi. Msajili Mkuu huyo wa Mahakama alitoa zawadi ya vazi la skafu kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama hiyo.

Aidha, Mhe. Chuma aliwahimiza watumishi hao kufuatilia taarifa mbalimbali zilizoko katika Mpango Mkakati wa Mahakama ili waweze kuufahamu kwa ustandi na kuwa tayari kuutekeleza kikamilifu.

Alisema kuwa sanjari ya kuelewa Mpango huo, watumishi wa Mahakama wanapaswa kuendelea kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Aliwataka watumishi wa Kituo hicho kuhakikisha wanamaliza mashauri kwa wakati na kuepuka mlundikano kwa kufanyakazi kwa bidii na kwa ufanisi.

Katika ziara hiyo, Msajili Mkuu huyo alibaini uchakavu, upungufu wa vitendea kazi na ufinyu wa jengo la Kituo hicho, hali inayolazimu kukosa sehemu ya kuhifadhia majalada na vielelezo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kituo cha Mahakama ya Mwanzo ya Manundu jana tarehe 27 Oktoba, 2022.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kushoto) akimkabidhi skafu Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Zaituni Haassan (kulia).
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwakabidhi skafu baadhi ya watumishi jana tarehe 27 Oktoba, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha Mahakama ya Mwanzo Manundu.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Zaituni Haassan (kulia) jana tarehe 27 Oktoba, 2022 wakati wa ziara yake.
Baadhi ya watumishi wakiwa tayari kumpokea Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (hayupo katika picha) jana tarehe 27 Oktoba, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mahakama ya Mwanzo Manundu.

Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Manundu wakiwa wamevaa skafu ambazo walikabidhiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa katika ziara kwenye Mahakama hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni